Wednesday, March 18, 2009

mallya wa chacha wange ala mvua 3
Deus Mallya akipelekwa kuanza kutumikia kifungo leo huko Dodoma

Kijana Deus Mallya (27) aliyekuwamo kwenye gari lililopata ajali na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kuendesha gari kwa mwendo kasi.

Hukumu hiyo iliyotolewa leo, ilimfanya wakili aliyekuwa akimtetea, Godfrey Wasonga, kulia mahakamani hapo na kusababisha shughuli za mahakama kusimama kwa sekunde kadhaa.

Wakili huyo alilia baada ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkoa wa Dodoma, Thomas Simba, kusoma vifungu vya kumtia hatiani mteja wake ambaye licha ya kuendesha kwa mwendo kasi, alihukumiwa kwa kuendesha gari bila leseni.

Hata baada ya hakimu kumaliza kusoma vifungu na kumtaka wakili atoe utetezi kabla ya hukumu, Wasonga alifanya hivyo huku akilia. Katika hukumu yake, Hakimu Simba alisema ameridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka ambao ulitolewa mahakamani hapo.

Hakimu alisema makosa aliyobainika kuyafanya Mallya, yana adhabu kali, lakini alimpunguzia kutokana na ombi la mshitakiwa. Katika kosa la kuendesha gari kwa mwendo kasi na kusababisha kifo, alisema kwa mujibu wa sheria namba 63 kifungu cha pili (A) adhabu yake ni kifungo cha miaka mitatu jela.

Alimhukumu pia kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la kuendesha gari bila leseni na kusema kwamba adhabu zote zinakwenda pamoja. Kwa mujibu wa hakimu, kifo cha Wangwe kilisababishwa na kubanwa mlango wa gari wakati wa ajali na kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na shahidi upande wa mashitaka namba nne, tano na sita, inaonyesha dhahiri mshitakiwa huyo aliendesha gari licha ya yeye kukana mashitaka hayo.

Hata hivyo, kabla ya hukumu kutolewa, Wakili Wasonga aliiomba mahakama itoe adhabu ya faini kwa mteja wake ombi ambalo lilitupiliwa mbali na mahakama. Awali, akijitetea kabla ya hukumu, Mallya aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kile alichodai kuwa ana wazazi wanaomtegemea.

Vilevile alidai kwamba anasomesha yatima na kwamba wapo vijana anaowasaidia kutokana na biashara zake na anamsomesha mdogo wake pia. Akizungumza baada ya hukumu nje ya mahakama, Wakili Wasonga alisema hajawa na uamuzi wa kukata rufaa hadi hapo atakapokaa na mteja wake (Mallya).

Ajali hiyo iliyosababisha kifo cha Wangwe na hatimaye kusababisha kijana huyo afungwe, ilitokea Julai 28 mwaka jana saa 2.30 usiku katika eneo la Pandambili, wilayani Kongwa takribani umbali wa kilometa 120 kutoka Dodoma.

Wangwe alikuwa akitoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ambako pamoja na masuala mengine, alikuwa akienda kuhudhuria mazishi ya mwanasiasa mkongwe, Bhoke Munanka.

Ajali hiyo ilizusha utata mkubwa baada ya familia ya Wangwe kudai kwamba ndugu yao aliuawa na hivyo kulazimu waite madaktari kufanya uchunguzi kabla ya kuzikwa nyumbani kwake, Kemakorere, Tarime mkoani Mara.

Mbunge aliyechukua nafasi yake ni Charles Mwera.

2 comments:

Anonymous said...

............Kwa ninavyokufahamu nilitegemea kuwa ungeandika ushabiki namna hii!. Uwezo wako wa kufikiri bado uko chini sana hadi kufikiria kufanya hii ni stori kwenye blogu yako???? Dah! Sasa huwa unafanya nini kama unakopi na ku paste halafu unaongeza maneno ya umbea??!!

Anonymous said...

POLE SANA MALYA