JK katika hatua za mwisho za ziara yake Mbeya

Rais Kikwete ashtushwa na mauaji Mbeya
Na Mwandishi Maalum, Mbarali, Mbeya
Mauaji mengi katika wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya yanasababishwa na imani za kishirikina na ulevi wa kupindukia, Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameambiwa katika siku yake ya nane (jana Ijumaa) ya ziara yake ya siku 10 mkoani humo.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Hawa Ngulume amemwambia Rais Kikwete kuwa katika mwaka mmoja uliopita kiasi cha wananchi 102 wa wilaya hiyo wameuawa kwa sababu mbali mbali, idadi iliyomshtua Rais Kikwete.
Mkuu huyo wa wilaya alikuwa akiwasilisha taarifa ya Serikali ya wilaya yake kwa Rais Kikwete kwenye eneo la Uturo, mwanzoni tu mwa ziara ya siku moja katika wilaya hiyo.
"Idadi hii ya mauaji iko juu sana kwa wilaya moja katika mwaka mmoja. Kuna nini? Nielezeni nini sababu ya mauaji kuwa mengi kiasi hiki katika wilaya yenu," Rais amemtaka mkuu huyo wa wilaya kueleza.
Akisaidiwa na uongozi wa jeshi la polisi wilayani humo, Ngulume amesema kuwa sababu kubwa za kiwango cha mauaji kuwa juu sana katika wilaya hiyo ni imani za kishirikina, ulevi wa kupindukia na wizi wa mifugo.
"Kuna unywaji mwingi sana wa pombe katika wilaya yangu, Mheshimiwa Rais," amesema Ngulume na kuongeza kuwa ushirikina umekuwa unasababisha watu kuuawa na kukatwa viungo vyao vya mwili kwa imani kuwa vinaweza kutumika katika kuwaletea watu utajiri.
Na kama ambavyo imekuwa katika wilaya karibu zote za Mkoa wa Mbeya wakati wa ziara hiyo, Rais Kikwete ameelezwa idadi kubwa ya watoto wa shule na wanafunzi wa kike walioachishwa masomo kwa kupewa mimba.
Kwa mwaka mmoja uliopita, kiasi cha watoto 38 wa shule za msingi na wanafunzi 34 wa shule za sekondari katika wilaya hiyo wamepewa mimba. Kesi 72 zinazohusiana na mimba hizo zimeripotiwa polisi.
"Hivi nyie madiwani mnakaa chini na kulijadili suala hilo. Hili ni jambo linakera mno. This is very serious. Hili ni tatizo la jamii na wala siyo la polisi kama mnavyotaka kunieleza," amesema Rais.
"Msipochukua hatua za kuwaadhibu watu wanaozalisha watoto wa shule, watu hawa watazoea. Watageuza shule kama sehemu zao za kuwindia. Hali hii hii nimeikuta kila wilaya katika mkoa huu," amesema Rais Kikwete akiwa anaonyesha wazi kuchukizwa na hali hiyo ya mimba za watoto wa shule.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Kikwete alizindua mradi wa umwagiliaji katika eneo hilo hilo la Uturo, na akaelekea katika makao makuu ya wilaya katika eneo la Lujewa, ambako amefungua Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali na kuwasalimia wananchi.
Akiwa njiani kwenda Madibira ambako alipokelewa na umati wa mamia kwa mamia ya wananchi na kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara, Rais Kikwete amesimama kuangalia hali ilivyo katika Bonde la Ihefu, baada ya Serikali kuwa imeamuru kuondolewa kwa mifugo yote katika bonde hilo.
Serikali iliamuru mifugo yote kuondolewa katika bonde hilo mwanzoni tu mwa Utawala wa Rais Kikwete.
Hatua hiyo ilichukuliwa katika jitihada za kulinda mazingira kutokana na uharibifu wa mazingira kuathiri kwa kiasi kikubwa kina cha maji katika kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera, na Mto wa Ruaha. Hali sasa imeanza kubadilika na kuwa nzuri zaidi.
Kwenye mkutano wa hadhara katika Paroko kongwe la Kanisa Katoliki ya Madibira, Rais Kikwete amewasimamisha mmoja mmoja maofisa na watumishi wa Serikali wanaohusika na huduma za afya, maji, umeme kujibu kero za wananchi kuhusu huduma hizo.
Rais pia amekagua mradi mkubwa wa umwagiliaji wa Madibira ambao umegawiwa katika mashamba madogo madogo ya wananchi binafsi.
Mradi huo ni tofauti na miradi ya umwagiliaji ya Kapunga na Mbarali katika mkoa huo huo wa Mbeya ambayo inaendeshwa na wakulima wakubwa.
No comments:
Post a Comment