Monday, September 15, 2008

Wana Rukwa acheni imani za
Kishirikina-Pinda
Pichani Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akizungumza na baba yake Mzazi kijijini kwake Kibaoni wilayani Mpanda akiwa katika ziara ya wilaya hiyo,Septemba 12,2008.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
---------
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wakazi wa mkoa wa Rukwa kuachana na imani za ushirikina pindi wanapoumwa na badala yake waende hospitali mara moja ili wawahi kupatiwa tiba sahihi.juzi mchana mchana wakati akizungumza na wananchi wa mji wa Sumbawanga waliofika hospitali ya mkoa huo kushuhudia akipokea na kukabidhi vifaa vya upasuaji vyenye thamani ya sh.milioni 25 vilivyotolewa na kampuni ya VODACOM Foundation.
“Wana-Rukwa wenzangu ninawaomba tuache mambo ya sing’ang’a(waganga wa kienyeji)na badala yake tuamke hospitali iwe ndiyo kimbilio lete kama daktari akisema kashindwa ujue huo ni ugonjwa mkubwa kama vile kansa ambao sote tunajua hata uende kwa sing’ang’a hawezi kuutibu”,alisema.
Alisisitiza kwamba dawa pekee ya kuondokana na tatizo hilo ni elimu. Aliwataka wazazi wawapeleke watoto wao shule kwani wakishaelimika hawawezi kuamini tena mambo ya mizimu Alimshukuru Mkuu wa VODACOM Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,Bw.Jackson Kiswaga kwa msaada huo ambao umejumuisha meza ya kisasa ya upasuaji,machela ya kubebea wagonjwa na vifaa vingine vya aina nane.
Aliyaomba mashirika mengine yaige mfano huo kwa kusaidia katika nyanja mbalimbali.Akijibu risala ya Mganga Mkuu wa Mkoa Dk.Saduni Kabuma Waziri Mkuu alisema anatambua tatizo la uhaba wa watumishi tangu akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI lakini aliwapongeza watumishi waliopo kwa kazi yao nzuri licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu.Aliahidi kulifuatilia suala hilo.
Hata hivyo,Waziri Mkuu Pinda aliwashauri viongozi wa mkoa wa Rukwa waangalie jinsi ya kujitangaza kwenye vyuo mbalimbali nchini kama mkakati wa kupata watumishi watakaokaa. Alisema kufanya hivyo,kutatoa fursa kwa wahitimu watarajiwa kupata taarifa sahihi kuhusu mkoa huo na hivyo kuwawezesha kuvutiwa kufanya kazi katika mkoa huo bila hofu tofauti na hali ilivyo sasa.
“Tatizo kubwa linalowakabili watumishi wanaopangiwa kufanya kazi katika mkoa huu ni kukosa taarifa sahihi wengi hawaji kwa sababu hawajui huko wanakoenda kuna nini..lakini leo huu wakikuona Mganga Mkuu unaongea mbele yao umejaajaa au RAS pale(Katibu Tawala wa Mkoa) lazima waatamini kuwa Rukwa kuna hali tofauti na inavyoelezwa na watu wengi”alisema huku akishangiliwa.
Mapema akisoma risala yake Dk.Kabuma alisema hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa watumishi na kuongeza kuwa upungufu huo ni janga kubwa kwa utoaji huduma bora za afya. Akitoa mfano alisema hospitali hiyo inahitaji madaktari na waganga wasadizi 35 lakini waliopo sasa ni 16 tu Maafisa Wauguzi wanaohitajika ni 105 lakini waliopo ni 38 wakati Wauguzi wanaohitajika ni 150 lakini waliopo ni 49 tu.
Alisema hospitali hiyo yenye vitanda 370 ina uwezo wa kulaza wagonjwa 300 kila siku na ndiyo inatumika kama hospitali ya rufaa kimkoa kwa kuhudumia wakazi wa mkoa mzima wapatao milioni 1.3 Alisema katika mwaka huu wa fedha wana mpango wa kununua gari la wagonjwa ambalo thamani yake ni sh.milioni 150 ili liweze kusaidia kupeleka wagonjwa wa rufaa katika mkoa wa Mbeya.
Waziri Mkuu ambaye yuko wilayani Mpanda kwa ziara ya siku 10,atahutubia mikutano ya hadhara wilayani humo katika maeneo ya Inyonga,Ilunde,Mapili,Nsekwa na Urwira.Maeneo mengine atakapohutubia wananchi ni Itenka‘A’Mamba,Igalukilo,Majimoto,Mwamapuli, Ilalangulu na Karema.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
13/09/2008

No comments: