Thursday, October 23, 2008

Zain yaomba Watanzania wampigie kura Profesa Jay



Mwandishi Wetu


KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zain inayotoa huduma katika nchi 22 barani Afrika na Mashariki ya Kati, imetoa mwito kwa Watanzania kumpigia kura mwanamuziki nyota wa Hip-Hop wa Tanzania, Joseph Haule 'Profesa Jay' ili ashinde katika tuzo za MTV Africa Music Awards zinazodhaminiwa na Zain.


Mwito huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Meneja Uhusiano wa Zain Tanzania, Beatrice Singano aliyewaomba Watanzania kumpigia kura Profesa Jay kupitia tovuti ya www.mtvbase.com.
Beatrice alisema pia wapenzi wa muziki wenye huduma ya WAP/GPRS katika simu selula zao wanaweza pia kupiga kura kupitia m.mama.mtvbase.com, na mwisho wa kupiga kura ni Novemba 18, 2008. Profesa Jay alitangazwa takriban wiki mbili zilizopita na MTV Networks Africa kuwa miongoni mwa wasanii watakaochuana, ikiwa ni mara yake ya kwanza kuwania tuzo za MTV Africa Music Awards na Zain (MAMA).


Profesa Jay alitangazwa kuwania tuzo hizo katika hafla iliyofanyika Planet One, Lagos, Nigeria. Profesa Jay ametajwa kuwania tuzo ya msanii bora wa Hip-Hop akichuana na wanamuziki wengine, 9ice kutoka Nigeria, HHP wa Afrika Kusini na wawili kutoka Marekani, Lil Wayne na The Game. Washiriki hao wanaowania tuzo za MTV Africa Music Awards na Zain, walichaguliwa kwa kura huru zilizopigwa kwa wanamuziki 150 wa kimataifa na maoni kutoka nchi 30 za Afrika zilizo katika ukanda wa Jangwa la Sahara.


Nchi inayoongoza kwa kutoa wanamuziki wengi wanaowania tuzo ni Afrika Kusini ambao wanawania katika kategoria 18, ikifuatiwa na Nigeria yenye kategoria 16. Wasanii wa Kenya wanawania katika kategoria tatu ambao ni Jua Cali (Mwanamuziki Bora wa Kiume) na Wahu (Mwanamuziki Bora wa Kike). Wasanii wa Ghana wanawania tuzo katika kategoria mbili ambao ni Samini na Kwaw Kese, ilhali Tanzania, Msumbiji, Gabon na Uganda kila moja inawakilishwa na mwanamuziki mmoja.


Wasanii wa Marekani na Ulaya wanawakilishwa katika kategoria tatu ambao ni pamoja na Akon, Rihanna na Alicia Keys, The Game, Lil Wayne na Buraka Som Sistema. Beatrice alisema washindi wa tuzo za MTV Africa Music Awards na Zain wanatarajiwa kukabidhiwa tuzo katika ukumbi wa The Velodrome, Abuja, Nigeria Jumamosi Novemba 22, mwaka huu na hafla hiyo itatangazwa kupitia MTV base (DStv Channel 322, GTV), RTGA (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), TV3 (Ghana), NTV (Kenya), AIT (Nigeria), STV (Nigeria), TBC (Tanzania) na WBS (Uganda), kuanzia Novemba 29, 2008.

No comments: