Friday, December 12, 2008

alutazzzzzz
Kwako Bwana Kadidi na wadau wa Blogu ya Inawezekana, Nami nimeona nisipitwe na mjadala huu wa kuelekea Shirikisho la Afrika ya Mashariki.
Kiswahili VS Kiingereza:
Hawa jamaa wamekuwa wanatusema sana kuwa sisi hatujui Kiingereza, lakini ukweli ni kwamba Kiingereza kwangu mimi si kigezo cha maendeleo,nchi nyingi sana zilizoendelea zimekuwa zikitumia lugha zao za asili, kwa mfano Ujerumani,China,Korea, Japan, n.k, Lugha ni lugha tu, ilimradi inatuwezesha kuwasiliana. Sasa sielewi wao wanaposema kuwa hatujui Kiingereza kwao ina maana gain.
Nakumbuka kuna kipindi nilikutana na bibi mmoja raia wa Kenya, nikawa namuongelesha kwa Kiingereza kwa mshangao yule mama akaniomba niongee Kiswahili sana,nilishikwa na butwaa, kwa sababu nilivyokuwa nasikia kwamba Kenya kila mtu anajua Kiingereza hata kama ni mzee,wakati huo nilikuwa sijafika Kenya bado,niivyofika Kenya ndio nikaja kufahamu ukweli kuwa Kiingereza chao ni cha Kawaida kiasi kwamba hata sisi tunazungumza Kiingereza.
Tofauti za Kiuchumi:
Wao waliamua kuchagua Ubepari nasi tukachagua Ujamaa,kila aina ya uchumi ina mambo inayoambatana nayo. Kwa mfano Ubepari unataka kama mtu unakuwa nacho unakuwa nacho sana na kama hauna hauna sana(kabisa), na hiyo ndio hali halisi iliyopo Kenya, kuna watu wana ardhi kubwa sana na hadi vilembwe vyao vinarithi na kuna watu hata hawajui kama vilembwe vyao vitakuja kumiliki ardhi mfano mzuri ni mtaa wa Mabanda na Kibera pale Nairobi, Tanzania hakuna hasa Dar es Salaam mimi sijawahi kuona makazi kama yale, kama nakosea naomba mnirekebishe.
Kiujumla mimi siwalaumu sana watani wa jadi kwa sababu kila kitu kina faida zake na hasara zake wao walichagua ubepari wamepata faida na hasara za ubepari, sisi tuliochagua Ujamaa tumepata faida zake na hasara zake.
Tatizo letu Watz:
Ukizungumzia kusoma watanzania tumeenda shule karibu sawa na hao ingawa inawezekana wao wametuzidi kidogo kwa idadi ya wasomi. Tatizo tulilo nalo ni aina ya elimu tunayopata, sisi tunasoma ili tuajiliwe wakati wenzetu wanasoma halafu wanaangalia fursa zilipo wakati sisi Watanzania tumesoma lakini hatuoni fursa tulizonazo, kwa mfano ili suala la wao kutaka ardhi yetu kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki ni kwa sababu wao wameona fursa(opportunity).
Sisi imefikia hata viongozi wetu kama wabunge na mawaziri hawaoni fursa ambayo nchi inayo ili kujua jinsi ya kuzitumia kwa manufaa ya nchi, hii inadhihirishwa na mikataba ambayo viongozi wetu wamekuwa wakisaini, Richmond, IPTL, AGGREKO.
Tuchukue mfano wa Shirika la ndege la Air Tanzania na tulifananishe na Shirika la ndege le Kenya,ona sisi tulivyoshindwa kuona fursa hadi tukauza kwa Shirika la Afrika Kusini na tuona ambavyo Kenya Airways ambavyo imeuzwa sehemu ya hisa kwa Air FranceKLM na tulinganishe hali ilivyo katika mashirika hayo mawili.
Tumekaa tunalalamika kwamba wao watatunyonya lakini suala linabaki pale pale kwamba hatuoni fursa tulizonazo, angalia mahoteli yanavyopewa msamaha wa kodi(Tax holiday) kwa wawekezaji ambao wamekuwa wakibadilishana utawala, hapa tunakumbuka Sheraton,Royal Palm na sasa Moevenpick na hadi leo sijui wabunge wetu wanafanya nini kuona kwamba fursa hiyo inatumiwa visivyo.
Wenzetu wakenya wazuri sana katika kuangalia fursa zilizopo na kuzitumia, waliangalia Mlima Kilimanjaro wakaona kuna fursa ya kuitangaza Kenya kwa kupitia Mlima Kilimanjaro. Je sisi Watanzania tuliona kwamba fursa tuliyonayo tunaibiwa? Kama tuliona tulichukua juhudi gain za haraka kubadili hali? Tulichukua muda mwingi sana, hata sina hakika kama hiyo hali tumeweza kuibadilisha.
Mfano nakumbuka kuna kipindi mwaka uliopita mwezi kama huu nilienda posta kutaka kulipia kodi ya sanduku langu la posta kwa ajili ya mwakani,niliambiwa kuwa hawajaanza kupokea malipo ya mwakani hadi tarehe 1 Januari ndio wataanza kupokea,mimi nilitaka kuwahi kulipa kwa sababu nilikuwa nataka kusafiri.
Sijawahi kuona taasisi inapelekewa pesa halafu inazikataa, katika uhasibu kuna kitu kinaitwa “prepayment” au malipo ya kabla,sikuelewa kwa nini mfumo huo haupo. Baadae shirika likifa kwa kushindwa kujiendesha tunaanza kutafuta mchawi na kutafuta ubia, watu watakaoshiriki katika kusaini mkataba wanakuwa ni wale wale wanaokataa pesa kwa kutakujua “prepayment”. INASIKITISHA SANA.
Watanzania lazima tufike mahala tukubali kuwa hasara moja wapo ya Ujamaa ni kutokuwa na mawazo ya kibiashara ya kisasa, na TUBADILIKE.
Naomba kutoa wito kwa Watanzania wenzangu kuwa malumbano ya kusema wakenya wanafanya hivi,wanafanya vile hayatatusaidia. Kitu kitakachotusaidia kwa wasomi wetu kuna na mtanzamo wa uchumi wa kisasa katika biashara, utawala,n.k. Tanzania leo hii ina wasomi wengi sana, lakini pale walipokaa hakuna tofauti ya kitu chochote katika kile mtu anachokiongoza au kukifanya.
Wengine ni maprofesa na wengine ni madaktari lakini katika sehemu zao za kazi na shughuli mbalimbali hakuna maendeleo wala ubunifu wowote unaopatikana liwe ni shirika binafsi au Serikali, hakuna jipya inasikitisha sana.
Mdau Mtanzania,

No comments: