Monday, October 13, 2008

Jk Amshukia Mwekezaji Wa Mgodi Kiwira


Rais Jakaya Kikwete, amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mashimba Hussein Mashimba, kumbana mwekezaji wa mgodi wa makaa ya mawe Kiwira, ili ahakikishe anawalipa wafanyakazi wa mgodi huo mishahara ya miezi miwili wanayodai. Rais Kikwete alitoa agizo hilo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kyela kuomba msaada wa serikali wa kumbana mwekezaji wa mgodi huo ambao pia Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amekuwa akihusishwa kuwa mmoja wa wamiliki wake, ili aweze kuwalipa mishahara wafanyakazi ambao hivi sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha. Mwingine anayehusishwa na mgodi huo ni aliyekuwa waziri katika serikali ya Mkapa, Daniel Yona. Rais Kikwete alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa, suala hilo lipo chini ya uwezo wake na kumtaka afanye kila jitihada za kumbana mwekezaji wa mgodi huo ambaye ni kampuni ya Kiwira Tanpower aweze kuwalipa wafanyakazi mishahara iliyobaki. ``Kama umeweza kumbana mwekezaji akalipa mishahara ya miezi mitatu, sasa unashindwaje kumbana tena amalizie mishahara ya miezi miwili iliyobaki. Hakikisha unambana tena awalipe, hili lipo chini ya uwezo wako,`` Rais Kikwete alisisitiza. Inadaiwa kwamba, mbali na wafanyakazi kutolipwa mishahara yao, kumekuwepo na hujuma ambazo zimekuwa zikifanyika kwa kuuza kinyemela mali za mgodi huo. Wafanyakazi waliotoa maombi hayo ni wale waliopunguzwa kazi na na serikali mwaka 2005, ambao wanaidai serikali zaidi ya Shilingi bilioni 47. Wafanyakazi hao walidai kusikitishwa na hali hiyo, kwani hata kamati ya rais aliyoiunda kuchunguza sekta ya madini na mikataba, chini ya uenyekiti wa Jaji Mark Bomani, ilipita katika mgodi huo na kupokea kilio cha wafanyakazi hao, lakini bado hawajalipwa fedha zao. Wafanyakazi hao wanaililia serikali kwamba hawajalipwa mafao na mishahara yao ya miezi kadhaa waliyokuwa wakidai tangu mgodi huo ulipokuwa chini ya serikali na kuwafanya washindwe kuondoka kwenye nyumba za mmiliki mpya aliyekabidhiwa mgodi huo. ``Baada ya suala letu kushindikana kwa muda mrefu, sasa tunataka kutumia ujio wa rais kuwasilisha kilio chetu kwake kwani ndiye pekee tunadhani anaweza kutusaidia,``alisema mmoja wa wafanyakazi hao zaidi ya 500. Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO), Thomas Cheyo, alisema hali za wafanyakazi hao waliopunguzwa kazi tangu mwaka 2005 ni mbaya na wengi hawana chakula, hivyo ujio wa Rais Kikwete ni faraja kwao. ``Tumepata taarifa kuwa Rais Kikwete anakuja Mbeya, tunaomba atembelee hapa mgodini ili tuweze kumfikishia kilio chetu,`` alisema.
SOURCE: Nipashe

No comments: