Saturday, March 15, 2008

Tabata wamzomea Makamba



*Ni wakazi waliovunjiwa nyumba zao

*Amnyang'anya kipaza sauti mjumbe wa shina

*Ni baada ya kupinga ushauri aliotoa kwa wakazi hao

* Wakataa kuchukua viwanja mpaka walipwe

Muhibu Said na Emmanuel Mtinangi

ZIARA ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba kwa wakazi waliovunjiwa nyumba zao katika eneo la Tabata Dampo, jijini Dar es Salaam jana iliingia dosari, baada ya kumzomea alipojaribu kuwashawishi wakubali kuchukua viwanja walivyopimiwa katika eneo la Buyuni, wilayani Ilala.

Wakazi hao wanaoishi katika mahema, walifikia hatua hiyo baada ya Makamba ambaye aliongozana katika ziara hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro na baadhi ya viongozi wa CCM mkoa na wilaya, kuwahutubia katika eneo ambalo wanaendelea kuishi katika mahema kwa takriban wiki mbili sasa.

Akiwahutubia wananchi hao, aliwashauri wakubali kwenda kuchukua viwanja walivyotengewa na serikali katika eneo hilo, baada ya kuvunjiwa nyumba zao kinyume na taratibu. �Msikubali tatizo hili kuwa la kisiasa, kwani halikufanywa na CCM, ni tatizo la mtu mmoja wa ovyo,� alisema na kuongeza: �Najua watakuja watu hapa, watawaambia, oneni hiyo CCM.

Msiwasikilize. Sisi ndio wenye majibu, chama kingine hakina majibu ya matatizo yenu�. Alisema mtu anayewazuia kwenda kuchukua viwanja hivyo katika eneo hilo hawatakii mema. Hata hivyo, ushauri huo wa Makamba, ulianza kupingwa na Mjumbe wa Shina namba 16 wa CCM katika eneo hilo, Tauzani Mbwana, baada ya kupewa fursa ya kuzungumza katika mkutano huo.

Katika maelezo yake, Mbwana alimweleza Makamba na ujumbe alioongozana nao kuwa hawawezi kwenda kuchukua viwanja hivyo, badala yake wanachotaka, nyumba zao zilizovunjwa kwanza zithaminiwe, walipwe na waachwe waendelee kuishi katika makazi yao ya zamani (Tabata Dampo).

�Tunaambiwa twende tukachukue viwanja Buyuni. Tunachosema, kabla ya kwenda kuchukua hivyo viwanja, kwanza nyumba zetu zilizovunjwa zithaminiwe, kisha tulipwe na turejeshwe hapa hapa,� alisema Mbwana huku akishangiliwa na umati wa wakazi waliofika katika mkutano huo. Hali hiyo ilimfanya Makamba kuingilia kati mazungumzo hayo kwa kumnyang'anya Mbwana kipaza sauti kilichokuwa kikitumiwa na kumkatiza kuendelea kuzungumza na kuwashawishi wakazi hao kwenda Buyuni kuchukua viwanja hivyo.

"Hivi kama mtu anataka kutandika kitanda, si lazima ashuke kwanza kitandani ndipo atandike kitanda," alisema na kuongeza: �Kama ningekuwa mimi, ningeanza kuchukua kwanza kiwanja na baadaye ndio niendelee kudai kuishi hapa hapa. Nawaomba muende mkachukue, mkikataa serikali itasema kuwa, tuliwapa viwanja lakini walikataa kuchukua".

Hata hivyo, ushauri huo wa Makamba uligonga mwamba baada ya wakazi hao kumkatiza na kuanza kuzomea na kumweleza kuwa kamwe hawawezi kwenda kuchukua viwanja Buyuni, badala yake wanachotaka watekelezewe madai yao.

Hali hiyo ilimfanya Makamba kurudi nyuma na kuwaeleza wakazi hao kuwa: �Sisi tunawapa ushauri, mna hiari kuufuata na mna hiari kutoufuata�. Mbwana naye alichukua kipaza sauti na kumjibu Makamba akisema: �Huwezi kwenda vitani bila silaha�.

Awali, Makamba aliwaeleza wakazi hao kuwa uvunjwaji wa nyumba zao ni moja ya mambo yaliyojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Jumanne wiki hii jijini Dar es Salaam, chini ya Uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete ambaye alisema kuwa alichukizwa na kitendo hicho. �Rais alilizungumza jambo hili, hakupenda na limemkwaza sana,� alisema Makamba.

Kwa hali hiyo, alisema serikali inalijua tatizo hilo na kwamba, inalishughulikia na itahakikisha wakazi hao wanapata mahali pa kuishi na kuwataka wawe na subira. Alimtaka Kandoro kuhakikisha vigogo wa serikali waliohusika katika uvunjaji wa nyumba za wakazi hao wanachukuliwa hatua badala ya kuishia kuwachukulia hatua wadogo peke yao. �Msiendelee kuwafukuza wadogo wakati wakubwa waliofanya hivyo wapo,� alisema Makamba.

Aliahidi kumkabidhi Kandoro misaada mbalimbali ya kibinadamu, ikiwamo chakula na maji kwa waathirika wa uvunjaji huo, uliofanywa na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kinyume na taratibu.

Naye Kandoro alisema serikali haiwalazimishi wakazi hao kuchukua viwanja katika eneo la Buyuni, bali itaendelea kuvipima na kwamba, wanaohitaji ndio watakaopewa. Hata hivyo, alisema serikali itaendelea kutoa huduma za kibinadamu na kwamba watahakikisha vigogo waliohusika na uvunjaji huo wanachukuliwa hatua.

�Kazi itafanyika haraka iwezekanavyo. Tutawahangaikia wakubwa, kote huko tutafika vilevile,� alisema Kandoro. Baadhi ya viongozi walioongozana na Makamba katika ziara hiyo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Ramadhani Madabida na Diwani wa Kata ya Hananasif, Abbas Tarimba.

No comments: