Saturday, September 27, 2008

chibiriti alipokaribishwa dar
Ndugu yangu kadidi,


Aisee nashukuru safari yangu ya kurudi huku Cesena, Italy, ilimalizika salama na jamaa wote nilikuta wazima. Wanawasalimia sana wadau wote na kutoa pole ya mfungo kwa wote wasio makobe.

Nakutumia picha hii ya mzinga niliolishwa na daladala pale magomeni siku ya pili tu toka nilipofika Dar. Unaweza kuita karibu mgeni maana jamaa alikuwa amechomekewa na daladala ingine, sasa wakati anarudi rivasi, mie ndio nakatiza na hilo gari dogo. Nikasikia kochooo!


Bahati nzuri hakuna aliyejeruhiwa ila gari iliumia vibaya mlango wa nyuma kama unavyoona. Majeraha yangu makubwa ni hasara niliyoipapa kwani huyo dereva wa daladala alinikomalia na kusema yeye hana kosa ati mie ndiye niliyemgonga.

Zogo liliendelea hadi kituo cha polisi magomeni ambako jamaa alikazania kuwa mimi ndiye mwenye makosa, akisema sheria inatamka wazi kwamba aliyegonga kwa nyuma ndiye mwenye makosa. Nilijitahidi kujieleza, wapi. Ah, nikaachana nao na kurudi nyumbani. Kesho yake nikapeleka gari kwa fundi wa mabodi akaninyooshea na kupiga rangi. Nilitumia visenti kibao.


Namalizia kwa kutoa wito kwa wenzangu wanaorudi nyumbani wawe wangalifu sana na madaladala. madereva wake wengi hawana adabu na sheria za barabarani wao hawazingatii kabisa, tena hata mbele ya askari trafiki.

Ni mimi yuleyule
B. Chibiriti

No comments: