Monday, October 13, 2008

Gavana Ndullu Kuanika Waliofanikisha Wizi EPA.

Hatima ya vigogo watano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) waliofanikisha uporaji wa Sh. bilioni 133 kwenye Akauti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika benki hiyo, inatarajiwa kujulikana mwishoni mwa wiki hii. Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, aliliambia Nipashe jana kuwa mchakato wa kuwashughulikia vigogo hao unakamilishwa na kwamba, anatarajia kuueleza umma hatima yake mwishoni mwa wiki hii.
Profesa Ndulu, ambaye kwa sasa anahudhuria moja ya mikutano ya kimataifa inayohusu masuala ya fedha mjini Washington, nchini Marekani, alitoa kauli hiyo kwa njia ya simu jana alipotakiwa na Nipashe aeleze mchakato wa kuwashughulikia vigogo hao umefikia wapi hadi sasa. ``Hilo nitakuja kuwaambia mwishoni mwa wiki ijayo (wiki hii), kwa sasa niko Washington kwenye mkutano, ambao utafungwa tarehe 15 (mwezi huu),`` `` alisema Profesa Ndulu.
Alisema mchakato wa kuwashughulikia vigogo hao ni moja ya mambo anayoyakamilisha huko aliko na kuwataka Watanzania wavute subira kuhusu hatima ya suala hilo hadi atakaporejea kutoka Marekani wiki hii.
Uchunguzi dhidi ya vigogo hao wa BoT, unafuatia mapendekezo kadhaa yaliyotolewa na Timu ya Rais ya Kuchunguza Upotevu wa Fedha kwenye EPA, iliyotaka zichukuliwe hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa wa Benki hiyo waliofanikisha wizi za fedha hizo kutoka kwenye akaunti hiyo. Mapendekezo mengine ya timu hiyo yaliyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa taifa aliyoitoa Bungeni, mjini Dodoma, Agosti 21, mwaka huu, ni pamoja na kubadili utaratibu wa Mtendaji Mkuu wa BoT (Gavana) kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo.
Pia, Wizara ya Fedha na Uchumi ianzishe kitengo maalum cha kushughulikia masuala ya EPA, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa akaunti hiyo na Wakala wa Serikali wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuanzisha uchunguzi wa kampuni zilizohusika na Ukwapuaji wa fedha hizo na kuzifuta kwenye daftari lake.
Timu hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika, inaundwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Saidi Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk. Edward Hosea. Kabla ya kutoa kauli hiyo jana, wiki chache zilizopita, Profesa Ndullu alikaririwa na gazeti hili akisema kuwa watumishi wa BoT waliofanikisha uporaji wa fedha hizo kwenye EPA, watashughulikiwa na Timu ya Rais, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kama watabainika kuwa wana kesi ya jinai ya kujibu. Alisema BoT itachukua hatua za kinidhamu pamoja na adhabu nyingine, lakini suala la kufikishwa mahakamani ni juu ya timu hiyo ya Mwanyika kwa maelezo kwamba, ndivyo Rais Kikwete alivyoagiza. Profesa Ndullu alisema katika agizo hilo, Rais Kikwete alitaka timu hiyo pamoja na BoT ziwashughulike watu hao kila mmoja kivyake. ``Tunachokifanya sisi ni kuchukua hatua za kinidhamu kazini, ambayo ina adhabu mbalimbali. Timu wana uchuguzi wao, na sisi tunatafuta haki,`` alikaririwa Profesa Ndullu akisema.
Kama BoT itawachukulia hatua za kinidhamu vigogo hao waliofanikisha uporaji wa fedha hizo, basi utakuwa mtihani mwingine kwa Mwanyika ama kukaa kimya au kuwafikisha mahakamani. Ufisadi katika EPA, kwa mara ya kwanza ulibainika kufuatia ukaguzi wa Kampuni ya Deloite & Touche ya Afrika Kusini, ambayo iliibua katika malipo ya Shilingi bilioni 40 kwa kampuni ya Kagoda, lakini ghafla BoT ikasitisha mkataba na kampuni hiyo. Baada ya mkataba huo kusitishwa, serikali iliipa kazi hiyo Kampuni ya Kimataifa ya Ernst and Young, ambayo katika uchunguzi wake, ilibaini upotevu wa Shilingi. bilioni 133 katika EPA. Katika hotuba yake bungeni Agosti 21, mwaka huu mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema watu walioiba fedha hizo kwenye EPA hadi wakati huo, walikuwa wamerejesha zaidi ya Sh. bilioni 60 na akawapa muda hadi kufikia Oktoba 30 wawe wamerejesha kiasi kilichosalia, vinginevyo, watafikishwa mahakamani ifikapo Novemba mosi, mwaka huu. Pia, Rais Kikwete aliagiza fedha zilizorejeshwa, ambazo zinahifadhiwa kwenye akaunti maalum, zitumike kwenye mfuko wa pembejeo kwa lengo la kukopesha wakulima na kutunisha Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB).
SOURCE: Nipashe

No comments: