Friday, September 26, 2008

Mgao Wa Umeme Waishtua Serikali


Serikali kesho itatoa tamko kuhusu mgao wa umeme ulioanza juzi, baada ya wahandisi wa umeme kutoka Marekani kuifanyia uchunguzi mitambo ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Songas iliyopata hitilafu na kusababisha kuwepo kwa mgao huo. Wakati hayo yakiendelea, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewataka Watanzania kuwa wavumilivu na kuvuta subira wakati serikali ikilishughulikia tatizo hilo. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Pinda, alisema kuwa serikali inalishughulikia kwa haraka tatizo hilo ili kuondoa kero kwa wananchi na athari zinazoweza kujitokeza. Alisema kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Songas ina uwezo wa kuzalisha umeme wa kiwango cha megawati 180, lakini kutokana na hitilafu hiyo umeme unazozalishwa kwa sasa ni megawati 140, hivyo kusababisha upungufu wa megawati 40. Pinda, alisema kutokana na tatizo hilo kutakuwa na mgao wa umeme nchi nzima muda wa jioni na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu na kuvuta subira wakati serikali ikilishughulikia. Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alieleza kuwa mitambo iliyoharibika ni mitatu kati ya sita ya kampuni ya Songas na kwamba hali hiyo iligundulika wakati mafundi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) walipokuwa wakiifanyia ukaguzi. Alisema kuwa, baada ya hitilafu hiyo kugundulika, mafundi hao walitoa taarifa kwa kampuni iliyotengeneza mitambo hiyo ya General Electrical (GE) ya Marekani, ambayo nayo baada ya kupata taarifa hiyo iliagiza mitambo hiyo izimwe ili itume mafundi wake kwa ajili ya kufanya uchunguzi na tathmini ya hali halisi ilivyo. ``Siyo kwamba mitambo hii imeharibika kabisa na haifanyikazi, kwani hata wakati ikizimwa ilikuwa inaendelea kufanyakazi kama kawaida, lakini baada ya mafundi wa GE kutaarifiwa kuhusu tatizo lililoonekana wameshauri izimwe ili waweze kufanya uchunguzi,`` Ngeleja alifafanua. Waziri huyo aliongeza kuwa mafundi hao watawasili nchini leo na kwamba baada ya kufanya tathmini na kutoa ripoti yao, serikali kesho itatoa tamko rasmi kuhusu nini kifanyike kutegemea na ukubwa wa tatizo lenyewe. Hata hivyo, Ngeleja alisema ana imani kuwa tatizo hilo siyo kubwa sana na kwamba mgao wa umeme utakuwa si wa muda mrefu kwani serikali inalifuatilia kwa karibu suala hilo. Juzi Tanesco ilitoa taarifa ya kuharibika kwa mashine za kuzalisha umeme za Songas na kusababisha upungufu wa umeme wa zaidi ya megawati 40, hali iliyolilazimu shirika hilo kuanza kutoa umeme kwa mgao kwa maeneo yanayopata nishati hiyo kupitia gridi ya taifa. Taarifa ya mgao wa umeme iliyotolewa jana na Tanesco na kusainiwa na Meneja wa Mawasiliano wa shirika hilo, Badra Masoud, ilieleza kuwa kuanzia jana maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam hayatakuwa na umeme kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 4:30 usiku, isipokuwa maeneo nyeti tu kama Ikulu, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Benki Kuu na viwandani. Ratiba hiyo inaonyesha kuwa leo mikoa saba itakumbwa na na mgao wa umeme. Mikoa hiyo ni Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Shinyanga, Morogoro na Tanga kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 4:30 usiku na kwamba maelezo kuhusu mgao yatazidi kutolewa kadri siku zinavyokwenda. Kabla Tanesco kutangaza kuwa hakutakuwepona mgao wa umeme kwa taasisi na maeneo nyeti jana, Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) lilieleza wasiwasi kuwa uamuzi wa kuanza kutoa umeme kwa mgao kwa maelezo kuwa hali hiyo ingeweza kuathiti sekta ya viwanda. Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Mtendaji wa CTI, Christine Kilindu ,alipozungumza na Nipashe. Alisema mgawo wa umeme kila unapotokea athari zake ni kubwa katika sekta ya viwanda. Kilindu alisema, mwaka 2006 uliathiri sekta hiyo ingawa hakuweza kutoa takwimu sahihi za athari hizo. Alipoulizwa ni hatua gani ambazo wangeweza kuchukua kama hali hiyo ingejitokeza alisema, angewasiliana kwanza na wananchama wake. Mwaka 2006 nchi ilikumbwa na tatizo hilo baada ya kupungua kwa kina cha maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme ya Mtera, Nyumba ya Mungu na Kidatu. Uhaba huo wa umeme ndio ulioilazimisha serikali kuingia katika mkataba na Kampuni ya Richmond ya Marekani kwa ajili ya kufua umeme wa dharura wa megawati 100. Hata hivyo, baadaye mkataba huo uliiingiza serikali katika hasara na kashfa kubwa, baada ya kampuni hiyokushindwa kuzalisha umeme na kubainika kuwa ilikuwa kampuni bandia. Chini ya mkataba huo wa miaka miwili, Tanesco ilijikuta ikilazimika kuilipa Richmond na baadaye mrithi wake Kampuni ya Dowans kiasi cha Sh. milioni 152 kila siku hata kama hazikuzalisha umeme.
SOURCE: Nipashe

No comments: