Wednesday, July 16, 2008

TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI...
-----------


Idara ya sanaa na Sanaa za Maonyesho ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam itaendesha kongamano la muziki na uhusiano wa fani hiyo na jamii ikiwa ni moja kati ya fani ambazo ni kielelezo muhimu cha Utamaduni wa taifa.Kongamano hilo ambalo linajulikana kitaalamu kama Ethnomusicology 2008 litafanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 17-19 Katika ukumbi wa Idara ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sanaa Dkt. Herbert Makoye alisema mihadhara katika kongamano itatolewa na wanataaluma waliobobea katika muziki wa Afrika na kwamba pamoja na mihadhara,kongamano litapambwa na maonyesha ya filamu na muziki.“Ni kongmano la aina yake ambapo pamoja na mada pia kutakuwa na maonyesho ya filamu,watakuwepo wataalamu waliobobea akiwemo Profesa Kelly Askew kutoka Chuo Kikuu cha Michigan ambaye ni mwongozaji wa filamu na mwandishi wa kitabu kiitwacho Performing the Nation: Swahili Music and Cultural Politics in Tanzania,” alisema Makoye.

Aliongeza kuwa Profesa Kelly atatoa mada inayosema ‘Maombolezo ya Mwalimu:Laments for a Sung Hero’ na pia ataonyesha filamu yake kuhusu miaka 100 ya taarabu huko Zanzibar.Filamu hii mpya inaitwa Poetry in Motion:100 Years of Zanzibar's Nadi Ikhwan Safaa ambayo imeitengeneza mwaka huu.Pia atakuwepo Professor Barbara Lundquist kutoka Chuo Kikuu cha Washington ambaye atatoa mhandara kuhusu muziki wa Cuba na matumizi ya muziki kutoka jamii mbalimbali ulimwenguni,shuleni na vyuoni.

Professor Diane Thram ambaye ni Mkurugenzi wa Maktaba ya Kimataifa ya Muziki wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Rhodes nchini Afrika Kusini ambaye atazungumzia kuhusu njia za kisasa za kukusanya na kuhifadhi muziki wa Afrika na pia atazungumzia kuhusu matumizi ya muziki katika shughuli za kitabibu na za kidini katika jamii za Wazimbabwe.“Wasemaji wengine katika kongamano hili ni wahadhiri na wanafunzi katika Idara ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,wanamuziki kutoka chuo cha Muziki wa Nchi za Majahazi cha Zanzibar ambapo wasanii kutoka kikundi cha Muheme kutoka Chamwino Dodoma watafanya maonyesho na kwamba kongamani ni la wazi kwa kila mtu kushiriki,”alisema.

No comments: