hii ndiyo hotuba alioisoma mwanaharakati john mashaka
Hitaji ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayotukabili imetulazimu wanadamu kutafuta mbinu ya kuyatatua;
Tumefanikiwa kugundua tiba dhidi ya maradhi ya kutisha na pia tumefanikiwa kuboresha maisha yetu.
Hitaji ya kuwasiliana kwa wepesi, imetulazimu wanadamu kugundua ,redio, simu, televisheni na njia nyingine nyingi ambazo zimerahisisha mawasiliano yetu na kuifanya dunia kuwa jamii moja ndogo.
Binadamu tumepiga hatua kubwa. Lakini cha ajabu ni kwamba, ingawa tuna mafanikio makubwa, tumeshindwa kuyatatua matatizo yetu madogo kuliko yote, matatizo yasiyohitaji upeo mkubwa wa kielimu au kiteknolojia
Tumeshindwa kuwa waadilifu katika matendo yetu kwa jamii. Tumeshindwa kuishi kwa amani,Tumeshindwa kupendana. Zaidi ya miaka kumi na mbili iliyopita, hitaji ya kutafuta elimu iliniondoa humu nchini ili kujifunza yale ambayo yangekuwa ya manufaa kwa jamii yetu, nchi yetu na dunia yetu kwa ujumla.
NDUGU ZANGU: Nimejifunza maadili yanayoweza kuwa ya manufaa kwa nchi yetu, ikiwa tu tutaukubali wito; wito wa kuwa, waadilifu kwao binadamu wenzetu. Nimejifunza maadili ya kuwa wavumilivu katika dhiki.
Nimejifunza kwamba wote tunaowaonea wivu nchi za magharibu, hawakuyafikia mafanikio yao kwa kuzisubiri serikali zao kuwakomboa,wamefanikiwa kwa kujitoa mhanga na kufanya kazi katika mazingira magumu bila ya kukata tamaa.
Nimefanikiwa kufanya kazi na watu wanaotambulika duniani kutokana na utajiri wao, watu ambao bidii zao za kazi zimenipa mtazamo tofauti wa maisha.Nimefanikiwa kufanya nao kazi zinazolingana kwa masaa 17 mfululizo, bila ya chakula au chakula kidogo ikiwa kipo, na hii ilinifundisha siri ya kujinyima. Hawa watu wamefanikiwa kutokana na unyekevu na uvumilivu.
Nimejifunza kwamba wale waliopewa dhamani ya kusimamia mali za umma, hawaendekezi tamaa zao.Bali Wanaweka mbele maslahi ya nchi zao na kuheshimu matakwa ya umma wakifahamu kwamba nyadhifa na vyeo walivyonavyo ni dhamana na heshima walizopewa zinazohitaji uadilifu wa hali ya juu
Baadhi ya hawa viongozi ujishusha hadhi, ujivua nyadhifa, pamoja na elimu zao na kujiweka katika hali ya kawaida, ili kuwatumikia wasiojiweza kwa kutenga muda maalum kutoka katika ratiba zao; mbali na utajiri na maisha yao ya kifahari, kuwapikia, na hata kusafisha vyoo vya wasiojiweza, huku wakiwafariji waliopoteza matumaini kutokana na ugumu wa maisha
Hawa ni watu ambao hawajioni na kujitafakari kama watumikiwa, bali wanajiona kama watumishi katika nchi zao.Haya ndiyo maadili niliyowaletea kwa manufaa ya nchi yetu. Kwa wale waliobahatika kuwa nacho, tusijione kana kwamba tu wafalme, nawasihi tujione kama watumishi Wengi wamejiuliza ni kwa nini nimeamua kujishugulisha na maswala ya kijamii,
Watanzania wenzangu basi napenda kuwajibu kwamba. Nilizaliwa humu nchini, nayafahamu matatizo ya watanzania walio wengi, ambayo siyo mahitaji ya kifahari bali mahitaji muhimu ya kumudu maisha. Nimeamua kujishugulisha na hizi shuguli ili kulipa fadhila,
Ninaamini sitakuwa nimewatendea haki binadamu wenzangu iwapo nitazamisha kichwa changu katika starehe na maisha ya kifahari nikasahau niliowaacha nyumbani wakiteseka kwa njaa na umasikini.
Huu ni utashi unahohitaji karama ya kumuwezesha binadamu kufanya maamuzi yenye busara baina ya utajiri na utu. Nayafanya haya kwa sababu naamini huu ni wito alionipa mwenyezi Mungu;
Ni wito wa kulipa fadhila pale panapostahili .Nayafanya haya kwa ajili ya amani katika jamii yetu. Na hii amani haiwezi kupatikana bila kuonyesha upendo kwa wale wanajiona kutelekezwa na kutokukubalika.
Watanzania wenzangu, sina utajiri wa aina yoyote, na wala siwakislishi taasisi yoyote, bali nimeamua kugawa sehemu ya kipato changu kidogo na wenzangu wanaodidimia katika lindi la ufukara na matatizo ya kijamii.
Msininiukumu na kuniona tofauti na vijana wengine wa kitanzania kwani hapa nilipo , kama walivyo vijana wengine moyo unaniuma; Baba yangu mzazi ambaye leo angekuwa nami hapa kuniunga mkono, nimemzika siku tano zilizopita, lakini kutokana na ukweli kwamba hitaji la walio wengi halijakidhiwa, naamini popote roho yake ilipo inaiombea taifa letu. Nayafanya haya kutokana na hitaji iliopo nchini kwetu.
Nafahamu fika kwamba wapo watanzania wengi wanaolala bila chakula, Nafahamu fika kwamba wapo wengi wakina mama wajawazito wanaopoteza watoto wao wachanga kila uchao kwa sababu tu ya kukosa huduma za msingi.
Watu hawa hawaombi majumba makubwa ya kifahari, Hawaombi vyakula vya gharama za juu,Hawaombi kwenda mwezini, Hapana ! Wanapigania mahitaji ya msingi. Wanapigania malazi, Wanapigania chakula kwa ajili ya familia zao.Wanapigania elimu kwa ajili ya watoto wao.
Wanapigania tiba dhidi ya maradhi yanayoididimiza nchi Wanapigania haki zao za kibinadamu, wanatafuta ufumbuzi dhidi ya umasikini .
Nchi yetu ina rasilimali ambazo hazipatikani kwingineko duniani, , nchi yetu ina sehemu nyingi za kihistoria, ina utamaduni unaoheshimika duniani pote. Nchi yetu ina hazina ya ukarimu.
Inabidi tuutambue ukweli huu na kuutumia kama nyenzo ya kutuwezesha kuondokana na umasikini na kufikia kilele cha maendeleo. Tunatakiwa kubeba jukumu la kuangalia mustakabali wa muda mrefu wa nchi, badala ya kuangalia yaliyopo mbele yetu kwa sasa tu.
Watanzania, Tusiihache historia kutuhukumu kuna hitaji;Hitaji yetu wote kutazama hatima ya nchi yetu kwa undani. Ni lazima tuwafikirie wale wanaoumia kutokana na ubinafsi na tamaa zetu.Hebu tuwafikirie watakaorithi matendo na maamuzi yetu
Nanyi viongozi wetu: Ni lazima muwatafakari watanzania millioni 40 ambao maisha yao yapo mikononi mwenu. muwakumbukeni wanaohangaika juani usiku na mchana kuzilisha familia zao.
Wafikirieni vijana wanaozurura kwenye miji yetu bila ya matumaini, bila kuogopa kupoteza maisha yao. Wafikirieni kwa ajili ya usalama wa hii nchi. Ni lazima muwatafakari wajukuu wenu watakaorithi maauzi na matendo yenu ya leo. Ni lazima mtafakari jinsi watakavyowakumbukwa.
Kuna hitaji kubwa ya viongozi wetu kulinda maslahi ya nchi kuliko kuwapa mzigo watu ambao tayari maisha yamewachosha. Lazima uadilifu uwepo katika maamuzi yenu kwa ajili ya mamimillioni ambao njaa zao hazijalishwa, lazima muwafikirie wanaoshindwa kupokea matibabu kutokana na umasikini Kuna hitaji ya viongozi watumishi badala ya vingozi watumikiwa, kwa sababu kipimo cha kiongozi bora siyo watu wangapi aliowaongoza, bali watu wangapi aliboresha maisha yao.
Mwanafalsafa wa kimarekani, Rosaline Carter alipata kutamka kwamba, “ Kiongozi uwapeleka watu wanapotaka kwenda, ila kiongozi bora, hawapeleki watu wake wanapotaka kwenda,bali wanapostajili kuwapo. Huyu ndiye kiongozi anayehitajika katika jamii yetu; Kingozi mtumishi ,siyo mtumikiwa. Kiongozi ambaye yupo tayari kuyatoa maisha yake kwa ajili ya jamii yake.
Kiongozi mwenye machungu na nchi yake, Kiongozi mzalendo ndiye tunayemhitaji Kwenu vijana Venzangu! Ingawa miaka 40 ya uhuru imepita, na wengi wetu bado wanaishi katika janga la dhiki na ukosefu wa matumaini, nawaombeni msikate tamaa, kwani muda siyo mrefu nchi tuliyohaidiwa tutaifikia.
kiwingu cha mikwamo kilichotanda katika upeo wa macho yetu utatoweka, ikiwa tutaonyesha .Muhimu ni kufanya kazi kwa uadilifu na kwa ushirikiano, siyo kwa manufaa yetu, bali kwa manufa yaa jamii na vizazi vijavyo.
Kwa walio bahatika kupata elimu, tumieni elimu na nafasi zenu kwa manufaa ya jamii. Msizitumie elimu na nafasi zenu kuwakandamiza wanyonge. Kwani elimu bila manufaa ya jamii ni elimu isiyo na thamani,tumieni elimu zenu kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii.Wafanyabiashara na wasanii, tumieni vipaji na ujuzi mlionao vyema bila kupotosha tamaduni zetu.
Profesa Jay,Afande sele na wengine wote wahabarisheni vijana kwamba ukimwi upo na unaua. Wanasiasa, viongozi wa kidini, Waalimu, wakulima wanaohangaika toka kuchwa hadi machweo, wachuuzi wanao umia na ugumu wa kiuchumi, nina imani kwamba hali ya sasa ni ya muda tu, itabadilika. Msikate tamaa,
Tusilale kuisubiria serikali kuyatatua matatizo yetu, kwani mabadiliko ya kijamii yanaletwa na watu wa kawaida kama mimi na wewe wanaojitolea mwanga kwa ajili ya jamii yao. Kuwepo kwenu hapa siku ya leo ni ishara tosha kwamba, wengi wenu wamechoka na dhiki ni lazima tujinyime leo kwa ajili ya kesho. Ingawa tunaongea lugha tofauti, Ingawa tunatofauti za kidini na kiitikadi,
Ingawa tuna tofauti za kiuchumi, Sote ni watoto wa familia moja na taifa moja. Tuonyesheni upendo kwao ambao hawakubahatika. Binadamu tumeumbwa kupendana, hii ndio asili yetu Katika kipindi ambacho dunia inapigana vita dhidi ya ukandamizaji na umasikini, tushirikiane ili kuuziba mwanya baina ya umasikini na utajiri katika jamii yetu.
Ili kuwapa matumaini waliokata tamaa Kwa maana jamii isiyokuwa na matumaini, ni jamii bila mwelekeo. Katika kipindi ambacho dunia inapigana na ukosefu wa amani, ni lazima tushirikiane ili kupunguza umasikini. Hatuwezi kuwaacha masikini wafe njaa,
kwani amani haina nafasi popote pale duniani pasipo na chakula. Huu ndio ujumbe wangu. Ujumbe wa Hitaji wa amani, hitaji ya kutumia mikono na nyoyo zetu siyo kwa manufaa yetu bali kwao waliokata tamaa kuishi
Asanteni
Asanteni
No comments:
Post a Comment