*Gavana asema hatua hiyo itaongeza uwazi
*Ajivua uenyekiti wa Kamati ya Hesabu
*IMF walipendekeza kuwapo uwazi
*Balozi Sweden naye aeleza mwelekeo wao
SIKU chache baada ya kukutana na ujumbe wa Shirika la Usimamizi wa Fedha Duniani (IMF), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imetangaza rasmi mpango wa kujitoa katika usimamizi wa malipo katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ambayo imekumbwa na matatizo ya ufisadi.
Mpango huo umetangazwa jijini Dar es Salaam jana na Gavana wa BoT Profesa Benno Ndulu, ambaye pia ametangaza kujivua uenyekiti na ujumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Hesabu ya benki hiyo, huku akielezea ufisadi katika EPA kama kujikwaa na kwamba asingependa utokee tena.
EPA ambayo ni akaunti iliyoanzishwa chini ya Mfumo wa Ujamaa kipindi ambacho nchi ilikabiliwa na uhaba wa bidhaa na fedha za kigeni, awali ilikuwa iko chini ya iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kisha ikahamishiwa BoT hadi sasa.
Akitangaza maamuzi hayo, Profesa Ndulu alisema lengo la BoT ni kubaki na majukumu yake ambayo yameainishwa katika Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006.
Sheria ya BoT mwaka 2006 pamoja na mambo mengine, inataja majukumu ya BoT kuwa ni kusimamia Ukuaji wa Sekta ya Fedha, Uchumi wa nchi na Usalama wa Mabenki.
"Hizo ndizo kazi zetu, sasa tunataka kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, siyo kwamba tunakwepa majukumu ndiyo hali halisi," alisisitiza Profesa Ndulu.
Sheria hiyo pia ndiyo ambayo imewezesha BoT kuwa na Manaibu Gavana watatu ambao kwa sasa ni Juma Reli (Utawala), Lila Mkila (Sekta ya Mabenki) na Dk Enos Bukuku (Uchumi).
Alisema katika kipindi hiki ambacho malipo ya EPA yamesimamishwa, BoT inatarajia kufanya tathmini kuona jinsi itakavyokuwa ikihusika katika akaunti hiyo.
Profesa Ndulu alifafanua kwamba, hata kama tathmini hiyo itaonyesha haja ya BoT kuendelea kujiingiza katika EPA, bado itajivua sehemu ya majukumu hasa uendeshaji wa akaunti hiyo.
Gavana huyo alisema kama ikiendelea na EPA benki hiyo itataka kuendelea na jukumu la kulipa fedha tu.
"Kama tathmini itaonyesha haja ya kuendelea, tutakuwa tukilipa fedha tu kwa kuangalia kama ni halali, hili suala la kama saini iko sahihi au hundi ni halisi, litapaswa kuwa jukumu la mamlaka nyingine za serikali," alisema.
Profesa Ndulu aliongeza kwamba, Kampuni ya Kimataifa ya Lazab ya Ufaransa imepewa kufanya tathmini kuangalia kama BoT iendelee kujiingiza katika uendeshaji wa EPA au la. Kampuni hiyo ndiyo ilisaidia Tanzania kupunguziwa mzigo wa madeni baada ya kubainisha deni halisi la nchi.
Alisema kampuni hiyo pia itasaidia kuonyesha nani wanapaswa kulipwa na wapi hawapaswi, katika akaunti ya EPA.
Profesa Ndulu akizungumzia utendaji ndani ya BoT na uamuzi wake wa kujivua nafasi katika Kamati hiyo ya Usimamizi wa Hesabu, alisema ni kuzidi kuimarisha utawala bora hasa katika misingi ya kuendesha benki kwa uwazi.
Alisema akiwa ni Mwenyekiti wa Bodi, asingependa kuona anaibana kamati wakati wa mijadala, hivyo ameamua kuwepo uhuru na uwazi kwa kamati hiyo kujadili mambo mbalimbali kuhusu hesabu za BoT.
"Katika eneo la utawala bora, nimeamua kujitoa katika Kamati ya Usimamizi wa Hesabu, lakini si mimi tu, hata wajumbe wa Bodi ambao ni watendaji hawaingii humo," alisisitiza na kuongeza:
"Lakini pia tumesimamisha wote waliotajwa katika EPA, tunawachunguza tunataka kujua walifanya kwa azma ipi hasa."
Hatua nyingine ya kuisafisha benki hiyo, alisema ni pamoja na kuimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani, ambacho kitaepusha matatizo kama yalitokea katika EPA.
"Tunachotaka sasa ni kuhakikisha hatujikwai tena, yale maeneo yote ya kujikwaa tunataka kuyaziba," alisisitiza Profesa Ndulu.
Tuhuma za ufisadi katika EPA hadi sasa zimebaki kuwa mada kuu katika majukwaa mbalimbali nchini huku Timu Maalumu (Task Force) ya Rais chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Johnson Mwanyika, ikiendelea na kazi.
Hata hivyo, timu hiyo imekuwa ikikabiliwa na upinzani kutoka kwa wananchi ambao wanaona kama ni yenye kufanya kiini macho katika mchakato mzima wa urejeshaji fedha za EPA ambazo ni zaidi ya Sh133 bilioni zilizochotwa na makampuni 22.
Taarifa zingine zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) baada ya kukutana Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo zinasema Shirika hilo limependekeza kuwapo kwa uwazi zaidi na mawasiliano ya kiwango cha juu katika operesheni na sera za benki hiyo.
Ujumbe huo ulioongozwa na Roger Nord, Jumatano wiki hii ulitaka Sera za kifedha (Monetary policy) katika kuhakikisha kiwango cha mfumko wa bei hakiongezeki ili kuwezesha benki kuiimarisha sekta binafsi.
Pia kwa kuwa Bajeti ya 2008/09 hivi sasa iko katika mchakato wa maandalizi ujumbe ulitaka kuwapo uwiano bora wa masuala ya rasilimali za umma na awamu ya pili ya vipaumbele vya Mkakati wa Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi (MKUKUTA) vikiwamo maendeleo ya kilimo, elimu, afya na miundombinu kwa kulinda fedha za umma.
Hatua hizo zimetakiwa kuchukuliwa kutokana na kutokuwapo uhakika wa kutosha katika misaada ya wafadhili katika bajeti hiyo ya 2008/09.
Ujumbe huo wa IMF ulikuwapo nchini tangu Februari 27 hadi Machi 12, mwaka huu kufanya tathmini ya tatu ya mpango ujulikanao kama �Policy Support Instrument� (PSI). Mpango huu ulibuniwa na IMF mwezi Oktoba 2005 kwa ajili ya nchi zinazoendelea, ambazo zimejenga uwezo wa kubuni na kusimamia sera za uchumi kikamilifu.
Ujumbe pia ulipata fursa ya kukutana na Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo, Gavana wa BoT Profesa Ndulu; na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini.
Katika hatua nyingine, Balozi wa Sweden nchini, Staffan Herrstrom, ametaka kuwepo matumizi mazuri ya fedha za walipakodi nchini.
Balozi Herrstrom ambaye alizungumza jana wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Maendeleo wa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAO), alisema Watanzania walipakodi wanapaswa kufahamishwa matumizi ya kodi zao.
Alisema kazi hiyo kwa sehemu kubwa ipo chini ya ofisi ya CAG, ambayo inapaswa pia kuhakikisha kunakuwapo utawala bora na uwajibikaji.
"Raia katika nchi hii wana haki ya kufahamu na kupatiwa taarifa hizo, wanapaswa kujua matumizi ya fedha katika maendeleo yao na watoto katika sekta za elimu, usambazaji maji n.k," alisisitiza Balozi Herrstrom.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango, Jeremia Sumari, akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri Mkullo, alisema Ofisi ya CAG ni nguzo muhimu ya kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma.
Naye CAG Ludovick Utouh, alisema kukamilika kwa mpango huo kutaipa nguvu ofisi hiyo kusimamia vema majukumu yake ya uhasibu wa fedha za umma.
Mpango huo ambao umegharimu Sh 7.7 bilioni umetekelezwa kwa pamoja kati ya Ofisi ya CAG Sweden, Shirika la Misaada ya Kimataifa la nchi hiyo (SIDA) na serikali ya Tanzania.
Katika mpango huo ambao ni awamu ya pili baada ya kumalizika ya kwanza mwezi Februari, pamoja na mambo mengine unalenga kuijengea uwezo ofisi ya CAG katika kutoa taarifa za kina na kwa wakati kuhusu ukaguzi pia kujiendesha kwa kujitegemea zaidi yenyewe.
No comments:
Post a Comment