Friday, October 24, 2008

PETE ZILIZOMLAZA JAMAA MOI:
Kumbe ni majini



Pete hizo 15 ambazo ziliwashinda Masonara kadhaa, hatimaye zimevuliwa na jopo la Madaktari wa hospitali ya Muhimbili kitengo cha Mifupa (MOI) huku zikimwacha mhanga huyo akiwa katika hali ya kurukwa akili sambamba na kunyolewa nywele zake za Rasta.

Imedaiwa kuwa, pete hizo ambazo zilikuwa mikononi mwa Omar miaka mitatu iliyopita (toka mwaka 2005) bila kuvuliwa zimeleta maswali mengi kutoka kwa watu mbalimbali, wengi wao wakidai kuwa, ni za majini.

Baadhi ya watu waliomshuhudia Omar akiteswa na pete hizo, waliliambia Ijumaa kwamba, mwezi mmoja uliopita, Omar alikuwa akihangaika kuzivua pete hizo nyumbani kwake, Temeke lakini bila mafanikio kwa kuwa kila zilipokuwa zikiguswa, ziliashiria kuwepo kwa umeme na kufanya shoti.

Wamesema kuwa, wanaamini kuwa, pete hizo zinahusiana na majini moja kwa moja hasa baada ya Mnajimu Mashuhuri Afrika Mashariki, Sheikh Yahya Hussein kuelekeza kuwa, kama ni za majini aende Shehe na kufukiza vitunguu saumu, ndipo zitakubali kutoka kwenye vidole vya Omar na kweli ikawa hivyo.

Baadhi ya wagonjwa ambao walikuwepo Wodi moja na Omar (Sewa Haji) walisema kuwa, siku moja kabla mgonjwa huyo hajavuliwa pete hizo, Shehe mmoja alifika na kumsomea Dua, aliamuru anyolewe nywele ambazo Omar alizifuga kama Rasta sambamba na kumfukizia kitunguu saumu.

Baada ya zoezi hilo la Shehe, Madaktari Bingwa wa Moi walimpeleka Omar kwenye chumba cha upasuaji ambapo walifanikiwa kuzivua pete zote huku wakiviacha vidole vyake katika hali ya kutisha na kutotazamika.

“Lakini chakushangaza zaidi, mara pete zote zilipovuliwa Omar alionesha hali ya kurukwa akili, akisemasema ovyo na kutojitambua katika utu wake,” alisema mmoja wa wagonjwa waliokuwa jirani na Omar.

Habari zaidi zinadai kuwa, baada tu ya pete hizo kuvuliwa, ndugu zake walimchukua haraka sana na kumrudisha nyumbani ili wakampeleke kwa waganga wa kienyeji.

“Huyu mgonjwa jamani ameteseka sana, pete zilikuwa zinatoa moto, zikianza hivyo basi jua lazima achanganyikiwe akili, aseme maneno yasiyoeleweka,” alisema jirani huyo.

Alipoulizwa kama anajua neno japo moja ambalo Omar alilisema na yeye akalisikia, alijibu:
“Ilikuwa kiarabu, kwa hiyo haikuwa rahisi kujua anaongelea nini! Kama si majini ni nini jamani?” Alihoji mgonjwa huyo aliyelazwa karibu na Omar.

Ijumaa ilifanya jitihada za kumtafuta Afisa Uhusiano wa Moi, Almasi Jumaa, lakini ikadaiwa yupo safarini huku msaidizi wake, Maria akikiri kuwepo kwa mambo ya ajabu katika pete hizo.

Alisema ni kweli pete hizo zilikuwa zikitoa cheche za moto, “lakini hiyo ni kwa sababu walikuwa wanagusisha chuma kwa chuma,” alisema Maria.

Aliongeza kuwa, suala la kuchanganyikiwa akili kwa Omar baada ya kuvuliwa pete hizo ni la kweli, “lakini hiyo imetokana na mwenyewe. Toka alipokuja alionekana hana akili timamu. Lakini alipovuliwa pete ilikuwa lazima achanganyikiwe akili kwani maumivu yalizidi,” alisema Maria.

Naye ndugu mmoja ambaye alikutana na na mwandishi wa blog yetu hii nje ya wodi aliyolazwa Omar akiwa hana habari kama aliruhusiwa, alisema kuwa, ni lazima pete za Omar zilikuwa za majini kwa sababu hata kuanza kumbana vidole ilikuwa kama mchezo mchezo hatimaye ikawa suala gumu kuzivua.

Jitiada za blog hii changa kufika kwenye makazi ya Omar ziligonga mwamba baada ya kuzunguka sehemu kubwa ya Temeke bila mafanikio.


No comments: