Rais Wa Walimu Apigwa
KIKOSI cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kimetumia nguvu za ziada ikiwamo kufyatua risasi kutawanya walimu waliokuwa wameanza kumsulubu Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bw. Gratian Mukoba baada ya kuwatangazia kusitishwa kwa mgomo wao uliokuwa uanze leo. Tafrani hiyo ilitokea kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam jana, ambapo walimu wa mkoa wa Dar es Salaam walikusanyika, pamoja na mambo mengine, kupata kauli ya mwisho kutoka kwa viongozi wao baada ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kuwataka wasitishe mgomo wao katika uamuzi uliotolewa juzi jioni. Katika vurugu hizo, walimu hao pia walieleza siri kuu iliyokuwa nyuma ya mgomo huo wakizitaja kashfa mbalimbali za ufisadi nchini kuwa mambo yaliyowachochea na kuvunja uvumilivu na kutaka kugoma. Nia, imani na utayari Walimu hao walianza kumiminika ukumbini hapo jana mapema asubuhi kutoka wilaya zote tatu za Dar es Salaam huku wakihamasishana kwa nyimbo, wengi wao walionekana kuwa tayari kuanza mgomo huo licha ya kuwapo kwa amri hiyo ya Mahakama. Shauku hiyo ya walimu hao kuona mgomo waliousubiri kwa siku sita zilizotimia leo unafanyika, ilipotea baada ya Bw. Mukoba kuwaeleza kuwa hakuwa tayari kutoa tamko la kuendelea na mgomo huo, kwani atakuwa anavunja sheria kwa kudharau amri ya mahakama. Aliwaeleza walimu hao kuwa kutokana na jukumu alilonalo kwa nafasi yake ni zito la kutamka kauli ambayo anaamini haitawafurahisha walimu kote nchini, lakini kwa kuwa wanafanya kazi kwa mujibu wa utawala wa sheria hawana njia nyingine. Bw. Mukoba huku akiwasihi walimu waliokuwa tayari wameanza kukosa uvumilivu, aliwaarifu kuwa juzi jioni alipokea taarifa ya uamuzi huo na ilimsikitisha. "Walimu tunaomba mfahamu kuwa hata sisi viongozi wenu tumesononeshwa na agizo la Mahakama Kuu, haikututendea haki. "Hatukuridhika na uamuzi, lakini kwa kuwa hatuna njia nyingine ya kufanya, tumelazimika kusitisha mgomo. Ni kauli nzito lakini...," alisema Bw. Mukoba kabla ya kusitishwa na kelele za walimu walioanza kuinuka katika viti vyao na kurusha chupa za maji kuelekea meza kuu kwa lengo la kuwapiga viongozi wao. Tafrani ilivyoanza Kuona kurusha chupa tu hakutoshi, Majira ilishuhudia baadhi ya walimu wakivamia meza kuu, kupindua meza na viti walivyokuwa wamekalia viongozi wakuu wa CWT na baadhi kumvaa Bw. Mukoba. Juhudi za walinzi waliokuwa ukumbini hapo kudhibiti hali ya usalama zilishindikana, hali iliyolazimu kuitwa kikosi cha Jeshi la Polisi. Hata polisi walipowasili na kujaribu kuwaondoa ukumbini hapo viongozi hao kwa mlango wa nyuma, vurugu ziliongezeka huku walimu wakirusha mawe hali angani na ndipo walipofanikiwa kuwaondoa viongozi hao akiwamo Bw. Mukoba kupitia gari la Polisi Land Rover Defender namba T 220 AMV. Rais mtaroni Hata hivyo, wakati Bw. Mukoba akijiandaa kupanda gari la Polisi alipigwa jiwe gotini lililomfanya apepesuke na kuangukia karibu na mtaro wa maji machafu kabla ya kunyanyuka haraka na kuondoshwa eneo hilo. Kuona viongozi hao wameondoshwa, hasira za walimu hao zilihamia kwenye magari ya viongozi yaliyokuwa yamebaki nje ya ukumbi kwa kuyatoa upepo yote. Pia walimu wengine waliamua kulala chini mbele ya magari ya Polisi yaliyokuwa yakifanya doria katika eneo hilo, wakisema wako tayari kukanyagwa na kufa. Majira ilishuhudia gari namba T 210 AMV Land Rover Defender, likiwa limeshindwa kuondoka baada ya makumi ya akina mama walimu kulala mbele ya gari hilo. Vilio vya uchungu Huku baadhi ya walimu hasa akina mama wakionekana kulia kwa uchungu, walimu waliobaki eneo hilo walisikika wakilalamika kuwa wataendelea kugoma kwa sababu Serikali haijawatimizia madai yao na inauhadaa umma. Walimu hao pia walisikika wakilalamikia kuwa wamesalitiwa na viongozi wao na kubaki kama yatima. Hata hivyo kisheria, uamuzi wa juzi jioni, endapo Bw. Mukoba angeikaidi kwa kuruhusu mgomo huo, angeweza kujikuta akienda jela kwa kosa la kuidharau mahakama. Uchungu, shida za maisha na ahadi za muda mrefu za viongozi wa Serikali, ni mambo ambayo walimu wengi walioangua kilio jana walisema vimewachosha. "Viongozi wetu wametusaliti leo na tunaomba wajiuzulu haraka, kwani wameshindwa kutusaidia katika kudai haki zetu. Hatuwezi kuishi maisha ya kunyanyaswa wakati watu wengine wanakula fedha za umma kifisadi," walisikika baadhi ya walimu ukumbini hapo wakilalamika. Ufisadi wawakera Baadhi yao walifichua siri kuu iliyowafanya mwaka huu kuamua kugoma baada ya miaka mingi ya kuvumilia hali ngumu, kuwa ni ufisadi uliokithiri. "Serikali ilinunua rada kwa fedha nyingi tukanyamaza, ikanunua ndege ya Rais mbovu tukanyamaza, ikasaini mikataba feki ya madini, kuilipa kampuni hewa ya Richmond na tulipoona mabilioni yameibwa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu (BoT) ndipo nasi tukaamua kudai haki zetu," alisema mmoja wa walimu hao kwa uchungu. Hasira 2010 Kutokana na walimu hao kuona kuwa Serikali inawaonea na haiwatendei haki, wengi wao kwa uchungu jana walitangaza rasmi kuwa hasira zao watazihamishia katika uchaguzi mkuu mwaka 2010 huku wakinyanyua mikono na kuonesha ishara ya vidole viwili inayotumiwa na CHADEMA.
Habari Kwa Hisani Ya Majira
No comments:
Post a Comment