libeneke la kujaza nafasi ya chacha wangwe
mgombea nafasi ya ubunge kupitia chadema mh. Job Qhenkori Chacha akinadi sera zake. picha kwa hisani ya www.globalpublisherstz.com
na Deogratius Temba
MCHAKATO wa kumpata mgombea ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umezidi kupamba moto, huku wagombea kupitia chama hicho wakizidi kumiminika.
MCHAKATO wa kumpata mgombea ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umezidi kupamba moto, huku wagombea kupitia chama hicho wakizidi kumiminika.
Jana ilikuwa siku ya mwisho kurudisha fomu kwa walioomba kugombea nafasi hiyo kupitia chama hicho, huku mgombea mwingine akijitokeza kuchukua fomu katika hatua hizo za mwisho.
Mgombea huyo ni Job Qhenkori Chacha, mzaliwa wa Kijiji cha Buhemba, wilayani Tarime.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, Chacha alisema kuwa ameamua kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo kwa sababu anajua shida zinazowakabili wananchi wa Tarime.
“Mimi nimeamua niache shughuli zangu nyingine niende kijijini nikashirikiane na wana Tarime kuijenga, tuendeleze kile ambacho marehemu Chacha alikiacha, pale alipoishia,” alisema Chacha.
Akijibu swali iwapo ataweza kuvaa viatu vya marehemu Wangwe, alisema anaamini anaweza kufanya kazi kubwa kuliko hata marehemu Wangwe.
“Viatu vyangu ni vikubwa zaidi ya vya kwake, mimi ni zaidi yake, na nitawajibika kuliko hata alivyofanya yeye. “…Mimi naweza kuwa mtu hatari kwa CCM, na nikiteuliwa na chama changu nitahakikisha kuwa CCM hawaibi kura hata moja, ni lazima CHADEMA ishinde,” alisema.
Chacha ambaye alijiunga na CHADEMA mwaka 1998 akitokea NCCR- Mageuzi, alisema yeye ni mwana mapinduzi wa siku nyingi lakini alichelewa kujiingiza kwenye siasa kwa sababu ya mfumo wa chama kimoja uliokuwa nchini, lakini baada ya kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, alijiunga na NCCR -Mageuzi.
Jana ilikuwa siku ya mwisho kurudisha fomu na usaili wa chama hicho utafanyika siku ya Jumatatu mjini Tarime. Job Qhenkori Chacha anakuwa mgombea wa tatu kuchukua fomu ya kugombea ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA, baada ya mwanahabari Nyaronyo Kicheere na mwanazuoni Easter Matiko, kujitosa kugombea nafasi hiyo.
Wakati huo huo, gazeti hili jana lilidokezwa kuwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiko katika mkakati mzito wa kuhakikisha kinafanya vizuri katika uchaguzi huo mdogo.
Habari hizo zilieleza kuwa CCM kimeunda kamati ya kutengeneza ushindi wa nguvu inayoongozwa na Katibu Mkuu wake wa taifa, Yusuf Makamba, na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ni wakongwe wa ‘fitna’ za kisiasa, akiwemo, Kingunge Ngombale - Mwiru na mwanasiasa mwenye uzoefu katika kampeni, John Samwel Malecela.
No comments:
Post a Comment