Na Profesa Leonard K. Shayo
HISTORIA inaonesha kwamba, kila jambo baya lililotendwa na kundi moja la binadamu, kwa kundi jingine la binadamu, halafu likatokomezwa bila ridhaa ya pande zote mbili, jambo hilo lilirudi kimamboleo!
Isitoshe, jambo linalorudi kimamboleo linakuwa na athari kubwa zaidi ya ilivyokuwa mwanzo! Kwa mfano, ukoloni ulitokomezwa bila ridhaa ya wakoloni, lakini ukarudi kama ukoloni mamboleo! Lengo la ukoloni wa mwanzo lilikuwa ni kupora rasilimali za nchi zilizotawaliwa na wakoloni! Lakini, imedhihirika kwamba, nchi nyingi zilizojikwamua kutoka ukoloni wa kutawaliwa moja kwa moja na wageni, sasa zinahamisha rasilimali nyingi zaidi na kwa kasi zaidi chini ya ukoloni mamboleo!
Siyo siri kwamba, hata waliokuwa wanapinga kutokomezwa kwa ubaguzi wa rangi, leo wanasherehekea uporaji wa rasilimali kutoka nchi kama Tanzania zilizokuwa mstari wa mbele kupigana vita vya kutokomeza ubaguzi wa rangi! Zipo tetesi kwamba, wanajilaumu ni kwa nini hawakukubali ubaguzi wa rangi ukaonekana kuisha mapema! Tunasema �ukaonekana kuisha mapema� maana ukweli ni kwamba ubaguzi wa rangi haujaisha huko ulikokuwa, na baya zaidi ni kwamba sasa unasambaa hata katika nchi zilizokuwa zinapinga ubaguzi huo! Kilichoondolewa ni mabango ya kutangaza kuwepo kwa ubaguzi wa rangi! Tunaweza kusema kwamba, sasa kuna ubaguzi wa rangi mamboleo!
Kama ilivyokwa ukoloni mamboleo, utumwa mamboleo unatumikisha akili badala ya mwili! Akili zilichukia utumwa wa mwili enzi zile za kuwauza mababu zetu huko Bagamoyo, Mikindani na Zanzibar, maana akili zilikuwa hazijachukuliwa utumwani! Lakini sasa utumwa mamboleo unazichukua akili utumwani! Je, ni nani atapiga vita utumwa wa akili?
Vita vya kutokomeza utumwa wa mwili vilifanikiwa kwa sababu watumwa waliunga mkono vita vile! Yaani akili zao zilikuwa hazijaingia utumwani, na ndiyo maana zikauchukia utumwa. Hii ni tofauti na utumwa mamboleo unaozichukua akili utumwani, na hivyo kuwafanya wahusika wafurahie kuwa watumwa.
Walioanza harakati za kutokomeza utumwa wa mwili walikuwa watu huru, kwa maana ya kutokuwa watumwa. Vivyo hivyo, wanaotakiwa kutokomeza utumwa mamboleo ni watu walio huru, kwa maana ya akili zao kutokuwa utumwani. Tatizo ni kwamba, wapinzani wakuu wa kutokomeza utumwa mamboleo ni watumwa wenyewe. Hapa ndipo panakuwa na vita vikali, maana wanaharakati wa kutokomeza utumwa mamboleo watajikuta wakipingwa na wafanyabiashara wa utumwa mamboleo, watumwa wenyewe, na wamiliki wa watumwa hao, ambao ni matajiri wa kukifu.
Vita vya kutokomeza utumwa mamboleo vinakuwa vikali kupindukia, kutokana na ukweli kwamba, watumwa mamboleo wana nguvu za kijeshi, kiuchumi, na kisiasa. Isitoshe, wanunuzi wa watumwa mamboleo wana nguvu za kijeshi, kiuchumi, na kisiasa pia. Siyo rahisi kuishi katikati ya makundi haya mawili, yaani kundi la watumwa mamboleo, na kundi la wanunuzi wa watumwa mamboleo. Kwa maneno mengine, siyo rahisi kutokomeza utumwa mamboleo. Ndiyo maana tunanena kwamba, mbinu za kisayansi zinahitajika kutokomeza utumwa mamboleo.
Nchi nyingi tajiri zinafanya biashara ya utumwa mamboleo katika nchi maskini. Zinatumia mbinu za kisayansi kuwateka kwanza viongozi wengi wa nchi maskini. Mbinu hizo zinaweza kujumuisha matoleo yaitwayo misaada, kwa makosa, pamoja na rushwa za vitisho, fedha, mali, na ahadi za kusimikwa tena madarakani. Zinaweza kujumuisha vitisho vya aina mbali mbali, na mikataba yenye ladha ya sukari nje lakini ndani ikiwa imejaa pilipili.
Kama vile mgonjwa anavyokubali kunywa dawa yoyote anayoambiwa itamponya, hata kama ni chungu, vivyo hivyo viongozi wa nchi maskini wanapokea ushauri wowote wanaoambiwa utatokomeza umaskini katika nchi zao. Isitoshe, kama ilivyo mila potofu kwa wagonjwa wa nchi maskini kupenda dawa kutoka nchi tajiri, vivyo hivyo mila potofu imewafanya viongozi wengi wa nchi maskini kupenda ushauri kutoka nchi hizo tajiri. Yaani mfanyabiashara ya utumwa mamboleo anampa mtumwa mtarajiwa ushauri wa jinsi ya kutekwa vizuri, na yeye anapokea ushauri huo kwa mikono miwili.
Siyo sahihi kuwalaumu watumwa mamboleo kwa sababu hawaelewi kwamba wametekwa utumwani. Pia siyo sahihi kutafuta ushirikiano wa watumwa hao katika harakati za kuwakomboa, maana watafungua kesi ya uhujumu wa uchumi. Kinachotakiwa ni kubuni mbinu madhubuti za kisayansi za kuwatoa utumwani. Mbinu hizo ni vyema zikashirikisha mahakama ili zisigeuzwe kuwa uvunjifu wa sheria, ama ili zisitungiwe sheria za kuzipiga marufuku.
Barabara walizotumia watumwa wa mwili zilipita kwenye mapori yenye wanyama wakali, na ndiyo maana akina Mwinyi Upate walibeba bunduki kusindikiza misafara ya watumwa. Lakini barabara za utumwa mamboleo zinapita kwenye mapori ya akili za binadamu wenye uchu wa kutokomeza umaskini wa nchi zao kwa njia za mkato, ambazo hazipo. Ndiyo maana akina Mwinyi Upate wa utumwa mamboleo wanabeba bunduki, za mipango hewa ya kutokomeza umaskini, kwa ajili ya kusindikiza misafara ya watumwa mamboleo waliobebeshwa mizigo ya rasilimali za nchi zao maskini kupeleka nchi tajiri.
Katika vita vyovyote, lengo la kila upande ni kumteka kiongozi wa adui. Hilo likitendeka, vita vinaisha, na upande uliotekwa unasalimu amri kwa kukubali kushindwa. Kwa mtazamo huo, kiongozi wa nchi akishatekwa kama mtumwa mamboleo, wafuasi wake wanakuwa hatarini kuwa mateka wa utumwa mamboleo. Tunasema hivyo kwa sababu, sera za kiongozi ndizo sera za wafuasi wake. Hapa ndipo tunaona faida kwa nchi maskini kukumbatia kwa dhati na kwa uadilifu utawala wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, maana kama kiongozi wa chama tawala atakuwa mateka wa utumwa mamboleo, kuna uwezekano finyu wa mkombozi wake kuibuka kutoka kwenye chama chake. Katika hali hiyo, mkombozi anaweza tu kutoka kwenye chama cha siasa mbadala.
Hata kama kiongozi wa leo katika nchi maskini hajatekwa utumwani mamboleo, wananchi walio huru na utumwa huo hawana budi kuchukua hatua za kuupiga vita, maana umaskini wa nchi yao ni ushahidi kwamba wapo viongozi waliotangulia waliokuwa watumwa mamboleo. Tutakuwa na kosa gani kama tukisema, kiongozi anayekaribisha wawekezaji ambao, hatimaye wananyanyasa wafanyakazi wazalendo, ni mtumwa mamboleo? Tutakuwa na kosa gani kama tukisema kwamba, kiongozi anayeridhia mikataba ya kuwaruhusu wageni kupora rasilimali za nchi yake, ni mtumwa mamboleo? Tutakuwa na kosa gani kama tukisema kwamba, kiongozi anayejitajirisha kwa kukumbatia ufisadi ni mtumwa mamboleo?
Kwa bahati mbaya mno, kuna njia moja tu ya kupiga vita utumwa mamboleo, nayo ni kujenga uchumi imara kwa kutumia vyema sayansi na tekinolojia. Kwa nchi kama Tanzania, ni lazima tuchukue hatua zifuatazo. Kwanza tumlinde mkulima kwa kuhakikisha kwamba haingii kwenye makucha ya walanguzi wanaoingia vijijini kununua mazao yake kwa bei ya kutupa. Pili ni lazima tumlinde mkulima kwa kuhakikisha kwamba, kilimo chake ni cha kisasa, na kinafuata kanuni za uchumi, yaani mkulima awezeshwe kulima kwa faida. Tatu, tushirikiane kimataifa na nchi zilizo tayari kutuwezesha tuwe na viwanda vingi. Nchi nyingi za aina hiyo ni za kusini, kwa mfano China. Huko Ulaya kuna nchi kama Italia ambayo iliwahi kujenga mtambo mkubwa kuliko yote duniani, kwa ajili ya uzalishaji wa umeme wa maporomoko ya maji, Amerika ya Kusini.
Kwa upande wa Tanzania, tunapongeza hatua iliyochukuliwa na serikali ya awamu ya nne kuunda wizara maalum kwa ajili ya kuendeleza sayansi na tekinolojia. Lakini tunahoji kwamba, kuunda wizara ni kitu kimoja, na kufanikisha malengo ya wizara ni kitu kingine. Kuanzishwa kwa wizara ya sayansi, tekinolojia na elimu ya juu, na kuanzishwa kwa tume ya sayansi na tekinolojia kulishangiliwa enzi zile. Je, kuna lipi la kujivunia kutokana na iliyokuwa wizara ya elimu ya juu, sayansi na tekinolojia? Je, kuna lipi la kujivunia kutokana na kuwepo kwa tume ya sayansi na tekinolojia kwa zaidi ya miongo miwili?
Harakati za kufanikisha mapinduzi ya sayansi na tekinolojia katika nchi siyo lelemama, na kwa vyovyote vile haziwezi kuzaa matunda kwa nchi zilizozamishwa kwenye utumwa mamboleo, unaodhihirishwa na tabia ya kupenda kusaidiwa samaki waliokaushwa badala ya mbinu za kufuga na kuvua samaki. Hatua ya kwanza ya kuondokana na utumwa mamboleo ni kwa wanasiasa kukaa na wanasayansi kwa ajili ya kupanga na kutekeleza mikakati ya kufanikisha mapinduzi ya sayansi na tekinolojia. Mikakati ya kisiasa isiyowaridhisha na kuwashirikisha wanasayansi wote itagota. Je, ni nchi gani iliyofanikisha mapinduzi ya sayansi na tekinolojia kwa kuunda wizara?
Kwa kuhitimisha, tunazishauri nchi zilizozamishwa kwenye utumwa mamboleo, ambao kwa wanaothamini utu ni umalaya wa kisiasa, ziukatae hata kama unaambatana na migao ya fedha nyingi za kigeni. Hayati baba wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikerwa na umalaya wa kisiasa.
Profesa Leonard K. Shayo ni Mtaalam wa Hisabati na Program za Kompyuta
Mobile: 0754 288 179 E-mail: shayolk@yahoo.com.
1 comment:
[url=http://sapresodas.net/][img]http://vioperdosas.net/img-add/euro2.jpg[/img][/url]
[b]windows vista skins, [url=http://vioperdosas.net/]office 2003 activation bypass[/url]
[url=http://vioperdosas.net/]adobe photo editor software[/url] educators discount software www macromedia com software flash fl4about
for software in canada [url=http://vioperdosas.net/]recommended educational software[/url] where to buy softwares
[url=http://sapresodas.net/]can i sell used software[/url] coreldraw 11 manual for mac user
[url=http://sapresodas.net/]software for cheap[/url] buy pocket pc software
poker software for sale [url=http://vioperdosas.net/]macromedia software flash fl4about[/url][/b]
Post a Comment