Mkapa ajitangaza kuwa ni "Mwadilifu"
RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa amevijia juu vyombo vya habari nchini kwa kile alichodai vimekuwa vikimnukuu vibaya na kupotosha ukweli wa mambo. Bw. Mkapa alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki,katika sherehe za Jubilee ya kutimiza miaka 100 ya Usista ya Kanisa la Mtakatifu Benedict lililopo Ndanda, wilayani Masasi. Katika sherehe hizo Bw.Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi, alitumia fursa hiyo kukanusha habari zilizochapishwa na kutangazwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni kuwa ameamua kuachana na siasa na kwamba sasa anajihusisha zaidi na masuala ya dini. Alisema kuwa hana nia ya kujihusisha na masuala ya dini zaidi kama kuwa kiongozi wa kanisa na kwamba yeye ni muumini sawa na waumini wengine, hivyo hakuna tofauti kati ya awali na anavyojihusisha sasa na masuala hayo nakusisitiza kwamba vyombo vya habari vilimnukuu vibaya. "Nilikuwa Chato, mkoani Kagera, baada ya hapo nilipitia Mwanza…niliporudi nyumbani mwanangu akaniuliza baba siku hizi unataka kuwa kiongozi wa kidini?...Nikamuuliza kulikoni? ...akanijibu magazeti yameandika hivyo," alisema Bw.Mkapa. "Kweli siku ya Pili nikakuta katuni kwenye gazeti ikiwa imebeba vitabu na Biblia…sasa nataka kuwahakikishia kuwa sitaki uaskofu wala siuhitaji…mimi ni mcha Mungu wa kawaida kama nilivyokuwa awali” alisisitiza Rais huyo mstaafu Hivi karibuni vyombo vya habari nchini vilimnukuu Bw. Mkapa wakati alipokuwa akizungumza na waumini wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Francisco Exaveri lililopo jijini Mwanza, kuwa ameamua kuachana na siasa na sasa anajihusisha zaidi na dini. "Enzi za mimi kujihusisha na siasa zilikoma pale nilipokabidhi madaraka kwa Serikali ya Awamu ya Nne mwaka 2005,” alinukuliwa Bw. Mkapa na vyombo vya habari, akiwaambia waumini wenzake katika Ibada hiyo jijini Mwanza. Sambamba na hilo, Bw. Mkapa aliwasifu watawa hao kwa kuinua kiwango cha elimu kwa mikoa ya Kusini na Tanzania kwa ujumla, sambamba na jitihada zao za kuboresha huduma za afya hasa katika kutoa tiba na elimu kuhusu ugonjwa wa ukoma uliokithiri eneo hilo. "Mimi binafsi nawashukuruni sana maana ujio wenu una mchango mkubwa kwa kiwango cha elimu niliyoipata ambayo imeniwezesha kuwa kiongozi mwadilifu wa nchi hii … na haya ni matunda yenu," alisema Bw. Mkapa ambaye alisoma Shule ya Sekondari Ndanda iliyokuwa inamilikiwa na kanisa hilo. Awali Nkuu wa wilaya hiyo, Bw. Said Amanzi, alisema serikali inatambua mchango wa watawa hao hasa katika kuboresha afya za jamii kwa kutoa tiba kupitia Hospitali ya Ndanda na kuahidi kuwa itapewa ruzuku ili kusaidia uendeshaji wake.
Habari Kwa Hisani Ya KLH News
Habari Kwa Hisani Ya KLH News
No comments:
Post a Comment