Wahariri wamweka kitanzini
Mkuchika
Hatua ya Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi, imepingwa vikali na wahariri, ambao wamepitisha maazimio saba kuhusu hatua hiyo, likiwamo la kutoandika na kutangaza habari na picha yoyote ya matukio yanayomhusu waziri huyo kwenye vyombo wana vyovisimamia.
Wahariri hao, pia wameazimia kumwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kumuasa afikirie upya uteuzi wa Mkuchika kuongoza Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, kutokana na maamuzi yake yanayohusu taaluma ya habari nchini, ambayo yameonyesha kuwa hana uwezo wa kuongoza wizara hiyo. Vilevile, wameazimia kuishitaki serikali kwenye Jumuiya ya Kimataifa na nchi wafadhili namna inavyovunja misingi ya utawala bora kwa kuminya uhuru wa vyombo vya habari; kufanya maandamano kwenda wizarani hapo kuwasilisha tamko kuhusu Mkuchika anakoipeleka taaluma ya habari nchini.
Wahariri hao pia, wameazimia kwenda mahakamani kuomba uamuzi wa Mkuchika kulifungia MwanaHalisi ubatilishwe na wamewataka watu wote wenye malalamiko yanayohusu taaluma ya habari, wayapeleke kwenye Baraza la Habari Tanzania (MCT) au kwenye Jukwaa la Wahariri au mahakamani. Maazimio hayo yalipitishwa kwa kauli moja na wahariri hao katika kikao chao cha pamoja, kilichofanyika katika Hoteli ya New Africa, jijini Dar es Salaam jana.
Kikao hicho kiliandaliwa na Jukwaa la Wahariri na kiliongozwa na Mwenyekiti wake, Sakina Datoo. Wahariri hao, wamefikia maazimio baada ya kujiridhisha kwamba, hatua ya Mkuchika kulifungia MwanaHalisi, sababu alizozitaja na matukio mengine ya nyuma aliyoyafanya kuhusu taaluma ya habari, imeonyesha kuwa ana upungufu mkubwa katika taaluma ya sheria, mbinafsi, si muadilifu, mbabe, mwenye hasira na anaiaibisha serikali ndani na nje ya nchi. Wahariri hao walisema kwamba suala la maudhui ya habari ya MwanaHalisi kama imezingatia vigezo vya taaluma. linaweza kujadiliwa na jukwaa hilo.
Walisema kwamba kimsingi, serikali haiwezi kuwa mlalamikaji, hakimu na bwana jela katika shitaka lake yenyewe, ndiyo maana wanaamini kwamba kama kuna malalamiko yoyote yawasilishwe kwenye vyombo husika ili haki iweze kutendeka. Vyombo vya habari vilivyoridhia maazimo ya jana ni pamoja na Nipashe, The Guardian, Guardian on Sunday, Tanzania Daima, Mtanzania, The African, The Express, Majira, Kulikoni, ThisDay, Mwananchi, Citizen, Changamoto.
Vingine ni ITV na Radio One, Star Tv, BBC na Channel Ten. Wahariri wa vyombo hivyo walisema kwamba kuanzia leo, habari zozote zinahusu Mkuchika hazitatolewa kwenye vyombo wanavyoongoza. Hatua kama hizi, ziliwahi kuchukuliwa dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ramadhani Omar Mapuri na Jeshi la Magereza kutokana na tukio la kushmabuliwa mpiga picha. Jumatatu wiki hii, serikali ililifungia gazeti la Mwanahalisi kwa muda wa miezi mitatu kwa madai ya kuandika habari mbaya ya kumdalilisha Rais.Habari Kwa Hisani Ya Nipashe.
No comments:
Post a Comment