Tuesday, March 18, 2008

MTAZAMO WA MSOMAJI
Jamani wandugu najua kuna watu mnapenda kusoma hebu pateni mambo kutoka kwa huyu mwanazuoni na mtazamo wake:


RASIMU YA KUINUA VUGUVUGU LA KULINDA MFUMO WA VYAMA VINGI – CONVENTION FOR THE DEFENCE OF MULTIPARTY DEMOCRACY (CDMD)

Jina: Convention for the Defence of Multiparty Democracy, kwa kifupi CDMD

Kielelezo cha uelekeo: Faith and Change Campaign (Kampeni ya Imani na Mageuzi)

Malengo:

(i) Kuhimiza kuachwa kwa kampeni ya hivi sasa kuhusu nchi kugubikwa na ‘ufisadi’ na hasa kumlenga Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, kuwa kampeni hiyo wa jumla itaiumiza nchi na kuweka hatarini mfumo wa vyama vingi.

(ii) Kuhimiza kuachwa kwa malengo ya hivi sasa ya kuirudisha nchi katika siasa za Azimio la Arusha, kwenye kipengele chake cha miiko ya uongozi, hali ambayo inaambatana na kukithiri kwa kukwamishwa mageuzi ya uchumi, kuhitaji njia kuu za uchumi (hivi sasa madini) kuwekwa chini ya sekta ya umma.

(iii) Kuhimiza kurudia sera za mageuzi ya uchumi ambazo ziliwezesha matumaini ya watu kukua katika kipindi cha awamu ya pili, kabla ya mwenendo wa mageuzi kubadilishwa katika awamu ya tatu, na kuanza kukwamisha ujenzi wa misingi ya kukua kwa uchumi na kuboresha maisha ya watu.

(iv) Kuhimiza mabadiliko ya imani za msingi kuhusu utaifa, Uafrika na maendeleo kihistoria na jinsi yanavyoonyesha tofauti kati ya nchi zilizoendelea au zinazoendelea kwa kasi, ikilinganishwa na zile za Afrika, na katika Afrika yenyewe, jinsi misingi hiyo ya imani inavyoonyesha vyanzo vya kukwama kwa kasi ya maendeleo na kuboresha maisha ya watu.

(v) Kuhimiza mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kupitia kanuni za uchaguzi za chama tawala, ili kiongozi anayepata wadhifa wa Waziri Mkuu katika awamu husika, au Waziri Kiongozi, asiwe mgombea kiti cha urais wakati Rais aliyeko madarakani akimaliza muda wake, ili kuzuia hali ya mvutano kati ya ngazi za juu za utawala (na za chama tawala) kutaka Waziri Mkuu au Waziri Kiongozi arithi nafasi ya Rais husika, na huku ngazi za chini za serikali, na chama tawala, na wananchi, wakiwa wanahitaji mageuzi,, au mabadiliko katika utawala ngazi za juu.

(vi) Kuhimiza tafsiri tofauti ya fikra ya maisha bora kwa kila Mtanzania, na ile ya utawala bora, kuainisha uhusiano kati ya mageuzi ya uchumi na kufikiwa maisha bora, na utawala bora.

(vii) Kuhimiza kuachwa kwa dhana za msingi za fikra kuhusu maendeleo zilizoainishwa katika Azimio la Arusha, ili Watanzania waanze kufikiria katika ‘masafwa’ yale yale wanayotumia watu wengine duniani, na hasa nchi ambazo zimeendelea au zinazoendelea kwa kasi.

(viii) Kuhimiza kutambuliwa kwa umuhimu kwa wataalamu wa uchumi na wasomi wengine katika nchi kuelewa msingi wa kukua kwa uchumi kuwa ni mali binafsi isiyohamishika, kuwa kukua kwa uchumi hasa ni kuongezeka thamani ya ardhi, pale inapokuwa mali binafsi inayoweza kuuzwa kwa yeyote anayetaka, bila kujali anakotoka, utaifa wake, rangi yake au imani yake kidini.

(ix) Kuhimiza kukumbukwa na kuenziwa kwa msingi wa imani kuhusu uzalendo wa Tanganyika na utaifa kwa jumla baada ya uhuru, aliopewa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1954, ule unaosema ‘binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja,’ kuwa mfumo huo wa imani unaainisha majukumu na wajibu kwa upande wa nchi kuwakubalia wanaotaka kuingia na kukaa kwetu, kwa mashari ya kawaida (asiwe mhalifu, au awe na kianzio cha biashara, au awe na mwenyeji anayemhitaji kwa shughuli fulani, n.k.)

(x) Kuhimiza kueleweka kwa msingi wa kifikra katika uchumi kuwa maendeleo hayatokani na ‘kujikomboa’ lakini kuwa na mipangilio ya uchumi na jamii inayofanana na nchi zilizoendelea au zile zinazoendelea kwa kasi. Kanuni inayozijumuisha nchi zote zinazopiga hatua katika maendeleo ni kuacha chuki za jadi dhidi ya wageni, kuwaruhusu kuhamia, hivyo kujumuisha ardhi na amana nyingine za nchi hii katika soko la kimataifa, ambako thamani yake inapanda, na watu wanapata mitaji ya kutosha kubadilisha maisha yao pale wakitoa dhamana ya ardhi au majengo kwa wengine.

(xi) Kuhimiza kueleweka kwa msingi wa kifikra na kiimani kuwa ingawa imani kuwa “binadamu wote ni sawa” haipingiki kimaadili, ina uhalisi mfinyu katika hali halisi, kwa sababu binadamu wanafanana tu katika kuzaliwa, si katika masuala mengine. Hivyo uwezekano wa maisha bora au maendeleo hutokana na tamaduni, zinazozaa taasisi, mifumo ya jamii ambayo inaweza kukuza au kubeza uhuru wa mtu binafsi, ikawezesha watu kuchanganyika au kuwatenga watu na kuwafundisha kuwa wapo maadui wa jadi, kama wakoloni, wabaguzi wa rangi (ambao kwa jumla wanakuwa Wazungu, Wahindi na Waarabu).

(xii) Kuhimiza kueleweka kwa vipengele vya historia ya imani (ya dini kuu mbili) katika mafundisho kuwa tamaduni zote siyo sawa katika ngazi ya maadili, na kuwa viwango vya maadili katika tamaduni tofauti vinaamua viwango vya maendeleo katika jamii zilizojikita katika tamaduni hizo. Hivyo kukua kwa uchumi au kukithiri kwa umaskini ni budi kuangaliwa kufuatana na tamaduni zilizopo na maadili inazopalilia.

(xiii) Kuhimiza kutambuliwa kuwa ugumu wa maisha ya watu umetokana na kuvuruga mwenendo wa urekebishaji uchumi, hasa kuanzia mwaka 1996 wakati wa kuunda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hivyo kukwamisha miundombinu ya mfumo wa bei za vitu, kuanza na kuafulu kwa biashara ngazi zote, na kuinua uwiano kati ya viwango vya mishahara na uwezo wa kununua.

(xiv) Kuhimiza umuhimu wa kueleweka kuwa viwango vya gharama za maisha havitokani na ubovu wa miingiliano maalum kama mikataba ila uhusiano kati ya fedha na vitega uchumi, kuwa kuna hali ya kupungua kwa uchumi mpana kupata fedha zinazotokana na faida katika shughuli tofauti za uchumi, hivyo ukuaji wa sekta kuwa haba, nje ya ile ya madini. Hali hii inawezesha mfumo wa uchumi wa ‘kikoloni’ kuendelea, ambako shughuli za madini au mashamba zinafanywa kupata faida ya kutoa nje, kwani haiwezi kujengwa nchini kama mali binafsi.

(xv) Kuhimiza kupanuka kwa uelewa kuwa tatizo muhimu la mchango wa sekta ya madini ni uhusiano kati ya wakazi wa asili na ardhi, ambayo inakuwa mali ya serikali (mmiliki halisi akiwa ni serikali za mitaa), na wananchi kusombwa kwa matingatinga mara anapotokea mwekezaji; kuwa hali hiyo haiwezi kuondoka bila wananchi kuwa na haki ya kumiliki ardhi kama mali binafsi, na wawekezaji kununua ardhi hiyo kutoka kwa wananchi, kwa maridhiano ya bei, ambayo msingi wake ni wastani wa bei ya ardhi, na halafu iongezeke chembe ya thamani ya madini yanapopatikana.

(xvi) Kuhimiza kueleweka kwa umuhimu wa kubadilisha mfumo wa umiliki ardhi katika kukuza uchumi wa jumla, kuwa ardhi inapokuwa mali binafsi inakuwa chanzo cha kuvuta mikopo kutoka mabenki, kuvuta akiba za watu binafsi kutoka sehemu tofauti duniani kuelekezwa huku kwa msingi wa kununua ardhi na mali nyingine isiyohamishika. Kuna haja ya kuwezesha msingi huo wa kukua kwa uchumi ueleweke kote nchini, kuondoa imani potofu kuwa kukua kwa uchumi kunawezekana kwa sera za Ujamaa mradi tu kusiwe na ‘mikataba mibovu.’

(xvii) Kuhimiza dhana na ufahamu kuwa kumiliki ardhi kama mali binafsi ndiyo msingi wa uhuru wa mtu binafsi katika uchumi, na kuwa kwa kuwachukia wageni watakaoshiriki kununua na kuuza mali zisizohamishika, wananchi wanajinyima haki yao wenyewe ya kuzaliwa, na matokeo yake ni kunyanyaswa kila kukicha katika kila kipande cha ardhi walipo, iwe ni mijini au mashambani, kwani ardhi yote ina mmiliki, hasa serikali kuu, na pale isipokuwa na mahitaji maalum na ardhi hiyo, mmiliki halisi anakuwa serikali za mitaa. Kukithiri kwa vitendo vya kusomba wananchi kwa amri za mahakama zinazotekelezwa kwa matingatinga siyo kielelezo cha rushwa ila cha kujinyima haki ya kimsingi ya kiraia na kibinadamu kutokana na ushiriki kimawazo na kiimani kuwa wageni hawana haki ya kumiliki ardhi, hivyo isiwe mali binafsi, kwani ikiwa mali ya serikali, wananchi wataendelea kuishi kwenye ardhi hiyo kwa misingi ya urithi wa koo na makabila.

(xviii) Kuhimiza kueleweka kuwa hali ya maisha ya Watanzania ni duni na ni moja ya nchi ambazo zimedumaa kabisa kimaendeleo, ingawa tumezoea kupata sifa kutoka kila upande kuhusu maendeleo yetu. Vigezo vya kusomesha wasichana shule za sekondari tuko sawa na Afghanistan, asilimia tano ya watoto wote wanaohusika, na kutumia mbolea ni kilo 1.8 kwa kilometa moja ya mraba, sehemu moja ya mia moja ikilinganishwa na nchi maskini kama Bangladesh au sehemu moja ya mia mbili ukilinganisha na Misri, ambayo si nchi tajiri na haina madini muhimu wala mafuta kwa wingi.

(xix) Kuhimiza kueleweka kuwa chanzo kimojawapo muhimu cha umaskini wa kutisha wa Watanzania ni kufuata siasa za Ujamaa (na Kujitegemea) ambazo ziliweka vikwazo kwa kila aina ya kujitafutia riziki, nje ya kilimo che jembe (la mkono) na ajira serikalini au kwa mfanyabiashara wa Kiasia.. Ni tatizo kubwa la kusaikolojia kuwa hadi sasa hali hii inawavutia watu wengi, kwa sababu ya kile kinachoonekana ni ‘usawa’ kati ya wananchi, fikra ambayo inaficha uovu wa kutotaka watu wajitafutie riziki, mapato na wakue, na fikra tegemezi ya kuonekana kuwa mtiifu kwa serikali kwa kuwabeza wale wanaotafuta ustawi, uhuru wao kiuchumi.

(xx) Kuhimiza kueleweka kwa dhana kuwa kujaribu kurudisha maadili ya Azimio la Arusha kwa waajiriwa wa serikali, au kuwabana washiriki katika siasa kuwa wasiwe na viwango fulani vya mali au ushiriki kibiashara wa kiwango hiki au kile inakiuka maadili ya mfumo wa vyama vingi. Kuhitaji kutenganisha biashara na uongozi unaweza kuwa adilifu pale tu inapokuwa suala la Rais wa Jamhuri ya Muungano kuchagua Baraza la Mawaziri, na siyo kuhusiana na uwakilishi katika ngazi yoyote ile.

(xxi) Kuhimiza kutiliwa maanani kwa hali halisi kuwa muungano wa Afrika Mashariki katika soko la pamoja ni hatua inayokaribia na haielekei kuwa inaweza kukwepwa, kama ambavyo baadhi ya wasomi au wafanyabiashara wangeweza kushauri. Katika hali hiyo ni muhimu kuwa ukuaji wa soko na upanuaji wa ushiriki katika soko kwa Watanzania katika hali zote ni jambo jema zaidi kuliko ndoto za miiko ya uongozi zinazoanza kujitokeza katika chama tawalla.

(xxii) Kuhimiza kuelewa dhana ya kihistoria kuwa kufuatwa kwa siasa ua Ujamaa na Kujitegemea kulitokana na kuhofia utawala wa ubaguzi wa rangi ambao ulikuwa adui mkubwa wa serikali zote katika ukanda wa kusini mwa Afrika na viunga vyake, kuwa wasiweze kutumia makampuni yenye nafasi kubwa kiuchumi, au wakishirikiana na maswahiba wao wa Uingereza na Marekani, kuiondoa serikali iliyokuwa inaunga mkono harakati za ukombozi kusini mwa Afrika. Kuwa nje ya harakati hizo ni budi kuangalia masuala ya uchumi kwa mpangilio wa tija, kuinua mzunguko wa fedha na kupanua soko la ndani na la nje, kuinua uwezo wa kununua wa kila mwananchi, na si maadili finyu na potofu ya kuuchukia ubepari kuwa jadi na dini halisi ya kila Mtanzania.

(xxiii) Kuhimiza kuangalia upya historia ya Tanzania ili mkazo wa kukua kwa nchi hii na wachangiaji wake uwekwe pale panapostahili, na kuondolewa pale pasipostahili.. Kwa maana hiyo waliokuza nchi ya Tanzania kama eneo halisi kijiografia siyo mababu zetu ila ni wageni na wakoloni, na katika mababu zetu wako wachache walioshirikiana nao na wengi walipigana kufa na kupona ili nchi isianze, zibaki himaya maridhawa za koo katika kila kabila.

(xxiv) Kuhimiza kueleweka kwa dhana kuwa kukwama kwa maendeleo ya Tanzania hakuwezi kutenganishwa na ufahamu potofu wa historia, na historia ya sifa potofu za Tanzania kama nchi iliyojaribu kujenga ‘Ujamaa wa ndoto’ kwa misingi ya ‘demokrasia ya chama kimoja.’ Hivyo kunatakiwa uangaliaji upya wa historia, ili misingi ya kukwama kimawazo hasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupatiwe ufumbuzi, na hivyo Tanzania ifikie hisia ‘chanya’ za kuwezesha maendeleo, na si kujiandaa kutumbukia katika shimo la giza la ‘miiko ya uongozi.’

(xxv) Kuhimiza kutambuliwa kwa hali kuwa pamoja na kuukubali msemo kwamba maendeleo yanahitaji nia thabiti kutoka kwa viongozi, hakuna linaloweza kufanikiwa kama fikra na hisia za nchi zinapingana kwa kauli moja na mifumo yote ambayo nchi zilizoendelea na zinazoendelea kwa haraka zinafahamu kuwa ni misingi ya lazima ya kukua kwa uchumi, na wao wenyewe popote wanafuata misingi hiyo. Hivyo ni budi Watanzania wahimizwe kuondokana na mazingira ya fikra ambako sisi tunatazamia tukienda kwa wengine tunakuwa na uhuru wa kufanya kazi, kusoma na kununua mali isiyohamishika, lakini tuwakatalie wengine uhuru huo, na pia kuwakatalia uhuru wa uraia wa Tanzania baadhi ya wenzetu ambao walihamia nje, au kuendelea kuishi huko baada ya masomo. Ieleweke kuwa hii ni njia mojawapo ya kukwamisha kukua kwa mitaji, miingiliano ya biashara, kukua kwa utalii na masoko, n.k.

(xxvi) Kuhimiza umuhimu wa ‘kurudi kinyumenyiume’ katika sera, kuanzia sera za awamu ya nne hadi zile za kabla ya uhuru, kurudia msingi wa fikra uliotangazwa mwaka 1954, halafu ukavurugwa baada ya hapo. Hii ina maana ya kuacha sera za kuzuia watu kupata riziki popote pale, kurudia mipango thabiti ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma yaliyobaki tena kwa mtindo wa awamu ya pili wa ubinafsishaji endelevu, kwa asilimia 70 au chini kabisa asilimia 60, na hisa nyingine kuwekwa katika soko la mitaji, kupanua ushiriki uchumi katika ngazi tofauti za jamii. Ufanikishaji wa ushiriki uchumi kunahitaji kukubali pendekezo la Sir Edward Twining la mwaka 1958 kuwa maadam Tanganyika inapata uhuru, kuweka sheria ya ardhi kuwa mali binafsi siyo tena tishio la wenyeji kunyang’anywa ardhi na wakoloni au wahamiaji. Inabidi Watanzania watofautishe uchukuaji wa ardhi na wakoloni, kwa nguvu za kijeshi au kuitawala kama serikali za mitaa na mikoa zinavyowafannyia wananchi hivi sasa, na ununuzi wa ardhi kutoka kwa wenyeji kwa bei ya soko, ambayo ni njia muhimu ya kuwezesha wananchi wengi kuacha jembe (la mkono) na kuingia katika uchumi wa kisasa, wa mikopo ya kibiashara iliyotapakaa ambao msingi wake ni urahisi wa kubadilisha umiliki wa mali isiyohamishika. Fikra kuwa ni ‘kuhamasisha’ mabenki yatoe mikopo kwa ‘wazawa,’ ni moja ya hisia mbadala ambazo ni potofu, zinazokwamisha maendeleo.

(xxvii) Kuhimiza kueleweka kimsingi kwa dhana kuwa tofauti kati ya jamii inayokaribisha wageni na kuwapa haki sawa (kulingana na maelekezo ya Torati ya Musa, kuwa ‘mtu akikaa kwako, akazaa kwako, urithi wake utakuwa sawa na ule wa watu wako’) na zile ambazo hazikubali fikra hiyo ni tatizo la kiimani ambalo jibu lake halitegemei uhuru wa kuamua wa nchi moja au nyingine, kuwa ni ukinzani wa kihistoria ambao unayasibu maendeleo hadi milango ifunguliwe, hisia zibadilike, na hivyo ujirani na udugu wa binadamu vikubalike. Nje ya hapo mikwamo inadumu, kutokana na ardhi kukosa thamani halisi na kuzuia kuinuka kwa mzunguko wa fedha.

(xxviii) Kuhimiza kudumishwa kwa nafasi ya Tanzania kama nchi yenye uwezo wa kifikra katika historia ya Afrika, kupitia kumbukumbu ya mchango wa Mwalimu Nyerere katika siasa na jamii Afrika baada ya uhuru, na hata kutoka kwa wageni Waafrika kama akina Walter Rodney, na hata nafasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kuchambua fikra kuhusu historia. Ingawa historia mara nyingi hairuhusu nchi moja au taasisi kuwa na nafasi muhimu mara mbili katika vipindi tofauti vya historia, kumbukumbu hii inaweza kuwa changamoto ya kuongoza fikra mpya katika Afrika ili kuinua kasi ya maendeleo kwa kukubali maadili ya ukaribu, udugu na ujirani wa binadamu, badala ya kung’ang’ania fikra muflisi ya ‘kujikomboa kutoka katika makucha ya ubeberu’ ambayo inalea mikwamo ya maendeleo, na kukithiri umaskini.

(xxix) Kuhimiza kutambuliwa kuwa Tanzania inayo nafasi ya kipekee katika kufikia dhana pana ya ujirani na udugu wa binadamu kutokana na mlingano maalum wa muundo wa taifa hili na watu wake, wenye vianzio muhimu vya kihistoria vya kuanza kusambaa kwa jamii ya binadamu huko Olduvai Gorge, kurithi vielelezo vya maeneo matakatifu ya asili ikiwemo Shekemu katika Israeli, na vile vya utukufu wa Misri katika historia, ikiwemo uwepo wa Joka Kuu au kielelezo cha Oliblish (kielelezo kimojawapo cha kuumba) kupitia maeneo ya maji yanayohama, yenye nguivu za kiroho za jadi, katika sehemu tofauti nchini. Pia upo urithi halisi wa ufunuo wa Uislamu ambao umewahi kuishangaza dunia, na hivi sasa, wimbi la ufunuo na matendo ya nguvu za imani katika Ukristo, kuonyesha kuwa nguvu zote za kiimani za historia ya dunia zinaitambua nchi hii au eneo hili kama lenye urithi maalum, na hivyo linafaa kuwa eneo ‘chanya’ katika kufafanua umuhimu wa udugu na ujirani wa binadamu, na kuunganishwa na historia za imani za watu wengine – zikiwamo jamii za Hamu zilizopo India, na ambazo udugu wake na Afrika ya kale yaani Misri bado kufahamika miongoni mwetu.


(xxx) Kuhimiza kuwakubali watu kutoka nje na michango yao muhimu katika kukua kwa taifa hili, na kukubali vile vile michango ya wazi ya watu wetu katika kukwamisha maendeleo, na kuwa baadhi ya vielelezo muhimu vya kimaadili na kijamii ambavyo vinahitajiwa kuenezwa na kuigwa nchini havimo katika jamii za Kiafrika na zaidi vimejengwa na jamii za wahamiaji kutoka nje. Hii ni pamoja na mshikamano wa kifamilia katika barizi au ‘kahawa’ saa za jioni, mshikamano wa kiimani na kuinuana kibiashara, na si utapeli na udanganyifu ndani ya familia, na kutakiana maovu ndani ya familia, koo na makabila. Ila tu wahamiaji hawa bado hawajatambuliwa kuwa wananchi mahsusi na utamaduni wao kuwa sehemu mahsusi ya ufahamu na elimu,. Hivi sasa nafasi yao inaishia katika ‘vipasho’ vya kibaguzi na kisiasa, katika mielekeo ya ‘tuhuma’ za wao kukwamisha ‘maendeleo,’ kutokana na mitandao ya ‘ufisadi,’ yaani kukwaza ufanisi wa sera za Ujamaa, ambako mfumo wa vitu vyote kuwa chini ya mtawala - naye avigawe kwa haki - umerithiwa kutoka Yusufu wa enzi za Misri ya Farao.


(xxxi) Kuhimizwa kueleweka kuwa wimbi la kupambana na kinachoitwa ‘ufisadi’ kunahatarisha misingi yote ya uthabiti wa jamii na pia mfumo wa vyama vingi; unazuia miingiliano ya jamii kwa kutazama nani anashirikiana na ‘adui’ wafanyabiashara, na kuanzisha ngoma ya ‘kutafuta wachawi’ kati ya ‘viongozi’ (yaani watumishi wa serikali na wawakilishi katika ngazi tofauti) ambao wanaingia katika ‘dhambi ya asili’ ya jamii za wahamiaji, yaani kutafuta fedha ‘nyingi’ kwa njia ya kufanya biashara. Lengo liwe ni kuanza upya kuzileta pamoja jamii hizi kwa kuikomboa jamii ya Waafrika kutoka imani yao ya msingi (kwa mapokeo ya Misri) ambayo ni ardhi kuwa mali ya ukoo, kabila au taifa (kulingana na vipindi vya historia au mfumo wa utawala) na pia ni ‘dhambi ya asili’ (kwa mfumo wa Torati ya Musa) ya kuwakataa wageni, na kukataa fikra ya Mungu Mmoja wa dunia yote, kwani imani kwa nguvu hii ya kihistoria ndiyo msingi wa binadamu kuchanganyika. Ndiyo maana upagani wa Kijamaa unalalamika chini kwa chini kuwa Waafrika ‘wamekubali kuabudu miungu ya kigeni’ ya wakoloni, na kabla ya hapo, kuenea kwa Uislamu.

Imetayarishwa na : Miki Tasseni
(M.A. - Dar, M.Phil. – Bordeaux I
Zamani mhadhiri msaidizi
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)

No comments: