AU Yawabana Viongozi Wasiotii Demokrasia
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, amesema umoja huo hautawavumilia viongozi wanaoingia madarakani kwa njia zisizo za kidemokrasia. Amesema nchi za Afrika lazima ziheshimu na kulea njia ya kidemokrasia katika kupata viongozi wake. Rais Kikwete alisema hayo juzi alipofungua rasmi kikao cha 10 cha Bunge la Afrika, kwenye ukumbi wa Bunge hilo ulioko Midrand mjini hapa. “Msimamo wa zamani wa kutoingilia mambo ya ndani ya nchi mwanachama hauna nafasi tena katika bara letu. Afrika sasa haiwezi kuendelea kukaa pembeni na kuangalia maadili ya kidemokrasia yakivunjwa, au serikali inapokandamiza raia wake,” alisema na kusisitiza kuwa ni lazima AU ichukue hatua dhidi ya tawala za aina hiyo. Alisema bara la Afrika siyo tena bara la kuendekeza utawala zisizoheshimu demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria, na ni muhimu suala la kupata viongozi wake kwa njia za demokrasia ziheshimiwa na kulinda. “Serikali yoyote itakayoingia madarakani kwa njia zisizo za kidemokrasia haitakubalika na itasimamishwa uanachama wake kwenye Umoja wa Afrika. Uamuzi huu umeshaanza kutekelezwa kwa baadhi ya nchi (ambazo viongozi wake wamejitwalia madaraka), Mauritania ikiwa mfano wa karibu,” alisema.
Alisema Afrika ni lazima ilinde misingi ya kidemokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu zinazoonekana sasa katika bara hilo kwa kuheshimu uchaguzi wa kidemokrasia na matokeo yake. Utamaduni wa nchi kufanya uchaguzi muda unapofika, alisema umeimarika na kutekelezwa na nchi kadhaa za Afrika, akisema tangu kuanzishwa kwa Bunge la Afrika mwaka 2004, uchaguzi wa kidemokrasia na wa wazi umefanywa katika nchi 45; mwaka pekee nchi tano zimefanya uchaguzi. Alisema wakati Afrika inafurahia maendeleo hayo ya kidemokrasia, bado kuna matukio machache yasiyofurahisha, na amelitaka Bunge la Afrika kuunga mkono juhudi za kulinda demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
Rais Kikwete amesema analitarajia Bunge hilo kuwa chachu na nguvu ya kulinda misingi hiyo, kwa kujadili na kuwasukuma viongozi wa Afrika juu wa wajibu wao wa kuheshimu utawala bora, kulinda haki za binadamu na kuwajibika kuhakikisha utawala wa sheria katika nchi wanazoziongoza. Mapema akimkaribisha Rais Kikwete kufungua kikao hicho cha Bunge, Rais wa Bunge hilo, Balozi Getrude Mongela, alisema lina wabunge 245 kutoka nchi 47 zinazowakilishwa.
Habari Kwa Hisani Ya HabariLeo
Habari Kwa Hisani Ya HabariLeo
No comments:
Post a Comment