Tuesday, December 23, 2008

Matokeo ya darasa la saba 2008: Kiingereza, hisabati bado not richebo shule za msingi
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe akitangaza matokeo hayo

Asilimia 80.73 ya wanafunzi 433,260 waliofaulu darasa la saba wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza katika shule za serikali ambapo wasichana ni 188,460 sawa na asilimia 82.13 na wavulana 244,800 sawa na asilimia 79.69 .

Akitangaza matokeo hayo jana mchana kwa waandishi wa habari, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe (pichani) alisema kuwa kati ya wanafunzi wote 1,017,967 sawa na asilimia 97.51 ya walioandikishwa walifanya mtihani huo mwaka huu na wanafunzi 536,672 sawa na asilimia 52.73 wamefaulu.

Katika matokeo hayo ambayo yataanza kutangazwa na kila mkoa kesho, wavulana walifanya vizuri zaidi ambapo walikuwa 307,196 sawa na asilimia 59.75 huku wasichana waliofaulu ni 229,476 sawa na asilimia 45.55.

Aliitaja mikoa iliyofanya vibaya na kiwango cha ufaulu kwa asilimia kwenye mabano ni Shinyanga(34), Lindi(40.7), Mara(42.6) na Tabora asilimia 43.2.Kwa Mikoa iliyofanya vizuri ni Dar es Salaam(73.9), Arusha(69.2), Iringa(64.1) na Kagera 63.5.

Kwa upande wa wanafunzi waliobainika kufanya udanganyifu alisema “watahiniwa 102 wamefutiwa mitihani wakiwemo wasichana 41 na wavulana 61”.

Akifafanua juu ya ufaulu wa masomo ya Hisabati na Kiingereza ambayo kwa miaka miwili mfululizo umekuwa wa chini, Profesa Maghembe alisema kuwa Hisabati ni asilimia 18.07 huku Kiingereza ni asilimia 31.5

Ameongeza: “matokeo ya Kiingereza ni sawa na mwaka jana na Hisabati mwaka jana ni asilimia 18.72, tumeweka mikakati ya kuboresha masomo hayo ikiwemo vyuo vyote vya ualimu kutoa nyenzo kwa wanafunzi wa ualimu kuweza kufundisha masomo hayo, kuwapa mafunzo walimu waliopo na tunatoa wito kwa wanafunzi wasiyaogope masomo haya”.

Ufaulu wa masomo mengine na kiwango katika asilimia ni Kiswahili(73.4), Sayansi(68.24) na Maarifa(61.03).
Waziri Maghembe alisema kati ya wanafunzi 346 wenye ulemavu waliofanya mtihani huo, wanafunzi 221 sawa na asilimia 64 ya watahiniwa wamefaulu na wote wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza.

No comments: