Tuesday, March 18, 2008

MAENDELEO Dewji aipa Singida bil. 1/-


Zatumika kwa miradi ya maendeleo
Shule sasa gumzo, maji bwerere Mwenyekiti wa CCm mkoani Singida Hamisi Nguli akihutubia wakati wa mkutano Mkuu maalum wa Wilaya ya Singida mjini ambapo mbunge wa jimbo hilo Mohamed Dewji alitoa taarifa ya utendaji kazi katika miaka miwili ya Ubunge.

MBUNGE wa Singida Mjini, Mohammed Dewji, amelipatia jimbo lake miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya sh bilioni moja.

Dewji, mfanyabiashara maarufu nchini anayemiliki kampuni ya Mohammed Enterprises, aliyasema hayo juzi kwenye Ukumbi wa Sekondari ya Mwenge mjini hapa, alipokuwa anatoa taarifa ya miaka miwili ya ubunge wake, mbele ya umati wa WanaCCM waliohudhuria Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Mapinduzi.
Huku akikatizwa mara kwa mara na makofi, vigelegele na nyimbo, Dewji alisema kwamba, baada ya kupata mafanikio makubwa katika miradi kadhaa ya maendeleo, sasa analenga kulifanya tatizo sugu la maji kuwa la kihistoria Singida, huku akipania pia kuelekeza nguvu katika kuboresha sekta ya elimu.
Akizungumzia maji, Dewji alisema ameshachimba visima katika maeneo mbalimbali ya Jimbo vilivyomgharimu sh milioni 76, lakini akaongeza kusema: “Na bado nitachimba visima vingine virefu zaidi ya 11 ndani ya wilaya ya Singida. Mradi huu utanigharimu zaidi ya sh milioni 500. Hadi kukamilika itachukua miezi sita.”
Alifafanua kwamba, alijiingiza kwenye miradi hiyo kutoka na Singida kukumbwa na uhaba mkubwa wa maji uliotajwa kusababishwa na kukauka kwa vyanzo vya maji.
Katika elimu, mbali ya kusomesha watoto zaidi ya 550, wengi wakiwa yatima na wale ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha, hasa katika shule za Sekondari, alisema ametumia zaidi ya sh milioni 450 katika kushirikiana na wananchi kujenga shule za Kata, ikiwa pamoja na kuweka samani na vitu vingine kulingana na mahitaji ya shule na shule.
Hata hivyo aliongeza kwamba, kujenga shule za Kata pekee si suluhisho, bali aliwaasa Wanasingida kufikiria kujenga shule zaidi za kidato cha tano na sita.
“Wakati nachukua Jimbo mwaka 2005, wilaya ya Singida ilikuwa na shule mbili tu za sekondari, lakini sasa nafurahi kusema kuna shule 15, haya yote yamekuja ndani ya miaka miwili, lakini tujiulize, hawa tutawapeleka wapi baada ya kuhitimu kidato cha nne?
“Lazima tuanze kufikiria shule za kidato cha tano na sita, kama ilivyokuwa katika shule za Kata, sitaacha kuweka nguvu pale ambapo wananchi wataonekana kuwa na mwamko na dhamira ya kufanya kitu cha maendeleo,” alisema na kuzungumzia mbinu za kuondokana na shule zisizo na maabara, nyumba za walimu, majengo ya utawala na kadhalika.
Katika sekta ya afya, Dewji ameamua kupambana na magonjwa ya macho kwa kujenga wodi maalumu ndani ya hospitali ya mkoa itakayowezesha kutoa tiba za macho ikiwa pamoja na kulaza wageni watakaofanyiwa operesheni.
Aidha, katika kupambana na malaria, ametumia sh milioni 24 kununua vyandarua zaidi ya 6,000 zilivyosambazwa katika vijiji 19 jimboni mwake. Aidha, amekuwa akitoa mchele na ngano kila Ijumaa kwa ajili ya waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi katika hospitali ya mkoa.
Kwa upande wa kilimo, ili kukabiliana na uhaba wa chakula, amelipatia jimbo treka kwa ajili ya kulima mashamba ya shule na vijiji. Aliongeza kwamba, amekuwa akitoa misaada ya hali na mali katika taasisi za dini, vikundi vya vijana na akinamama na kadhalika.
Kutokana na taarifa yake, wajumbe wa mkutano huo waliompongeza na kumtaja kuwa mzalendo wa kweli kama ilivyo kwa Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono wanaotumia utajiri wao katika kuhakikisha majimbo yao yanakuwa ya mfano kimaendeleo.

No comments: