Wednesday, March 26, 2008

Comoro yakombolewa !!!!


Comoro yakombolewa

Majeshi ya Umoja wa Afrika yanayoongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na jeshi la Shirikisho la Comoro jana yalifanikiwa kukikomboa kisiwa cha Anjouan kwenye operesheni ambayo haikupata upinzani.

Operesheni hiyo iliyopewa jina la `Demokrasia Comoro` ilianza majira ya alfajiri jana.

Kanali Mohamed Bakari aliyekuwa akikiongoza kisiwa hicho kimabavu baada ya kujitangazia utawala mwenyewe mwezi Julai mwaka jana, anadaiwa kutorokea katika kisiwa cha Mayotte ambacho kiko chini ya Utawala wa Ufaransa.

Taarifa za Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, zilisema jana kwamba Kanali Bakari alionekana akiwa amevalia nguo za kike katika pilikapilika za kutafuta upenyo wa kutoroka kisiwani Anjouan kwa kutumia boti.

``Kanali Bakari ameonekana katika kijiji cha Sadanpoini ambako inaaminika ametoroka kwa kutumia mashua ndogo hadi kisiwa cha jirani cha Mayotte,`` alieleza msemaji wa serikali ya Comoro, Abdourahim Bakari jana.

Habari zilisema kuwa Ikulu ya kisiwa cha Anjouan ilikuwa imetelekezwa huku askari wa vikosi vya Comoro na AU wakipewa amri ya kumsaka Kanali Bakari popote alipojificha.

``Nimeliamuru jeshi la Comoro na nchi marafiki kusaidia kuleta hali ya amani ili Anjouan iweze kuongozwa kwa kuzingatia utawala wa sheria,`` BBC lilimkariri Rais wa Shirikisho la Visiwa vya Comoro, Ahmed Mohamed Sambi akisema jana.

Operesheni ya jana iliendeshwa na askari wa Shirikisho la Comoro, Sudan na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Taarifa za Reuters zilisema kwamba vikosi vya Comoro na AU vilianza operesheni hiyo alfajiri jana ambapo pamoja na mambo mengine vililenga kumtia mbaroni Kanali Bakari ambaye alipata mafunzo ya kijeshi nchini Ufaransa na baadaye kukitwaa kisiwa hicho kwa mapinduzi mwaka 2001.

Katika operesheni hiyo vikosi vya Tanzania vilipewa jukumu la kukamata uwanja wa ndege, bandari na kasri la rais ambapo majeshi ya Sudan yalipewa jukumu la kudhibiti kituo cha redio na televisheni.

``Kisiwa chote cha Anjouan kipo chini ya usimamizi wa majeshi yetu,`` Meja Ahmed Sidi aliwaambia waandishi wa habari katika kisiwa jirani cha Moheli jana.

``Hadi sasa hakuna taarifa zozote za mtu aliyekufa au kujeruhiwa kutokana na operesheni yetu ingawa wanamgambo wote wa Kanali Bakari wamekimbia na bado hatujamkamata hata mmoja,`` alisema kamanda huyo.

Kutokana na kukatika kwa mawasiliano yote ya simu inasemekana kwamba ilimsaidia Kanali Bakari kukimbia.
Anjouan ambayo ilipata uhuru mwaka 1975 kutoka Ufaransa inakadiriwa kuwa na watu 700,000 hadi sasa.

Afisa mmoja wa Ikulu ya Comoro alisema jana kwamba operesheni ya jana alfajiri ilihusisha askari wa jeshi la AU 400 wakati jeshi hilo tayari limeshapeleka askari 1,350 kutoka JWTZ na Sudan huku lengo lilikuwa na kuwa na jumla ya askari 1,800 ikijumuisha Comoro na Senegal. Nchi ya Senegal haikupeleka askari na mpaka sasa hakuna sababu zilizotolewa.

Baadhi ya wachunguzi wanasema kwamba vikosi vya AU na Comoro havikutarajiwa kukutana na ushindani mkubwa katika operesheni ya jana huku ushindi huo ukionekana kutoa sifa kwa AU kuendelea na operesheni nyingine za kulinda amani nchini Sudan na Somalia. Halikadhalika, wachunguzi wengine wanaichukulia operesheni hiyo kuonyesha udhaifu wa kujitwalia maeneo kutokana na mipaka ambayo iliwekwa na wakoloni.

Serikali ya Shirikisho la Comoro inamtuhumu Kanali Bakari kwa uasi wake wa kujitangazia madaraka mwenywe kimabavu huku naye akidai kwamba anatetea uhuru wa kisiwa cha Anjouan kujitawala chenyewe kuliko kupata uhuru.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Comoro ilisema jana kwamba Rais Sambi, ambaye pia ni mfanyabiashara wa Kiislamu na mzaliwa wa Anjouan amedhamiria kuitisha uchaguzi huru kisiwani humo mapema iwezekanavyo.

Msemaji wa serikali ya Comoro alisema kwamba operesheni ya jana kwanza iliutwaa mji mkuu wa Anjouan, Mutsamudu na miji mingine ya Domoni na Ouani kwa kutumia vikosi ambavyo viliingia kwa kutumia boti za kijeshi.

Taarifa iliyotolewa na serikali ilisema kwamba kulikuwa na kurushiana risasi kwa muda mfupi kati ya vikosi vya Comoro vikishirikiana na vya AU dhidi ya askari wa Kanali Bakari kwenye mji wa Ouani na baadaye kutwaliwa kwa mji mkuu wa Mutsamudu.

Msemaji wa serikali ya Comoro alisema jana kwamba baadhi ya askari walikuwa wamejichimbia kijiji anakotoka Kanali Bakari kijulikanacho kama Barakani kilichopo umbali mfupi kutoka mji mkuu wa Anjouan.

``Baadhi ya askari wetu wamepewa amri ya kumtafuta popote alipo ingawa tunajua kwamba katika miezi ya hivi karibuni alikuwa halali nyumbani kwake kutokana na hofu,`` alieleza msemaji huyo wa Ikulu.

Mkazi mmoja wa Anjouan, Aboulatuf Mohamed aliliambia Reuters kwa njia ya simu ya setalaiti kwamba mapigano hayo yalianza mapema alfajiri jana.

``Operesheni ilianza saa 10.00 alfajiri ambapo jeshi la Comoro na AU liliuteka mji wa Domoni na baadaye kuchukua bandari na uwanja wa ndege,`` alisema Mohamed ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa kikundi kimoja cha wanaharakati kisiwani Anjouan.

Akiongea na waandishi wa habari juzi kwenye kambi ya majeshi ya Tanzania kisiwani Moheli, Mkuu wa vikosi vya AU, Brigedia Jenerali, Daniel Chacha Igoti, alisema lengo la majeshi ya Tanzania kushiriki kwenye operesheni hiyo ni kuwarejeshea wa-Comoro demokrasia.

``Kama mjuavyo Comoro ni jirani zetu ni ndugu zetu na ni waafrika wenzetu, hivyo kumetokea matatizo hapa ya kidemokrasia na majeshi yetu yakishirikiana na Sudan yamekuja kuwasaidia,`` alisema Brigedia Jenerai Igoti.

Akitangaza vita kupitia redio ya taifa ya Comoro, Rais Sambi, alisema anamshukuru rais Jakaya Kikwete na rais wa Sudan kwa kupeleka vikosi vya kusaidia kurejesha kisiwa hicho cha Anjouan kwenye muungano wa visiwa vya Comoro unaojumuisha pia kisiwa cha Moheli.

Historia inaonyesha kuwa visiwa hivyo vimekumbwa na mapinduzi ya kijeshi mara 19 na jaribio moja lilifeli tangu nchi hiyo ipate uhuru wake toka kwa wafaransa mwaka 1975.

Baadhi ya wakazi wa kisiwa cha Moheli kilicho jirani kabisa na kile cha Anjouan, wamemlaumu kiongozi aliyekitangazia madaraka, Kanali Mohammed Bakari kwa kuwasaliti wenzake na kuanza njama za kujitenga.

Bendera ya taifa ya visiwa hivi inaonyesha alama ya nyota nne ikimaanisha muungano huo una visiwa vinne, kikiwemo kile cha Mayotte, ingawa wakazi wa kisiwa hicho waliamua kuendelea kuwa chini ya Ufaransa.

Maisha ya wakazi wa visiwa hivi ni duni ambapo wachambuzi wa masuala ya kisiasa hapa wamedai kuwa yanachangiwa zaidi na kutokuwepo kwa utulivu wa kisiasa.

Inaelezwa kuwa kisiwa cha Mayotte ambacho kiko chini ya Ufaransa kimepiga hatua kubwa ya kimaendeleo ambapo lengo ni kuvishawishi visiwa vingine virejee kwenye ukoloni.

No comments: