Saturday, March 15, 2008

Kikwete, hofu yetu imeanza kuonekana

Na Julius Samwel Magodi

NAKUMBUKA hivi karibuni baada ya Rais Jakaya Kikwete kuamua kuvunja Baraza la Mawaziri kutokana na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujizulu, nilijadili katika safu makosa ambayo alifanya kuwa na kikosi cha mawaziri ambao baadhi yao hawakufaa hata kupewa wadhifa wa afisa mtendaji wa kata.

Kwa ujumla nilijaribu kumtahadharisha kwamba kama hatakuwa makini katika uteuzi wa baraza jipya ipo hatari akalazimika kulivunja tena na kuunda serikali mpya hivi karibuni.

Nilimtahadharisha achague mawaziri kutokana na uwezo wao, uandailifu wao, walioko tayari kujitoa sadaka kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na si kuwateua kutokana na urafiki mkubwa alionao au kumteua waziri kutokana na jinsi alivyomsaidia kwenye kampeni za urais.

Naamini Rais Kikwete ambaye ni mpenzi wa kusoma habari mbalimbali katika karibu magazeti yote, alipata rai yangu kwake. Hata hivyo baada ya kutangaza baraza lake la mawaziri sikuridhishwa na uteuzi wa baadhi ya mawaziri wake.

Sisi wananchi ndio tunaofanya kazi na hawa mawaziri, hatukuridhishwa kabisa na uteuzi wa mawaziri karibu wanne, tunajua kabisa kwamba hawa walichaguliwa si kutokana na utendaji wao wa kazi, bali kutokana na sababu nyingine ikiwamo ukaribu na Rais Kikwete.

Mmoja wa mawaziri hao ambaye baadhi ya wananchi hawakuridhia kabisa uteuzi wake ni Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya.

Wananchi walikuwa na sababu nyingi ya kuwa na wasiwasi na uteuzi wa Kapuya kuchukua nafasi hiyo. Moja; wanamjua sana waziri huyu alipokuwa katika wizara hiyo katika serikali ya awamu ya tatu jinsi alivyovuruga masuala ya kazi na yale ya michezo.

Wizara iligeuka kuwa ni sehemu ya kuibua vurugu migogoro ya wafanyakazi na kwenye michezo badala ya wizara kuwa ni sehemu ya kukuza na kusimamia michezo ilibadilika kuwa ni sehemu ya kuchochea mizozo katika vilabu na hata katika Shirikisho la Soka Tanzania (wakati huo Chama cha Soka Tanzania-FAT).

Ni kutokana na hali hiyo, ndiyo maana baadhi ya watu ambao wana uchungu na nchi hii walitamka wazi wazi kumpiga Rais Kikwete kwa uamuzi wake wa kumteua Kapuya kurudi katika wizara hiyo.

Kwa hakika wananchi nikiwamo mimi hatuna kinyongo na wala hatumwonei wivu Kapuya kuteuliwa kuwa waziri lakini tunachohoji ni uwezo wake wa kuwatumikia Watanzania katika wadhifa huo aliopewa.

Ingawa uteuzi huo uliwafanya watu wengine kuanza kupunguza imani na Rais wetu, baadhi ya watu wenye msimamo wa mlengo wa kati walisema kuwa Profesa Kapuya apewe muda anaweza kuwa amebadilika na akaweza kuchapa kazi kuliko zamani kutokana na uzoefu alionano katika wizara hiyo.

Kama kawaida ya Watanzania hilo likaisha tukaendelea na shughuli zetu huku, tukishangazwa na hatua ya serikali kupokea fedha zilizochotwa kwa njia ya wizi kutoka katika Mfuko wa Madeni ya Nje Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na watu bila ya kuwachukulia hatua wahusika.

Kwa hakika suala hili kwa kiasi kikubwa linashangaza na linashtua kuona kwamba hivi sasa Tanzania mwizi wa hela za umma amegeuzwa kuwa mfalme ambaye anawekewa zulia jekundu anaporejesha fedha alizoiba kama vile analeta hela za kuikopesha serikali! Ebo!

Huu upuuzi tunaoufanya kamwe hauwezi kufanyika katika nchi nyingine yoyote duniani. Huu ni mtihani mwingine mgumu kwa Kikwete, kama atashindwa kuamru kuwekwa hadharani majina ya watu wanaorejesha fedha basi heshima yake ambayo ilikuwa imeanza kurejea kwa wananchi itashuka mno na wananchi tutaamini kwamba rais anajua mchezo huu mchafu unavyochezwa.

Wakati Watanzania tunaendelea kuhoji uhalali wa serikali kushindwa kuwakamata watu walioiba fedha za EPA, Kapuya wiki hii aliibuka na mpya ya kuanza upya majadiliano baina ya waajiri na waajiriwa wa sekta binafsi kuhusu mishahara mipya ambayo yalishajadiliwa na kufikia tamati.

Hatua hiyo ya Kapuya ndiyo ambayo imenifanya nikumbuke malalamiko ya baadhi ya Watanzania kuhusu uteuzi wake kushika wadhifa huo.

Kilichonifanya nikumbuke malalamiko ya wananchi ni ukweli kwamba sasa Kapuya badala ya kuweka mambo sawa sasa ameamua kuharibu kabisa kuhusu mfumo wa malipo ya mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binfasi.

Nasema anavuruga zaidi kwa sababu waziri aliyepita katika wizara hiyo, John Chiligati alikuwa amefikia tamati kuhusiana na suala hilo, na kufanya marekebisho pale yalipohitajika.

Kutangazwa kwa mishahara mipya ilikuwa faraja kubwa kwa wafanyakazi wengi wanaofanyakazi katika sekta hiyo nchini kwa ukweli ni kwamba wengi wanalipwa Sh 30,000 kwa mwezi ambazo zinaishia katika nauli ya kwenda kazini.

Hata hivyo, wakati wafanyakazi katika sekta hiyo wakifurahia kupanda kwa mishahara ghafla waajiri wengi katika sekta hiyo hususan wenye viwanda walipinga ongezeko hilo na kuamua kuanza kupunguza wafanyakazi wakidai kuwa gharama za uendeshaji ni kubwa mno.

Pingamizi hilo la waajiri lililokwenda sambamba na kupunguza wafanyakazi lilimfanya waziri Chligati kusikiliza kilio chao, na kukubali kupitia upya na hivyo kupunguza kima cha chini katika sekta.

Bado waajiri katika sekta hii walikuwa wajanja, waliendelea kulia kwamba bado kima hicho ni kikubwa ingawa wengi walikubali kuwa kulipa kiasi hicho cha mshahara.

Wakati wafanyakazi katika sekta hii wanaendelea kupata mishahara mipya ya kadri ya makubaliano, licha ya amalalamiko lukuki, Profesa Kapuya kaibuka na hili la kuunda tume kuchunguza suala la mishahara.

Swali ambalo ninajiuliza kwamba Kapuya anataka tume yake ifanye kitu gani wakati mwezake Chiligati alishafanya utafiti kwa muda mrefu kujua kima cha chini kinachopaswa kulipwa wafanyakazi katika sekta binafsi.

Rais Kikwete hofu yetu ya kumteua Kapuya kuchukua wizara hiyo sasa ndio hii imeanza kuonekana.

Mwandishi wa Safu hii ni Mhariri wa Habari Maalum. Anapatikana kupitia baruapepe, juliusmagodi@yahoo.com simu 0754 304336

Tuma maoni kwa Mhariri

No comments: