Tuesday, March 18, 2008

Wananizulia kufifisha vita dhidi ya ufisadi - Mbowe


2008-03-18 10:18:16
Na Mashaka Mgeta

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mbowe Hotels Limited, Bw. Freeman Mbowe, amesema tuhuma zinazomkabili kuhusu kinachoitwa `hujuma` dhidi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), zina lengo la kufifisha vita dhidi ya ufisadi nchini.

Bw. Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), aliyasema hayo akiwa na Mkurugenzi Mwenza wa kampuni hiyo, Dk. Lilian Mbowe, ambaye ni mke wake, walipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Wiki iliyopita, baadhi ya vyombo vya habari, viliripoti kuhusu kampuni hiyo kukopa Sh. bilioni 1.2 za NSSF, lakini Bw. Mbowe, alisema deni halisi lilikuwa Sh milioni 15 zilizokopwa mwaka 1990.

Alisema fedha hizo zilikopwa wakati huo NSSF ikijulikana kama Mfuko wa Taifa wa Pensheni (NPF), kwa makubaliano ya kulipa riba ya asilimia 31, ili itumike katika mradi wa kupanua na uboreshaji wa hoteli yake jijini hapa.

Bw. Mbowe, alisema mwaka mmoja baada ya mkopo huo kusainiwa, hali ya kutoelewana ilijitokeza kati ya pande mbili hizo, baada ya kampuni yake kuomba ongezeko la mkopo ili kukamilisha mradi wake.

Alisema ombi hilo lilikubaliwa, lakini NSSF ilitumia kigezo cha sera zake kutoruhusu ongezeko la mkopo na kuishauri (kampuni ya Mbowe), kukopa katika taasisi nyingine ya fedha.

Bw. Mbowe, alisema ilibidi kampuni yake kukopa fedha katika Benki ya CRDB, ikiwa ni kiasi kikubwa kuliko kilichokopwa NSSF.

``Ni dhahiri kuwa mradi huu uliathiriwa kwa kiasi kikubwa, na ninaamini umakini na utaalamu wa kibenki haukutumika katika maamuzi haya? Inanilazimu kuhoji uwezo wa kitaaluma wa Mfuko kujishughulisha na biashara za ukopeshaji,`` alisema.

Bw. Mbowe, alikiri kuwapo kesi namba 277 iliyofunguliwa Septemba, 1996 na Bodi ya NSSF dhidi ya kampuni yake, ikidai malipo ya Sh. milioni 80.1, ikiwa ni jumla ya salio la deni mama la Sh. milioni 12 na riba ya Sh. milioni 68.1.

Alisema ombi hilo lilikubaliwa na Mahakama Kuu bila upande wa walalamikiwa ama wakili wao, kuwapo mahakamani hapo.

Bw. Mbowe, alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, kampuni yake ilishalipa Sh. milioni 75.5 na kwa mujibu wa mchanganuo wa kitaalamu, deni la sasa linapaswa kuwa Sh. 43,169,727.

Hata hivyo, alisema kampuni yake iliwasilisha ombi namba 151 na 152 la mwaka juzi, kutaka amri ya kukamatwa kwa Wakurugenzi wake (akiwamo Mbowe) isitekelezwe, na Mahakama ya Rufaa ilikubali.

Bw. Mbowe, alisema kesi ya kusikiliza dai la kampuni yake, kuhusu shauri la msingi kuwa na hukumu mbili, itasikilizwa Aprili 29, mwaka huu, Mahakama Kuu.

Hivyo, Bw. Mbowe, alisema taarifa zinazomhusisha na ufisadi katika NSSF, zina lengo la kuipotosha jamii, na kuondoa fikra za umma kutoka kwa watu waliohujumu uchumi na mali za umma, kwenda kwa `Mbowe na NSSF`.
Kwenye mkutano huo, Bw. Mbowe alifuatana pia na wabunge Bw. Chacha Wangwe (Tarime), Bw. Kabwe Zito (Kigoma Kaskazini), Bw. Said Arfi (Mpanda Kaskazini) na Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA, Bw. John Mnyika.

No comments: