Saturday, October 18, 2008

JK asikitishwa msafara wake kurushiwa mawe chunya
Rais Jakaya Kikwete amesikitishwa na kitendo cha wananchi wa Kijiji cha Kanga wilayani Chunya kuurushia mawe msafara wake na kuwajeruhi baadhi ya watu waliokuwa kwenye
msafara huo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza(BBC) jana kufuatia habari kwamba msafara wa Rais Kikwete umeshambuliwa kwa mawe na wananchi wa kijiji hicho.

Rweyemamu alisema kuwa Rais Kikwete amesikitishwa na tukio hilo na kwamba lilitokea baada ya kushindwa kusimama na kuwasalimia wananchi wa kijiji hicho kwa kuwa muda haukuruhusu kufanya hivyo.
"Rais amesikitishwa kwa kuwa alishindwa kusimama na kuwasalimia wananchi, lakini pamoja na hayo mazingira ya jana asingeweza kusimama,"alisema Rwehemamu.
Alisema tukio hilo lilitokea baada ya saa 1:00 jioni na kwamba baadhi ya vijana waliurushia mawe msafara huo baada ya kuona Rais anawapita bila kusimama na kuwasalimia.
Habari na Salim Said na John Stephen

No comments: