Saturday, March 29, 2008

Mgogoro wa maiti: Wakristo, Waislamu sasa kwenda mahakamani

Na Jackson Odoyo

SIKU moja baada ya kutokea vurugu za kugombea maiti kati ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu na kisha Jeshi la Polisi kuingilia kati kwa kuchukua maiti hiyo kuirudisha katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyamala, pande zote mbili zimeamua kwenda makahamani.

Wakizungumza na Mwananchi Jumapili jana kwa nyakati tofauti waumini wa dini hizo wamesema, watakwenda kufungua kesi katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu ili kudai haki ya kuuzika mwili huo.

Ibrahimu Msumari ambaye ni Shemeji wa Marehemu, Paul Goriam (40) alisema watakwenda kufungua kesi katika Mahakama ya Kisutu Machi 31 mwaka huu, ili kudai maiti hiyo aliyosema ndio wana haki ya kuizika.

Msumari alisema wao ndio ndugu wa damu wa marehemu, hivyo hakuna shaka yoyote kuhusu hilo na wala hakuna atakaye pinga kwamba marehemu hakuwa ndugu yao.

Alisema sababu nyingine inayowaruhusu kuuzika mwili huo ni kuwa marehemu alikuwa Mkristo safi.

Msumari alisema marehemu alizaliwa katika familia ya wakristo mwaka 1968, akalelewa katika familia hiyo mpaka alipofariki dunia na kwamba, japo mwaka 2004 alibadili dini na kuwa muumini wa dini ya kiislamu lakini bado alikuwa analelewa katika familia hiyo ya wakristo.

Alisema marehemu aliamua kurudi katika dini aliyozaliwa ya kikristo mwaka 2006 na kubatizwa tena kwa kufuata kanuni na taratibu zote za kikristo.

Msumari alisema mara baada ya marehemu kutubu dhambi zake na kuwa Mkristo, aliendelea kutekeleza imani ya dini hiyo.

�Ninashangaa kuona wenzetu wa dini ya kiislamu wanadai kuwa, marehemu alikuwa muumini wao lakini kipindi chote alipoumwa hatukuwaona hata kuja kumletea panado iweje leo hii waseme marehemu alikuwa muumini wao?,�alihoji Msumari.

Naye Imamu wa Msikiti wa Swafa, Othman Njama alisema yeye akiwa kama Imamu wa msikiti aliokuwa anaswali marehemu, ndiye mwenye dhamana ya mwili wa marehemu kuanzia kipindi cha uhai wake hadi mauti yalipompata.

Imamu Njama alisema kutokana na dhamana aliyokabidhiwa kwa mujibu wa misingi ya dini ya kiislamu, wako katika majadiliano kati yake na kamati iliyoundwa kushughulikia suala hilo.

Alisema moja ya majadiliano ambayo wanafanya ni kuamua kesi hiyo ikafunguliwe mahakama gani, japo kulingana na uzito wa kesi wanatarajia kufungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Imamu huyo alisema mbali na kufungua kesi hiyo wana imani ya kushinda kesi hiyo kwa sababu mpaka marehemu anafariki dunia alikuwa muumini wa kiislamu katika Msikiti huo wa Swafa na yeye ndiye aliyekuwa Imamu wake.

No comments: