SERIKALI imeagiza Mhandisi na Mwanasheria wa Manispaa ya Ilala, wafukuzwe kazi kwa ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kusimamia ubomoaji wa nyumba za baadhi ya wakazi wa Tabata Dampo.
Mkuu wa Mkoa huo Abbas Kandoro asema adhabu hiyo pia itamhusishe, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, John Lubuva endapo atabainika kuhusika moja kwa moja ama kwa kuamuru kufanyika au kubariki ubomoaji wa nyumba hizo.
" Nimeagiza watendaji wote wa Manispaa ya Ilala waliohusika katika zoezi hilo wafukuzwe kazi hasa Mhandisi," alisema Kandoro.
Akielezea sababu za hatua hiyo kali kwa watendaji hao, Kandoro alisema imetokana na ama uzembe au kutowajibika kwao katika maamuzi yao, hivyo kusababisha uvunjaji wa haki za wakazi wa eneo hilo ambao nyumba zao zilivunjwa Februari 29, mwaka huu.
Alisema kitendo cha uongozi wa manispaa hiyo, kuwabomolea nyumba wakazi hao, siyo cha kiungwana na kimekiuka misingi ya haki za binadamu, utawala bora, taratibu na sheria.
"Sisi kama serikali kuu hatukuwa na taarifa ya kuvunjwa nyumba hizo, tumesikia kwenye vyombo vya habari tu na baada ya kufuatilia tumegundua kulikuwa na ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu ambazo ama zilifanywa kwa makusudi au kutoelewa," alisema
Alisema uchunguzi wa kina uliofanywa na ofisi yake umebaini kuwa eneo la Tabata Dampo lilikuwa na mgogoro wa muda mrefu na mtu anayejulikana kwa jina la Allied Cargo Freight, ambaye amedai kumilikishwa kihalali mwaka 2002.
" Freight Eneo hilo limeanza kuvamiwa na watu na hivyo akaamua kufungua kesi mahakamani ambako alipata haki kwamba arudishwe eneo lake na waliovamiwa wakati ule walikuwa watu 17, " alisema.
Lakini walalamikiwa wakakata rufaa Mahakama Kuu ambako mwaka 2003, chini ya Jaji Masati mahakama hiyo haikutoa haki kwa upande wowote bali iliamuru kesi hiyo irudishwe katika baraza la usuluhishi
" Tangu wakati huo hakukuwa na mtu aliyeenda kwenye baraza hilo na ilipofika Januari 28, mwaka huu mmiliki huyo alimwandikia Mkurugenzi wa Ilala kulalamika kuwa ametoa hati za makazi kwa wakazi hao, "alisema Kandoro.
Alisema ilipofika Februari 5, mwaka huu Freight alifungua kesi katika Baraza la Ardhi Ilala, kuishtaki manispaa hiyo kwa kutoa vibali hivyo vya makazi, kesi ambayo hukumu yake ilitolewa Februari 18 kwa kutaka wakazi hao waondolewe eneo hilo kwa gharama za Manispaa yenyewe.
Katika kutekeleza hukumu hiyo, Februari 27 mwaka huu Manispaa hiyo, ilipeleka notisi kwa Afisa Mtendaji wa Tabata kumtaka awatangazie wananchi hao kuondoka au kusubiri kubomolewa nyumba zao.
'Siku mbili baada ya notisi hiyo, yaani Februari 29 Manispaa ilienda kuvunja" alieleza Kandoro na kufafanua kuwa, kitendo hicho kimekiuka taratibu za kisheria zinazotaka utekelezaji wa notisi kufanywa siku 30 baada ya kutolewa.
No comments:
Post a Comment