Friday, December 4, 2009

Tumekuwa Watu Wa Ovyo Ovyo!


Sio maneno yangu ila nikutoka kwenye mtandao nikaona nibora tushee pamoja uchoyo si mzuri jamani hata kwa makala.
Sanamu hiyo ya mzee anayepiga ngoma inayotoa maji ( sasa haitoi) nimeiona tangu nikiwa chini ya miaka mitano kiumri. Iko kwenye bustani ya Mnazi Mmoja wilayani Ilala. Nilipita mahali hapo jioni ya leo, pamenikumbusha utotoni. Ndio, ni enzi hizo ambapo wazazi wetu walikuja mahali hapo kupumzika nyakati za jioni na sisi watoto wao. Leo mahali hapo pamefungwa, watu wa Darisalama hawaruhusiwi kuingia hapo kujipumzisha. Muhusika hapo ameniambia wakiwaruhusu watu, basi huchafua eneo hilo hata kwa haja ndogo na kubwa! Kuna choo cha public mahali hapo, lakini ni cha kulipia.

Kwanini tunashindwa kuwa na taratibu zitakazorudisha utamaduni wa watu kujipumzisha bustanini kama ilivyo kwa jirani zetu wa Kenya pale Nairobi? Nahofia kuna watoto wa kizazi cha sasa ambao hawaelewi hata bustani ya kupumzikia ina maana gani kwao. Jamani, nahofia hata baadhi ya viongozi wakiwamo baadhi ya waheshimiwa madiwani wa jiji hawaelewi umuhimu wa bustani. Ndio, maana kuna kiroja kimetokea mjini na hakuna anayelalamika au kuandika gazetini. Pale viwanja vya Mnazi Mmoja siku hizi wanakodisha kwa ajili ya shughuli za harusi binafsi! Ndio, kwenye bustani ya umma.
Kuna wajanja wamejitengenezea kamradi kao.

Watu wa Darisalama lazima waamke na kukataa ujinga huu. Itakumbukwa miaka ya 90 enzi za Meya Kitwana Kondo kuna mfanyabiashara kwa jina la Baghdad alipewa ruhusa na jiji ajenge jengo la ghorofa la biashara katika bustani hiyo na chini kuwe na maduka yanayozunguka bustani. Basi, mfanyabiashara yule akazungushia mabati bustani ile tayari kwa ujenzi. Watu wa Darisalama walikataa ujinga ule, wakagawana mabati yale. Baadae Serikali kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ikapiga 'stop' ujenzi huo. Walichopigania watu wa Darisalama wakati ule ilikuwa ni haki yao ya kutumia viwanja hivyo kwa mapumziko. Kinachotokea sasa hakina tofauti sana na cha miaka ile ya 90. Viwanja vya umma vilivyotengwa kama bustani ya kupumzikia kwa umma vinabinaifsishwa kiholela. Kamwe, watu wa Darisalama na Watanzania kwa ujumla hatutakubali kuchungulia kwenye matundu ya ukuta , harusi na shughuli binafsi kwenye viwanja vya umma, tena vya kupumzikia. Wahusika wabadili utaratibu huu wa sasa, wavirudishe viwanja hivi vya umma vya kupumzikia kwa wenye navyo, wananchi. Kumbi za kufanyia sherehe binafsi ziko tele mjini!

No comments: