Saturday, March 15, 2008

JWTZ kuongoza ukombozi Comoro

Umoja wa Afrika (AU) umeiteua Tanzania kuwa kamanda wa jeshi la AU litakalohusika na operesheni maalumu kukikomboa kisiwa cha Anjouan ambacho kwa sasa kinakaliwa kimabavu na kiongozi aliyejitangazia madaraka mwenyewe,
Kanali Mohamed Bacar.

Akizungumza katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alisema tayari sehemu ya askari wa Tanzania watakaojiunga na kikosi hicho waliondoka nchini Jumanne wiki hii kwa ajili ya operesheni ambayo inaweza kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

Alisema kwamba wizara yake ilishindwa kutoa taarifa rasmi kwa umma kuhusiana na kushiriki kwa Tanzania katika jukumu hilo kwa kuwa kiutaratibu ilihitaji kwanza Rais Jakaya Kikwete aliarifu Baraza la Mawaziri na uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kuvitaarifu vyombo vya habari.

Waziri Membe alisema kwamba jeshi hilo limepangwa kuwa na jumla ya askari 1,800, ambapo Tanzania inatarajia kupeleka askari 750, Senegal na Sudan (750) na Comoro yenyewe 300.

Alisema tayari Tanzania ina askari 200 waliopo Comoro kwa ajili ya kulinda amani.

Alisema kwamba jeshi hilo limepewa majukumu makuu matatu ambayo ni kumtia mbaroni Kanali Bacar ili ashtakiwe, kuhakikisha kuwa wanamgambo wanaomuunga mkono Bacar wanaporwa silaha na kulinda amani kisiwani Anjouan hadi kutakapofanyika uchaguzi halali utakaoitishwa na AU.

``Majeshi yetu hayatarudi nyuma hata kidogo kwa kuwa tumedhamiria na operesheni hii imeandaliwa kisayansi ili pasitokee madhara kwa wananchi,`` alisema.

Alieleza kwamba askari hao wamepangwa kuwepo Anjouan hadi Mwezi Mei mwaka huu ambapo hali inatarajiwa kurejea katika hali ya utulivu.

``Siku 9 zilizopita Bacar aliombwa ili ajisalimishe mwenyewe lakini aligoma tena kwa kiburi kikubwa, na ndiyo maana sasa tumeamua kutumia nguvu za kijeshi,`` alieleza Waziri Membe.

Alisema kabla ya kufikia maamuzi ya kutumia nguvu za kijeshi, AU ilitumia vikao 12 kama njia ya kidiplomasia na baadaye kukiwekea vikwazo kisiwa hicho lakini njia zote hazikufanikiwa.

Alieleza kwamba serikali inaandaa utaratibu ambao utawawezesha waandishi wa habari kutoka Tanzania kuungana na jeshi hilo la AU huko Anjoun ili kuwapasha wananchi matukio yote.

Katika mkutano huo huo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema serikali imehakikisha usalama na maslahi ya askari wote ambao wamepelekwa kwa operesheni ya Comoro.

Alikuwa akijibu swali la Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi, Saed Kubenea aliyetaka kujua jinsi serikali itakavyowalinda askari watakaojeruhiwa au kufa huko Comoro.

``Tunawahakikishia wananchi kwamba serikali itaendelea kuziangalia familia za askari wote tuliowapeleka Comoro huku tukiwahakikishia usalama wao,`` alisema Waziri Mwinyi.

Kanali Bacar ambaye aliingia madarakani katika maasi mwaka 2001 alijitangazia ushindi wa kuwa Rais wa Anjouan mwezi Juni mwaka jana katika uchaguzi ambao haukuwa halali.

Tangu ajitangazie madaraka hayo, Kanali Bacar amefunga Uwanja wa Ndege, bandari pekee ya Comoro, Anjouan na kumzuia Rais wa Shirikisho la Comoro, Mohamed Abdallah Sambi asiingie kisiwani humo. Sambi ni mzaliwa wa Anjouan na familia yake iko huko.

Shirikisho la Comoro linaundwa na visiwa vya Muheri, Anjouan na Ngazija na mbali na rais wa shirikisho, kila kisiwa kina rais wake.

Kuna kisiwa kingine cha Mayotte ambacho hakijajiunga na shirikisho na hivyo kinatawaliwa na Ufaransa.

1 comment:

Anonymous said...

Your blog keeps getting better and better! Your older articles are not as good as newer ones you have a lot more creativity and originality now keep it up!