Tuesday, September 9, 2014

TAARIFA ZILIZOSAMBAA KUACHIWA KWA BABU SEYA NA PAPII KOCHA NI UZUSHI - JESHI LA MAGEREZA TANZANIA

Hivi sasa kuna taarifa zimesambaa kupitia Ujumbe mfupi wa simu (SMS) na mitandao ya kijamii zikihusisha kuachiliwa huru kwa wafungwa wawili wanaotumikia Kifungo cha Maisha gerezani. Wafungwa hao wanaotajwa ni Nguza Vicking (Maarufu kwa jina Babu Seya) na Johnson Nguza (Maarufu kwa jina la Papii Kocha).

Napenda kuufahamisha Umma wa Watanzania kuwa taarifa hizo zote zilizotolewa kupitia njia hizo ni za Uongo na uzushi mkubwa na zinalenga kuipotosha jamii kwani wafungwa hao wapo gerezani na wanaendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha Maisha gerezani kwa mujibu wa Sheria.

Jeshi la Magereza nchini linatoa onyo kali kwa watu kujiepusha na uhalifu huo na linawataka wale wote wanaotumiwa ujumbe wa aina hiyo waepuke kuusambaza ujumbe huo kwa wengine bali waufute, kwani kuendelea kuusambaza ni kosa kisheria.

Aidha, Jeshi la Magereza linaendelea na uchunguzi wa kina ili kuwabaini wanaosambaza ujumbe huo likishirikiana na Vyombo vingine muhimu kwa lengo la kuwakamata wahalifu hao ili mkondo wa Sheria uchukue nafasi yake.

Imetolewa na;
Lucas Mboje, Mkaguzi wa Magereza,
Afisa Habari wa Jeshi la Magereza,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
DAR ES SALAAM.
Septemba 8, 2014

Tuesday, March 25, 2014

Laptop ya Nguvu za Jua

Maonyesho ya wiki ya kimazingira yanayojulikana kama ‘Inhabitants Week in Green’ yanamalizika rasmi leo, lakini hayakupita bila ya kugusa hisia zetu sisi wapenzi wa gajeti, kampuni ya Fujitsu wameshusha laptop sahihi kabisa inayoendana na mazingira ya nchi kama Tanzania, hili linatokea tukiwa bado hatujasahau kwamba si muda mrefu uliopita kule Zanzibar umeme ulikatika kwa muda wa kiasi cha miezi mitatu. 

Kilichotuvutia sisi wa Gajetek katika laptop hii ambayo haikutolewa habari zake za kutosha kwa sasa ni mambo mawili. Mosi, laptop hii haihitaji chaja kabisa kwani inajichaji na paneli zenye kutumia nguvu za jua (Solar panels) zilizo kwenye eneo linalokaa kibodi na nyuma ya skrini. Pili, ni kuwa laptop hii bado imeweza kuwa nyembamba na yenye kuvutia mno kimaumbile huku ikiwa imezungukwa na paneli ya kioo (glass panel).
Hivyo umeme ukatwe mwaka mzima, wewe unaendelea na kazi zako bila ya kujali lolote kwa vile laptop hii inajichaji ikiwa inatumika na hata ikiwa haitumiki. Hivi karibuni Apple wamejigamba kuwa sasa wanaelekea kwenye hali ya ‘cable free’ wakitumia kauli ya kimatangazo (slogan) ya kata waya lakini hii ndio laptop ambayo inakupa uhuru wa kuondokana na miwaya kikweli, kwani gajeti za Apple bado zinahitaji waya ili kuzichaji.
Fujitsu hawakutoa fununu zozote juu ya ni lini laptop hii itakuwa tayari kwa mauzo au ina vianisho halisi vya aina gani. Laptop hii inatumia paneli aina ya photovoltic katika kuichaji na hivyo imeondoa mchukizo wa kisura na upana paneli za nguvu za jua za kizamani. Pamoja na uchache wa habari zake laptop hii imevutia wengi, ingawa kwa wenzetu wa nchi zilizoendelea ni suala la kimazingira tu, kwetu sisi wa nchi zinazoendelea ni suala linaloendana na hali halisi ya maisha yetu, yaani kukosa umeme kwa maeneo ya vijijini na kukatika katika kwa umeme kwa maeneo ya mijini. Tunamalizia kwa kusema hii ni laptop halisia kwa mazingira ya Tanzania.

Hacker Geohot Aajiriwa na Facebook

 
Geohot, hacker maarufu aliyejailbrake iPhone ameajiriwa rasmi na Mark Zuckerburg, yaani Facebook. Hacker huyu ambaye pia aliwahi kushitakiwa na Sony kwa shughuli za uchakachuaji baada ya kuihack PS3 na kuruhusu watumiaji kuweza kutumia DVD feki za kuchakachua. Facebook hawakuthubitisha Geohot atafanya kazi gani kwenye kampuni hiyo. Hacker huyu ambaye anatumia majina mbali mbali katika shughuli zake pevu ikiwa ni pamoja na million75, mil, dream na hax0r ameshafanya fujo nyingi sana katika ulimwengu wa kompyuta. Kijana huyu kwa sasa ana umri wa miaka 22 tu.
Jina alilopewa na wazazi wake ni George Francis Hotz. Katika kazi za karibuni kabisa alizofanya hacker huyu ni kujailbraik iPhone na iPod Touch kwa kutumia njia aliyoiita Blackra1n na pia kuifungua (sim unlock) simu hiyo kwa njia aliyooiita blacksn0w.
Alipoihack PS3 Sony walimpandisha kizimbani, hata hivyo mwezi wa nne mwaka huu Sony na Geohot walikubaliana nje ya mahakama na hivyo Sony kufuta kesi ile. Geohot alipewa sharti la kuto-hack tena PS3 ili kufutiwa kesi hiyo, sharti ambalo alilikubali. Ajira hii kwa dogo huyu ni hasara kubwa kwa wachakachuaji kwani watakosa mengi pale atakapotingwa na kazi za Facebook. Hacker huyu huwa hana noma, baada ya kufanya mambo yake huyaweka wazi kabisa katika tovuti yake ambayo ni www.geohot.com 
Kwa sasa kwenye tovuti yake ameacha ujumbe mfupi wa ajabu, waweza kwenda kuangalia mwenyewe.