HATIMAYE waumini wa Kanisa la Wasabato wenye imani kali, waliohamia porini wilayani Kyela, Mbeya kwa lengo la kumsubiria Yesu, waliyedai angefika nchini kabla ya Machi 30, mwaka huu, wameanza kurejea katika makazi yao.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi kwa kuomba majina yao yahifadhiwe, walisema waumini hao wengi wao walianza kuondoka katika eneo hilo lililopo kati ya Kijiji cha Tenende na Lukuju tangu juzi jioni.
Walisema waliwaona waumini hao wakiondoka huku baadhi yao wakiwa wamebeba magodoro na vyombo vya ndani kwa kuvipakia kwenye baiskeli zao na kuanza safari ya kurudi mjini Kyela.
Uamuzi huo unaonyesha kuwa waumini hao wametii wito wa serikali wa kuwataka warudi kwenye makazi yao badala ya kukaa porini kumsubiri Yesu.
Wananchi hao walisema kitendo cha utii kilichoonyeshwa na baadhi ya waumini hao kwa kuondoka katika maeneo hayo, ni uungwana kwa sababu mazingira katika eneo hilo hayakuwa mazuri kutokana na ukosefu wa vyoo na huduma nyingine muhimu za kijamii hivyo kuhatarisha maisha yao.
Mmoja wa wananchi hao, Geofrey Mwakibelege alizishauri taasisi zote za dini
kuendesha shughuli zao kwa kufuata Katiba na sheria za nchi ili kuepusha maafa kama yaliyotekea nchini Uganda wakati wa Kibwetere.
Alisema imani iliyokuwepo miongoni mwa waumini wa kanisa hilo kwamba Yesu angekuja nchini, iliwashangaza wengi kutoka na wengi wa waumini hao kuacha familia na nyumba zao nzuri na kwenda kuishi porini wakinyeshewa na mvua na kuumwa na mbu na hatimaye kuhatarisha maisha yao kwa kupatwa na magonjwa mbali mbali kama malaria na yale ya kuambukizwa kama kipindupindu.
Juzi mwandishi wa Mwananchi aishuhudia baadhi ya waumini hao wakiondoka, lakini walitakata kuzungumza lolote kwa madai kuwa yeye ndiye chanzo cha wao kuamriwa kuondoka na kuongeza kwamba ushetani umewajaa waandishi wa habari.
Baadhi ya waumini hao wakizungumza kwa hasira walisema hawawezi kuondoka kijijini hapo, kwa kuwa nyumba walizokuwa wamepanga mjini Kyela kwa sasa zinakaliwa na watu wengine, hivyo watatafuta mashamba huko na kufanya makazi yao ya kudumu.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Mashimba Hussein Mashimba alisema kuanza kuondoka kwa waumini hao ni matokeo ya mazungumzo ya kina yaliyofanywa kati ya serikali na viongozi wa kikundi hicho na kuahidi kwamba serikali itakuwa karibu zaidi na viongozi hao kuhakikisha kila azimio lililofikiwa linatekelezwa.
Alisema Serikali iliamua kutumia utaratibu wa kawaida wa kukaa na viongozi wa waumini hao ili kutafuta njia rahisi ya ufumbuzi wa suala hilo, bila kuingilia uhuru wa mtu kuabudu.
Wakati huohuo, Kanisa la Waadventista Wasabato, Nyanda za Juu Kusini limetoa msimamo kuwa hali uhusiano na kikundi hicho.
Akitoa tamko hilo kwa niaba ya Askofu wa Jimbo hilo Isaac Maiga, Mchungaji wa Kanisa kuu la Wasabato Kyela, Joshua Magai alisema kwamba Kanisa hilo linaamini juu ya
fundisho la kurudi kwa Yesu Kristo mara ya pili, lakini halifundishi kuweka tarehe maalum za kurudi kwake kama inavyoeleza wazi kwenye Maandiko Matakatifu ya Biblia.
Alinukuu maandiko matakatifu kutoka Injili ya Mathayo24: 36,42,44 yanayosema: �Walakini habari ya siku ile, na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni,wala mwana, ila baba peke yake, Kesheni basi, kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu, kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari kwa kuwa katika saa msiyodhani, mwana wa Adam yu aja�.
No comments:
Post a Comment