KAMPUNI 11 za udalali zimeomba zipewe kazi ya kukusanya Sh bilioni 199 zilizochotwa serikalini na ‘wajanja’ kupitia Mpango wa Uagizaji wa Bidhaa Nje (CIS), lakini zikatumika kwa matumizi mengine bila kurudishwa. Wizara ya Fedha na Uchumi inalazimika kutumia madalali kukusanya fedha hizo kutokana na watu waliochota fedha hizo kwa kisingizio cha kuagiza bidhaa nje kugoma kuzirudisha kama mkataba ulivyowataka kufanya.
Jana ilikuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha zabuni za kufanya kazi hiyo ya kukusanya mabilioni hayo ya fedha. Hadi kufikia saa nne jana, kampuni 11 ndizo zilikuwa zimewasilisha maombi ya zabuni hiyo.
Kampuni itakayopewa kazi hiyo italazimika kukusanya madeni hayo kutoka kwa watu na kampuni zipatazo 916 ambazo zilikopeshwa Yeni ya Japan Bilioni 16 (Sh bilioni 199). Watu hao wamegoma kurejesha fedha hizo, kitendo kinachotafsiriwa kuwa ni ufisadi dhidi ya fedha za umma.
Kampuni za udalali zilizoomba kufanya kazi hiyo ni Yono Auction Mart, Majengo Auction Mart, Rhino Auction Mart, Msolopa Investment Co Ltd, Bani Investment Ltd, Kitindi Co Ltd, GM Auction, Mpoki & Associates Advocates, Nakara Auction Mart, Aslyla Attorneys & TMK Enterprises na Rex Attorney. Kila kampuni ambayo imeomba kufanya kazi hiyo imeambatanisha dhamana ya Sh milioni mbili na mapendekezo ya riba inayoombwa ilipwe kutokana na kiasi cha fedha itakachokusanya.
Wizara ya Fedha na Uchumi imeitisha zabuni hiyo huku tayari ikiwa imeshatishia kuwaanika hadharani na kuwachukulia hatua za kisheria watu waliochota fedha hizo kama hawatalipa deni hilo ndani ya miezi mitatu tangu tangazo hilo lianze kutoka kwenye vyombo vya habari.Miongoni mwa wadaiwa hao wamo wafanyabiashara maarufu nchini, wanasiasa wakiwamo wabunge na baadhi ya maofisa wa serikali.Habari hii kwa msaada wa Shadrack Sagati
No comments:
Post a Comment