Thursday, September 25, 2008

Kesi Ya Ajali Ya Wangwe Kuanza Okt 7

Kesi ya Deus Mallya (27), aliyenusurika katika ajali mkoani Dodoma Julai mwaka huu iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, inatarajiwa kuanza kusikilizwa Oktoba 7 huku mfanyabiashara huyo akiendelea kusota rumande. Upande wa mashitaka uliifahamisha mahakama jana kuwa kesi hiyo iko tayari kwa kusikilizwa.
Mallya ambaye alifikishwa tena mahakamani jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Thomas Simba, aliieleza mahakama kuwa haelewi chochote kuhusiana na dhamana yake kwa kuwa yeye yuko rumande. “Mheshimiwa Hakimu kwa kuwa nipo ndani sijui chochote kinachoendelea kuhusiana na dhamana yangu,” alisema Mallya mahakamani hapo.
Alieleza hayo mara baada ya kuulizwa na Hakimu mbele ya Mwendesha Mashitaka Mrakibu Msaidizi wa Polisi Polycarp Urio ni nini kinachoendelea kuhusiana na dhamana yake kwa kuwa ipo wazi. Awali alijitokeza mtu mmoja ambaye jina lake halikufahamika na mahali alipotoka na kusema kuwa angewasilisha hati ya nyumba baada ya mahakama kuahirishwa, lakini baada ya kumalizika kwa kesi zote mahakamani hapo, mtu huyo hakuwa na barua ya utambulisho wala hati ya nyumba. Mdhamini anayetakiwa kumdhamini Mallya ni mkazi wa Dodoma, mwenye barua ya uthibitisho kutoka kwa viongozi wa eneo analoishi na dhamana ya Sh milioni tano au mali yoyote isiyohamishika yenye thamani hiyo.Mallya anakabiliwa na shitaka la kuendesha gari bila leseni, kwa mwendo kasi na kusababisha kifo cha Wangwe.
Habari Kwa Hisani Ya Habarileo

No comments: