Wednesday, October 15, 2008

Serikali Yalifungia Gazeti La Mwanahalisi
Pichani Ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika
*******************************
Serikali imelifungia gazeti la MwanaHalisi kwa muda wa miezi mitatu kuanzia juzi kwa madai ya kuandika habari za uchochezi. Kauli ya kulifungia gazeti hilo, ilitolewa juzi jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika.
Mkuchika alisema kwa mujibu wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 serikali imelifungia gazeti la MwanaHalisi kwa madai ya kuandika habari za uchochezi. Alisema habari iliyoandikwa Oktoba 8 mwaka huu yenye kichwa cha habari kisemacho ``Njama za kumng\'oa Rais Kikwete zafichuka- Mwanae Ridhwani atumika- Watuhumiwa wa ufisadi wajipanga`` Aidha, alidai gazeti hilo limekuwa likiandika habari za uchochezi na uchonganishi dhidi ya serikali na wananchi. Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, gazeti hilo liliitwa mara kadhaa na ofisi ya msajili wa magazeti na kuonywa, lakini halikujirekebisha. Mkuchika alisema kuwa kufungiwa kwa gazeti hilo itakuwa fundisho kwa vyombo vingine vya habari vyenye mwelekeo wa kuandika habari za uchochezi Kwa upande wao, wadau mbalimbali wa habari wamelaani uamuzi wa kulifungia gazeti hilo.
Akizungumza na Nipashe Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya, alisema serikali imekurupuka. Alisema hatua hiyo hailikomoi gazeti hilo pekee bali wananchi ambao wana haki ya kupata habari. Aliongeza kuwa Waziri Mkuchika amepitwa na wakati pamoja na sheria yake ya magazeti ya mwaka 1976 Nkya alisema serikali haipo juu ya wananchi hivyo kitendo cha kutumia ubabe katika kulifunga gazeti hilo ni kuwadharau wananchi. Mwanaharakati huyo alisema kuna chombo cha mahakama kama serikali iliona gazeti hilo limevunja sheria ingefungua kesi mahakamani.
Chombo kingine ambacho alisema kingefaa kutatua tatizo hilo ni Baraza la Habari Tanzania (MCT). Aliongeza kuwa serikali imeshindwa kutumia vyombo hivyo na badala yake imetumia sheria ya mwaka 1976 ambayo imepitwa na wakati. Alisema sheria hiyo bado ipo kutokana na uzembe wa watendaji wa serikali, lakini isingefaa kuwepo. Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (Misa- Tan), Ayoub Rioba, alisema anawasiliana na wenzake ili kutoa tamko la kulaani tukio hilo. Hata hivyo, kwa maoni yake alisema, kitendo hicho ni cha dharau na kwamba Mkuchika amepitwa na wakati pamoja na sheria yake. Akizungumza na Nipashe ofisini kwake, mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, nchini, Sakina Datoo alisema, leo watakutana ili kutoa tamko. Alisema Jukwaa la wahariri limeshtushwa na hatua hiyo ya serikali. Aliongeza kuwa hilo ni jambo zito na kwamba atakapokutana na wenzake watatoa tamko la pamoja. Alisema licha ya gazeti hilo kufungiwa pia mhariri wake, Saed Kubenea juzi alikamatwa na polisi akahojiwa kwa saa kadhaa, lakini akaachiwa kwa dhamana.
Habari kwa Hisani Ya Richard Makore/Nipashe

No comments: