Thursday, October 30, 2008

Kiama Cha Wezi EPA Chawadia

IKIWA imebaki siku moja kabla ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kiama cha wezi waliochota mapesa katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA), kazi iliyokuwa ikifanywa kwa zaidi ya miezi sita na timu ya rais, kufuatilia wizi huo, imekamilika.
Timu hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, tayari imemaliza kazi hiyo na kupeleka majalada yake kunakohusika kwa hatua zaidi.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata, zinasema kuwa Rais Kikwete ambaye kwa muda mrefu yuko katika ziara za kikazi mikoani, ameamua kulishughulikia suala hilo kwa uhakika ili kurejesha imani ya serikali yake ambayo imekuwa ikipakwa matope kutokana na kashfa hiyo.
Watakaokumbwa na rungu hilo ni wale walioshindwa kurejesha mapesa waliyochota, ambayo ni zaidi ya sh bilioni 133, lakini pia hata wale waliofanikisha uchotaji wa fedha hizo, nao wataguswa.
Vyanzo vyetu vya habari vinadai kuwa Rais Kikwete amepania kuwaonyesha Watanzania kuwa hana mzaha na mafisadi.
Agosti 21 mwaka huu, wakati akilihutubia Bunge mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema wazi kuwa wote waliojihusisha na wizi wa fedha za EPA, watachukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwaburuza mahakamani.
Aidha, katika hotuba hiyo ambayo Rais Kikwete alisema fedha zitakazorejeshwa zitawanufaisha wakulima, alisema hadi Agosti tayari waliochota fedha hizo walisharejesha zaidi ya sh bilioni 53, huku wengine wakitoa ahadi ya kurejesha zaidi kufikia mwisho wa mwezi huu.
Wezi wa fedha za EPA, waligunduliwa na kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa Ernest & Young, iliyopewa kazi kukagua mahesabu ya BoT na kubaini kuwa fedha hizo ziliibwa katika kipindi cha mwaka 2005/2006.
Baada ya hapo, ndipo rais alipoamua kuunda timu iliyoongozwa na Mwanyika kuchunguza wizi huo.
Habari Kwa Hisani Ya Tanzania Daima

No comments: