Saturday, December 6, 2008

TRA yaipiga pini kampuni ya kuzalisha umeme aggreko
Meneja mradi wa kuzalisha umeme wa Kampuni ya Aggreko, Shaughn Tyreman akitoka nje ya lango la kuingia eneo la mradi huo baada ya kuamriwa na Kampuni ya Udalali ya Majembe ili ifunge eneo hilo, kufuatia idhini waliyopewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inayowadai kodi ya Sh bilioni 10.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezuia kwa kuweka makufuli katika lango la kampuni ya kufua umeme ya Aggreko Dar es Salaam jana, baada ya kuwapo taarifa inahamisha kinyemela mitambo yake na kuipeleka nje ya nchi, kwa lengo la kukwepa kulipa deni la Sh bilioni 10 inalodaiwa na mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka chanzo cha habari ndani ya TRA juzi na jana, zilidai kuwa Aggreko inadaiwa Sh 10,117,558,321 ikiwa ni deni la kodi ya miaka mitatu ya uzalishaji umeme nchini. TRA ilithibitisha Aggreko kudaiwa deni ingawa hawakuwa tayari kusema ni kiasi gani, kwa kuwa ni mkataba wa siri kati yake kampuni hiyo ambayo wanaitambua kama mlipakodi wao.

“Tangu wameingia hapa nchini hawa wawekezaji ambao waliitwa kutokana na dharura iliyolikumba taifa kipindi cha nyuma, hawajawahi kulipa kodi, na tumefanya nao mikutano bila mafanikio, tumewaletea taarifa za maandishi, hawajaonyesha kujibu,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Katika eneo la tukio jana, tafrani ilizuka wakati maofisa wa TRA pamoja na wa Kampuni ya Majembe Auction Mart, walipofika wakiwa katika magari ya kawaida na kuwaamuru walinzi wafungue mlango mkuu wa kuingia ilipo mitambo hiyo.

Kutokuelewana kulianza pale walipogundua kuwa ni maofisa wa TRA na wanahitaji Mkuu wa eneo ili waamuru wafanyakazi wake watoke ndani, kwani mtambo huo unafungwa hadi deni hilo litakapolipwa; ndipo walinzi walipotaka kuwatoa kwa nguvu maofisa na wanahabari, jambo lililozua zogo bila mafanikio ya kuwaondoa.

No comments: