Tuesday, September 23, 2008

RC Abdulaziz Aipongeza Zain Kusaidia Yatima


Abdulaziz Kizito: Meneja wa Zain Kanda ya Kaskazini, Kizito Millambo (kushoto) akikabidhi vyandarua kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mohamed Abdulaziz vilivyotolewa na Zain kwa watoto yatima wa kituo cha Abu-Abdulrahman, jijini Tanga wikiendi. Katikati ni Meneja wa Huduma za Jamii wa Zain, Tunu Kavishe na wa pili kulia ni Mlezi wa Abu-Abdulrahman Orphan Centre, Hassan Waziri.

RC Abdulaziz aipongeza Zain kusaidia yatima vyandarua
Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mohamed Abdulaziz amepongeza mchango wa Kampuni ya simu ya mkononi ya Zain kwa kuisaidia Serikali katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.

Abdulaziz alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki wakati akipokea msaada wa vyarandua 89 vilivyotolewa na Zain kwa ajili ya watoto yatima 102 wa kituo cha Abu-Abdulrahman, katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Kola Prieto jijini Tanga.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema ugonjwa wa malaria kwa sasa unashikilia rekodi ya kuua watu wengi zaidi nchini kuliko hata UKIMWI, na akatoa mwito kwa wananchi kuendelea kutumia vyandarua ili kujikinga na ugonjwa huo.

"Napenda kuishukuru Zain kwa msaada wa vyandarua kwa watoto hawa yatima... nanyi watoto napenda kuwaasa kwamba, vitunzeni vyandarua hivi mlivyopewa na Zain, navyo vitawatunza. Mkivitunza, mtawapa Zain shauku ya kuzidi kuwasaidia katika mambo mengine," alisema Abdulaziz.

Aliishukuru Zain kwa kujali wasiojiweza, kwani kutoa ni moyo na si utajiri, hivyo akatoa mwito kwa Zain inapopata nafasi iendelee kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu, afya, yatima na waathirika wa UKIMWI.

Aliwaomba watoto hao yatima walioko chini ya taasisi ya Answar Muslim Youth Centre yenye maskani yake Makorola mjini Tanga, wazidi kuiombea dua njema Zain ili iendelee kusaidia jamii. Zain pia iliwapatia futari watoto hao yatima.

Baada ya kukabidhi vyandarua hivyo, Meneja wa Huduma za Jamii wa Zain, Tunu Kavishe alisema Zain itaendelea kuisadia jamii katika miradi mbalimbali ikiwemo elimu, na akabainisha hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, kampuni hiyo itakuwa imetumia zaidi ya sh. bilioni 1 kwa ajili ya kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

Mbali ya Tunu, pia Zain iliwakilishwa na Meneja wa Zain Kanda ya Kaskazini, Kizito Millambo, Mratibu Maendeleo ya Biashara wa Zain Tanga, Karugaba Rugaimukamu na Mhandisi Mitambo wa Zain Tanga, Abdallah Abdallah.

Mlezi wa Abu-Abdulrahman Orphan Centre, Hassan Waziri aliishukuru Zain kwa msaada huo, na akasema wataiombea dua njema kampuni hiyo izidi kufanikiwa. Waziri alisema kituo hicho hivi sasa kinalea watoto zaidi ya 100 wanaosoma chekechea, shule za msingi, sekondari na vyuo, wakiwamo wasichana na wavulana.

No comments: