Thursday, October 9, 2008

Profesa J Kuwania Tuzo MTV, Zain

Profesa Jay achaguliwa kuwania tuzo MTV, Zain

Na Mwandishi Wetu

MWANAMUZIKI nyota wa Hip-Hop wa Tanzania, Joseph Haule
'Profesa Jay' amechaguliwa kuwa miongoni mwa wasanii
wanaowania tuzo za MTV Africa Music Awards
zinazodhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Zain.

Meneja Uhusiano wa Zain Tanzania, Beatrice Singano
alisema Dar es Salaam jana kuwa Profesa Jay
alitangazwa jana na MTV Networks Africa, ikiwa ni mara
yake ya kwanza kuwania tuzo za MTV Africa Music Awards
na Zain (MAMA).

Beatrice alisema Profesa Jay alitangazwa kuwania tuzo
hizo na Makamu wa Rais na Mkurugenzi Mkuu wa MTV
Networks Africa, Alex Okosi, na Ofisa Mkuu wa Masoko
wa Zain Nigeria, Norman Moyo, katika hafla
iliyofanyika Planet One, Lagos, Nigeria.

Profesa Jay ametajwa kuwania tuzo ya msanii bora wa
Hip-Hop akichuana na wanamuziki wengine, 9ice kutoka
Nigeria, HHP wa Afrika Kusini na wawili kutoka
Marekani, Lil Wayne na The Game.

Washiriki hao wanaowania tuzo za MTV Africa Music
Awards na Zain, walichaguliwa kwa kura huru
zilizopigwa kwa wanamuziki 150 wa kimataifa na maoni
kutoka nchi 30 za Afrika zilizo katika ukanda wa
Jangwa la Sahara.

Nchi inayoongoza kwa kutoa wanamuziki wengi wanaowania
tuzo ni Afrika Kusini ambao wanawania katika kategoria
18, ikifuatiwa na Nigeria yenye kategoria 16. Wasanii
wa Kenya wanawania katika kategoria tatu ambao ni Jua
Cali (Mwanamuziki Bora wa Kiume) na Wahu (Mwanamuziki
Bora wa Kike).

Wasanii wa Ghana wanawania tuzo katika kategoria mbili
ambao ni Samini na Kwaw Kese, ilhali Tanzania,
Msumbiji, Gabon na Uganda kila moja inawakilishwa na
mwanamuziki mmoja.

Wasanii wa Marekani na Ulaya wanawakilishwa katika
kategoria tatu ambao ni pamoja na Akon, Rihanna na
Alicia Keys, The Game, Lil Wayne na Buraka Som
Sistema.

Beatrice alisema washindi wa tuzo za MTV Africa Music
Awards na Zain wanatarajiwa kukabidhiwa tuzo katika
ujumbi wa The Velodrome, Abuja, Nigeria Jumamosi ya
Novemba 22, mwaka huu na hafla hiyo itatangazwa
kupitia MTV base (DStv Channel 322, GTV), RTGA
(Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), TV3 (Ghana), NTV
(Kenya), AIT (Nigeria), STV (Nigeria), TBC (Tanzania)
na WBS (Uganda), kuanzia Novemba 29, 2008.

Beatrice alitoa mwito kwa Watanzania kumpigia kura
Profesa Jay kupitia tovuti ya mama.mtvbase.com.
Alisema pia wapenzi wa muziki wenye huduma ya WAP/GPRS
katika simu zao wanaweza pia kupiga kura kupitia
m.mama.mtvbase.com, na mwisho wa kupiga kura ni
Novemba 18, 2008.

Wanaowania tuzo za 2008 MTV Africa Music Awards na
Zain ni:

MSANII BORA WA KIKE
Wahu (Kenya)
Asa (Nigeria)
Dama Do Bling (Msumbiji)
Sasha (Nigeria)
Zonke (Afrika Kusini)

MSANII BORA WA KIKE
Jua Cali (Kenya)
2Face (Nigeria)
D’Banj (Nigeria)
DJ Cleo (Afrika Kusini)
HHP (Afrika Kusini)

MTUMBUIZAJI BORA 'LIVE'
Samini (Ghana)
D’Banj (Nigeria)
P-Square (Nigeria)
Cassette (Afrika Kusini)
Jozi (Afrika Kusini)

KUNDI BORA
P-Square (Nigeria)
Freshly Ground (Afrika Kusini)
Jozi (Afrika Kusini)
The Parlotones (Afrika Kusini)
East African Bashment Crew (Uganda)

WANAOPOKEZANA BORA
Buraka Som Sistema (Ureno)
Goldfish (Afrika Kusini)
Seether (Afrika Kusini)
The Parlotones (Afrika Kusini)
Coldplay (Uingereza)

MSANII BORA HIP-HOP
9ice (Nigeria)
HHP (Afrika Kusini)
Professor Jay (Tanzania)
Lil Wayne (Marekani)
The Game (Marekani)

MSANII BORA R&B
P-Square (Nigeria)
Akon (Senegal / Marekani)
Loyiso (Afrika Kusini)
Alicia Keys (Marekani)
Rihanna (Marekani)

MSANII BORA WA MWAKA
Asa (Nigeria)
D’Banj (Nigeria)
P-Square (Nigeria)
HHP (Afrika Kusini)
Seether (Afrika Kusini)

MSANII BORA CHIPUKIZI
Kwaw Kese (Ghana)
Wahu (Kenya)
9ice (Nigeria)
Naeto C (Nigeria)
Da L.E.S. (Afrika Kusini)

VIDEO BORA
Movaizhaleine (Gabon) – Nous
Ikechukwu (Nigeria) – Wind Am Well
P-Square (Nigeria) – Roll It
Freshlyground (Afrika Kusini) – Pot Belly
Pro Kid (Afrika Kusini) – Uthini Ngo Pro.

No comments: