Thursday, March 27, 2008
Mvua kubwa yasababisha vifo Jijini Dar es Salaam !!
WATU watano wamefariki dunia, wakiwemo wanne waliofariki kutokana na mvua kubwa iliyonyesha juzi jijini Dar es Salaam.
Wakati mvua hiyo ikuua, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari kuwa mvua za masika zilizoanza huenda zikaleta madhara zaidi kwa wananchi wanaoishi mabondeni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Kandihabi alisema, jana saa 10.00 jioni maeneo ya Mbagala Kiburugwa, Saidi Mkumba (75) alifariki dunia kwa kudondokewa na ukuta wa nyumba wakati mvua ikinyesha.
Kandihabi alisema, ukuta uliosababisha kifo hicho ulikuwa wa nyumba ya mtoto wake, Fadhili Lila (32).
Katika tukio la pili, Hadija Shabani (3) alifariki dunia baada ya kudondokewa na ukuta wa nyumba yao maeneo ya Manzese Uzuri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow alisema, juzi saa 1.00 jioni maeneo ya Manzese Uzuri mtoto huyo akiwa anajisaidia pembeni mwa ukuta huo ulianguka na kumuua papo hapo.
Katika tukio lingine, Rwambow alisema, mkazi wa Mikocheni, aliyefahamika kwa jina moja la Mawaya (30) alifariki dunia baada ya kutumbukia kwenye mtaro uliokuwa umejaa maji yaliyotokana na mvua hiyo.
Rwambow alisema, tukio hilo lilitokea saa 3.00 usiku makutano ya barabara ya Sam Nujoma na Ali Hassan Mwinyi na kwamba, Mawaya (30) na Michael Charles (59) wakiwa wanatembea kwa miguu kando ya barabara hiyo, ghafla waliteleza na kutumbukia mtaroni uliojaa maj.
Katika tukio jingine lililosababishwa na mvua hiyo, lilitokea Tandale Sokoni ambako mtoto Rehema Hamis (1), alifariki dunia baada ya kutumbukia kwenye mfereji wa maji,jirani na nyumba yao.
Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi TMA, Abidan Mlaki alisema, mvua kubwa zinaweza kunyesha katika kipindi kifupi katika baadhi ya maeneo.
Mlaki alitoa mfano wa mvua zilizonyesha juzi jijini Dar es Salaam na Zanzibar, kuwa ni kubwa tofauti na walivyotarajia na kwamba, awali mikoa itatabiriwa kiwango kidogo hadi chini ya wastani ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro na visiwa vya Pemba na Unguja.
Pia, Mlaki alisema izingatiwe kuwa mvua za msimu wa Machi hadi Mei ni muhimu zaidi kwa maeneo ya kaskazini mwa nchi na matukio ya vimbunga Bahari ya Hindi.
Alisema mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara mvua zinatarajiwa kunyesha kwa kiwango cha wastani na juu ya wastani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment