Saturday, December 27, 2008

SALAM ZA MHESHIMIWA BALOZI MWANAIDI SINARE MAAJAR KATIKA KUSHEREHEKEA SIKUKUU YA NOELI NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2009
Mheshimiwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Mama Mwanaidi Sinare Maajar, akitoa salam za Noeli na Mwaka Mpya
The Original Comedy, waalikwa wengine na Maofisa wa Ubalozi wakipata Msosi wa pamoja baada ya kupokea salam za Sikukuu ya Noeli na Mwaka mpya toka kwa Mh. Balozi Mwanaidi Sinare Maajar.

Ndugu Watanzania wenzangu,
Kwa mara nyingine tena tumepata fursa ya kufikia kipindi muhimu cha mwisho wa mwaka kwa kusherehekea kwa pamoja sikukuu ya Noeli na kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2009.

Kama ilivyo ada yetu, napenda kujumuika nanyi katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi hiyo.

Kwa niaba ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa niaba ya wafanyakazi wenzangu katika Ubalozi wa Tanzania London, na kwa niaba yangu binafsi napenda kuwatakia heri katika kipindi hiki muhimu.

Katika kipindi cha mwaka mmoja Watanzania waliopo Uingereza na Jamhuri ya Ireland wameshuhudia harakati zetu mbalimbali za kuhakikisha wanaimarisha ushirikiano kati yao. Pamoja na kasi ndogo katika harakati hizo, tumeshuhudia mafanikio yaliyotuwezesha kuanzishwa kwa Jumuiya za Watanzania sehemu mbalimbali, zikiwemo Birmingham na Edinburgh.

Huu ni mwanzo mzuri kuelekea kwenye ushirikiano thabiti wa Watanzania waliopo Ughaibuni (Diaspora). Aidha, mwaka 2008 umekuwa na mafanikio makubwa kwa kuweza kufanya Mkutano wa Diaspora hapo Mwezi Aprili.

Mkutano huo ulikuwa na mafanikio makubwa kwanza kwa kuweza kuwakutanisha zaidi ya Watanzania 400, wawakilishi wa kampuni zinazotoa ajira Tanzania na wawekezaji.

Ubalozi wenu unaendelea kufuatilia mapendekezo ya Mkutano huo na kwa kushirikiana na Tanzania Association (TA) tumeshaanza kufikiria kuandaa Mkutano mwingine wa Diaspora kwa kushirikisha washiriki wengi zaidi.

Tunaendelea pia kuwa na azma yenye imani kubwa ya kuwaunganisha Watanzania wote waliopo Ughabuni, si hapa Uingereza na Ireland tu, bali na Ulaya nzima na Amerika.

Tutafanikiwa endapo tutaendelea kuwa na mshikamano thabiti na ushirikiano wa kupigiwa mfano sisi wenyewe kwanza.

Natarajia mtaendelea kusherehekea pamoja fursa hii na kukumbushana kwamba Umoja ni nguvu na siku zote Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe.

Nawatakieni nyote Noeli njema na heri ya Mwaka Mpya.
Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania.

BALOZI MWANAIDI SINARE MAAJAR





No comments: