Wednesday, October 8, 2008

Mallya wa kifo cha Wangwe akosa tena dhamana

MFANYABIASHARA Deus Mallya (27), aliyenusurika katika ajali iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, jana alikosa dhamana baada ya vithibitisho vya mdhamini wake kutiliwa shaka na upande wa mashitaka kuwa huenda ni vya kughushi. Mallya ambaye jana alitinga mahakamani hapo akiwa na Biblia mkononi, alikosa dhamana baada ya barua iliyowasilishwa na mdhamini wake, Julius Michael kuwa na mhuri ambao hauonyeshi ni wa Ofisa Mtendaji wa Kata ipi, licha ya mdhamini huyo kudai anatoka eneo la Majengo mjini hapa. Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Thomas Simba, Mwendesha Mashitaka, Mrakibu wa Polisi, William Maganga alidai jana kuwa barua ya mtu aliyejitokeza kumdhamini Mallya iliyowasilishwa Septemba 12, kwa Hakimu Moses Mzuna, ilionyesha kuwa Michael alikuwa akiomba mahakama impe dhamana Denis Maliwa badala ya Deus Mallya mtu ambaye yupo katika jalada. Maganga alidai licha ya mdhamini huyo kuiomba mahakama imdhamini Denis Maliwa, pia katika barua hiyo kulikuwa na mhuri usiosomeka kuwa ni wa Ofisa Mtendaji wa Kata ipi, jambo alilodai kuwa linautia shaka upande wa mashitaka na hivyo linahitajika kufanyiwa upelelezi kabla ya Mallya kupewa dhamana. Pia Maganga alidai kuwa katika barua nyingine ambayo pia iliwasilishwa mahakamani hapo jana, haikuwa na muhuri unaoonyesha kuwa ni kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ipi, jambo ambalo liliutia shaka upande wa mashitaka na kuomba mahakama itoe muda wa kulifanyia uchunguzi jambo hilo na kukabidhiwa barua hizo kwa ajili ya kujua iwapo aliyeandika barua hizo ni kweli au la. Kwa upande wake, hakimu Simba alikubali ombi hilo na kudai kuwa hata yeye ana shaka juu ya vielelezo vya mdhamini na kuongeza kuwa iwapo mahakama itabaini kuwa vielelezo hivyo ni vya kughushi, waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria. Aliagiza upelelezi ufanywe kuhusu vielelezo hivyo na kutoa siku tatu kwa ajili ya upelelezi huo kufanyika; hivyo kesi hiyo itaanza kusikilizwa na kupokea ushahidi Oktoba 13, mwaka huu kutokana na kuhamishiwa hakimu mwingine. Hakimu Mzuna sasa anasikiliza kesi za mauaji Mahakama Kuu. Kwa upande wake, Mallya aliyekuwa pamoja na Wangwe katika ajali ya Julai 28, mwaka huu, aliiomba mahakama ianze kusikiliza kesi yake mapema akidai kuwa jela kuna taabu sana. Jamaa mbalimbali wa Wangwe walifika mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo, wakiwamo watoto wa marehemu, Bob Chacha na Zakayo Chacha.
Habari kwa Hisani Ya:
Martha Mtangoo, DodomaDaily News

No comments: