Saturday, December 6, 2008

mjadala wa ist afrika mashariki: aluta kontinyua!!
Hii ni safu iliyoka Majira Jumapili iliyopitaNovemba 30, 2008.
Desemba 14 itatoka nyingine.
Tathmini Kutoka Washington,
Na Mobhare Matinyi
Ardhi ya Tanzania ni ya Watanzania tu!

HIVI karibuni jirani zetu hasa Wakenya, wamekuwa wakipiga kelele kulalamikia serikali yetu tukufu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hasa hii ya Rais Jakaya Kikwete, kwamba inazorotesha juhudi za kurahisisha nyendo za watu, ukazi wa kudumu na umilikaji ardhi Afrika Mashariki.

Kelele za majirani zimeongezeka katika siku za karibuni baada ya mjadala wa soko la pamoja kushika kasi. Kikao cha juzi juzi kisiwani Zanzibar kimeendeleza zogo hili. Hiki kilikuwa kimoja ya vikao vingi vya mchakatao huu ambao unafafa na ujambazi wa mchana kweupe.

Kama ilivyo kawaida kwa wenzetu Wakenya, kuropoka maneno makali hadharani kwao ni jadi, hata pale wasipokuwa na hoja.

Waziri wa Kenya aliyehudhuduria kikao cha Zanzibar, Jeffah Kingi, aliporejea kwao Nairobi alitoa tamko la kulalamikia hicho wanachokiita “ukwamishaji” wa Tanzania katika kufikia soko la pamoja na baadaye taifa moja.

Mara zote walalamishi hawa huwa hawaelezi kwa nini Tanzania inakwamisha, wao huwa ni kulalamika tu. Hivi nani aliwaambia kuwa ni lazima ardhi yetu igawanywe kwao? Wao ya kwao iko wapi? Watatupa nini cha mbadala? Kama haiwatoshi wasitupe shida, wajibane hivyi hivyo.
Waziri huyu wa Kenya hakuwa wa kwanza na wala si Kenya pekee, hivi sasa Rwanda na Burundi zimejiunga katika ulalamishi huo. Aidha, katika kikao kingine cha hivi karibuni kilichofanyika nje ya Tanzania, ilifikia mahali eti Rwanda na Burundi zinajadili misamiati ya kutumia kwenye kuhalalisha umilikaji ardhi.

Labda niulize swali: Kati ya Rwanda na Burundi, kuna anayetegemea kuwa watu wake watakwenda kwenye nchi nyingine kumiliki ardhi? Hivi Ututsi na Uhutu utakuwa umekwisha lini? Kujazana kwa watu Burundi na Rwanda kutaruhusu vipi umilikaji ardhi kwa watu wasiokuwa wazawa?

Jibu ni rahisi sana: Wanachotaka ni kuhamishia mamilioni ya watu kwenye ardhi ya Tanzania. Basi! Haiwezekani Mnyarwanda akahamia Burundi au Mrundi akahamia Rwanda, tusidanganyane mchana kweupe!

Uganda ingawa haijaanza kulalamika sana, lakini Rais wake, Yoweri Museveni alishawahi kusema maneno fulani na kisha kuyakimbia mwenyewe. Bahati nzuri kwa Uganda, ni nchi ya wanyonge wanaokimbizwa na Museveni mwenye ajenda za kisiasa na kiutawala huku vita vikimuandama.

Hata hivyo, Waganda nao wameanza kushituka na kujiuliza hivi wanataka nini kwenye hii Jumuiya ambayo Wakenya wako mstari wa mbele kuitaka iwe Shirikisho ghafla. Mwezi uliopita wakati akizungumza kwenye semina ya Taasisi ya Wahasibu Uganda (ICPAU), Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wauzaji Bidhaa Nje cha Uganda, George Walusimbi, alionya kwamba Waganda wawe waangalifu na hili wazo la soko la pamoja la Afrika Mashariki.

Tatizo la Walusimbi pengine lilikuwa kuitilia mashaka sekta binafsi ya Tanzania, na kutolea mfano wa makao makuu kuwekwa Arusha. Sikumuelewa. Nadhani ingawa alijitahidi kuwaonya Waganda lakini alipotea kwenye kutoa sababu. Hata hivyo inaonesha kwamba Waganda wanaanza kujihoji.

Hivi karibuni wakati wa kikao kilichofanyika Kampala, Mkurugenzi mmoja kwenye Wizara inayoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki ya Uganda, Edith Katende, alisema: “Kwetu sisi, Waganda, Wanyarwanda na Warundi, tunachotaka ni kuwa na urahisi wa kuzifikia bandari ili watu wafanye biashara kirahisi, wapate fedha.” Haya ni maneno ya ubinafsi wa waziwazi.

Ofisa mwingine wa Kenya, Barrack Ndengwa, alisema kwamba kufikia mwaka 2010 lazima soko la pamoja lililo huru liwe limesimikwa Afrika Mashariki huku waziri wa Uganda, Gaggawala Wambuzi, akisema mwaka 2009 tu mambo yatakamilika.
Naye Naibu Waziri wa Burundi akiwa Kampala pia, Nduwimana Deogratius, alisema kuhusu soko hili: “Mambo yanakwenda vizuri.”

Wakati viongozi wa Uganda, Rwanda na Burundi wakiendelea kutoa matamko yenye matumaini kwao na hata ya kulazimisha, Wakenya wao wanaendelea na lugha yao ile ile ya kijeuri. Lugha chafu, ujeuri na kiburi ni ugonjwa kwa wenzetu hawa. Hivi nani asiyejua kuwa tatizo kubwa la Kenya ni ardhi?

Lakini turejee kwenye mada, hivi kuna sababu gani ya Wakenya kutulaumu hivi? Kwani ni lazima tuungane? Hebu tujikumbushe kidogo. Miaka ya 1960 wakati Waafrika tukipigania uhuru, Mwalimu Julius Nyerere aliwaambia Wakenya na Waganda kwamba ataichelewesha Tanganyika kupata uhuru hadi wao watakapokuwa tayari, kisha tuungane na kuwa nchi moja.
Nadhani ambao hata hatukuwepo tunajua majibu yalikuwaje. Mwaka 1967 Nyerere tena akawaweka pamoja wenzetu hawa na ikaundwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Miaka kumi baadaye Uganda ikiwa na mwendawazimu Idi Amin na Kenya ikiwa na Mzee Jomo Kenyatta, wakaivunja Jumuiya. Mabwana wakubwa hawa hawakujali umoja.

Jumuiya ilipovunjika mwaka 1977, Wakenya walisherehekea kwa mvinyo na Waganda hawakujua kinatokea nini kwani Dikteta Amin alikuwa anawamaliza kwa risasi. Chuki na dharau ya Wakenya kwa Tanzania ikafikia kilele, wakatucheka sana na Ujamaa wetu na wakajivuna na viwanda vyao wa Wazungu na Wahindi. Safi!

Kwenye miaka hiyo pia, Tanzania tulikuwa tukitumia kila senti yetu, ardhi na damu yetu kuwapigania wenzetu wa kusini mwa Afrika ili wapate uhuru. Tanzania ilikuwa makao ya kila wapigania uhuru, achilia mbali Kamati ya Ukombozi wa Afrika. Wakenya wajipendekeza kwa makaburu na nchi za magharibi, wakadharau harakati za ukombozi kusini mwa Afrika. Hawakujali umoja.

Wakati Watanzania tunajenga Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar, Wakenya walikuwa wanajenga ukabila. Leo hii ni wavunaji wazuri wa ukabila. Mabwana wakubwa hawa. Nasikia wanatuonea wivu sana, na hata Rais wao wa zamani, Daniel Arap Moi alikuwa akiwasihi waige Tanzania. Safi sana!

Hata hivyo baada ya kuvunjikia kwa Jumuiya mwaka 1977, Watanzania hatukujali sana pamoja na hasara kubwa tuliyopata ilihali wenzetu Wakenya wakifaidika. Marehemu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine, alianzisha mkakati wa uhusiano na Kenya.

Mzee Ali Hassan Mwinyi alipokuwa Rais aliwakalisha Moi na Museveni na kuzungumzia mali na madeni. Hatimaye wazo la Jumuiya likarejea tena. Mambo yakaanza vema lakini kumbe wenzetu walibaini mwanya ambao sasa unaonekana wazi.

Wakati wa Rais Benjamin Mkapa wazo la Jumuiya lilizaa Shirikisho na sasa umekuwa mzigo. Kimsingi, nionavyo mimi, hii mijadala inayoendelea ni unyang’anyi. Inasikitisha sana kwamba Watanzania tumefikishwa hapa huku tukitukanwa. Hivi tangu lini Wakenya wakajua umoja kuliko sisi? Hii hata mtoto mdogo hadanganywi.

Mambo kama kuruhusu eti mtalii akija Afrika Mashariki atumie viza ya nchi moja kuzunguka kwenye nchi zote, ni wizi wa mchana. Tanzania hivi sasa tunajenga utalii wetu kwa nguvu, na serikali inatumia mamilioni ya dola kuitangaza nchi. Inawezekanaje mwisho wa siku tuchangie faida ya watalii.

Upo ukweli kwamba Kenya ilijitangaza zaidi kuliko sisi huko nyuma, ikiwa ni pamoja na kutumia Mlima Kilimanjaro, na imejenga miundo mbinu bora ya utalii. Kwa mazoea tu, watalii wote watakuwa wakifikia Kenya, na kuingia Tanzania bila kulipa viza kwetu. Tatizo la ulaghai lililokithiri Kenya kwa watalii tunalijua; hivi tuna sababu gani ya kuongeza shida hii ya viza? Hii ni dhambi.
Wakati mwingine huwa najiuliza, hivi kama si busara na ushujaa wa Rais Kikwete hivi karibuni kukataa maoni bandia yaliyowasilishwa na Tume ya Amos Wako, Mwanasheria Mkuu wa Kenya, tungekuwa wapi? Akina Wako walidai eti watu wa Afrika Mashariki wanataka shirikisho haraka.
Itakumbukwa kuwa Rais Kikwete baada ya kukataa ujanja ujanja huu, aliunda Tumeya Rais iliyoongozwa na Profesa Samuel Wangwe. Tume hii ilizunguka nchi nzima na asilimia 76 ya Watanzania wakasema hawataki kusikia Shirikisho mpaka hapo baadaye.

Nchi yetu siku hiyo ilikombolewa na kama kuna sifa anazostahili Rais Kikwete, basi ni hii ya kuiokoa Tanzania. Watanzania tuna tatizo la viongozi wetu kufanya maamuzi kwa maslahi ya watu wengine wa nje, lakini hapa tuliamka.

Na huu ni mfano mmojawapo unaoonesha kwamba tunahitaji mfumo wa kuangalia maamuzi yanayofanywa na kila upande kabla ya utekelezaji, yaani urari wa madaraka. Hebu fikiria kama tungekuwa na Rais asiye makini katika kulinda maslahi ya nchi, kingetokea nini?

Kimsingi Tanzania imepona kwa huruma ya Rais Kikwete, hebu fikiria kama angekubali mawazo ya akina Wako? Leo hii Watanzania tungekuwa tunapelekwa machinjioni. Na kama kuna mtu mwingine anayestahili sifa ni Waziri wa Afrika Mashariki, Dkt. Diodorus Kamala, na Naibu wake, Mohamed Aboud. Hawa watu wanastahili sifa kwa kuitetea Tanzania.

Naomba mniwe radhi wasomaji, najisikia kuwasifu mno viongozi hawa kwa sababu Watanzania tumezoea kuumizwa na viongozi wasiofanya maamuzi kwa maslahi yetu. Mifano ya mashirika ya umma yaliyouzwa, migodi yetu inayochimbwa na masuala ya umeme na gesi inajulikana na kila Mtanzania. Kwa taarifa tu, tunachekwa duniani kwa haya mambo!

Inapotokea viongozi wakafanya maamuzi kwa maslahi ya Taifa ni lazima tuwapongeze kwa vyovyote vile. Narejea tena pongezi zangu kwa serikali ya awamu ya nne, na kama tungekuwa hivi siku zote, mali zetu zisingepotea kijinga kama inavyotokea sasa.

Kutokana na mjadala huu kuwa nyeti, natarajia kupiga kambi kwenye suala hili kwa takriban mwezi mzima hivi. Wiki ijayo nitapekua zaidi sababu zinazowafanya majirani zetu watung’ang’anie.

Barua pepe:

No comments: