Tuesday, December 29, 2009

tarehe ya mwisho ya usajili wa namba za simu yasogezwa hadi juni 30 mwakani
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Profesa John Mkomwa akimbrifu Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aliyetembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya kimataifa ya mawasiliano huko Geneva mwezi oktoba mwaka huu. Katikati ni Naibu katibu mkuu wa ITU Houlin Zhao


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesogeza mbele kwa miezi sita zaidi tarehe ya mwisho la zoezi la kusajili namba za simu nchini ili kutoa fursa kwa wote wanaomiliki namba hizo kujisajili.

Tarehe ya mwisho ya kusajili
namba ya simu sasa ni Juni 30, 2010.

Awali TCRA ilitoa iliwajulisha wananchi kuwa kuanzia tarehe 1 Julai 2009 makampuni yote ya simu za mikononi yataanza kusajili wateja wao waliopo na wapya ili kuhakiki umiliki wa namba za simu wanazozitumia. Zoezi hili limeendelea kwa miezi sita na mwisho ulikuwa tarehe 31 Desemba 2009.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Profesa John Mkomwa amesema jana jijini Dar kwamba zoezi la kusajili simu limeenda vyema na kwamba takriban namba za simu milioni 6 zimeshasajiliwa.

Amesema ulazima wa kusogeza tarehe ya mwisho mbele umetokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa umeme na vitambulisho hasa sehemu za vijijini. Akaeleza imani yake kwamba ifikapo Juni 30 mwakani kila mmoja atakuwa ameshasajili namba yake.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inawahimiza wananchi kufahamu na kuzingatia mambo yafuatayo ambavo yametayarishwa kwa mfumo wa maswali na majibu kwa mujibu wa tangazo hilo la awali:

1. Swali: Kwa nini usajili namba ya simu?
Jibu: Kwa ajili ya kukulinda wewe na namba yako dhidhi ya matumizi mabaya ya simu.

2. Swali: Kitambulisho cha aina gani kitahitajika wakati wa usajili?
Jibu: Ili uweze kusajiliwa unahitaji kufika kwenye ofisi ya kampuni yako ya simu au wakala
wake na moja ya vitambulisho vifuatavyo ambapo utawapatia kivuli chake:-
(i) Kitambulisho cha mpiga kura
(ii) Pasipoti
(iii) Kitambulisho cha mfuko wa pensheni
(iv) Leseni ya udereva
(v) Kitambulisho cha SACCOS
(vi) Kitambulisho cha benki
(vii) Kitambulisho cha ajira pamoja na barua ya mwajiri
(viii) Kitambulisho cha chuo cha elimu ya juu
(ix) Kitambulisho cha uanachama kwenye kilabu
(x) Barua ya serikali za mitaa ikiwa na picha, sahihi na muhuri


3. Swali: Nisipojisajili ifikapo tarehe 30 juni, 2010 nini kitatokea?
Jibu: Namba yako itafungwa ili usiweze kuitumia kwenye mtandao wa simu nchini Tanzania.

4. Swali: Nani na wapi ninaweza kusajili namba yangu ya simu?
Jibu: Unaweza kusajiliwa na kampuni yako ya simu za mkononi au mawakala wao waliopo sehemu mbali mbali nchini.

5. Swali: namba ngapi za simu (simcard) ambazo ninaweza/ninaruhusiwa kusajili?
Jibu: Idadi yoyote kadri utakavyo.

7. Swali: Kuna uhakika gani wa usiri wa taarifa zangu nitakazotoa kwa kampuni ya simu za mkononi au wakala wao?
Jibu: Kampuni zote za simu nchini zinawajibika kwa mujibu wa sheria, kutunza taarifa za wateja wao ikiwa ni pamoja na taarifa za matumizi.

8. Swali: Taarifa zipi zinahitajika wakati wa usajili?
Jibu: Tafadhali angalia mfano wa fomuya usajili hapo chini:-


Imetolewa na
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)

No comments: