Kijana anayetuhumiwa kula watu acharuka mahakamani
Na Nora Damian
MTUHUMIWA Ramadhani Mussa (18), anayedaiwa kumuua mtoto Salome Yohana (3), jana aliuohoji upande wa mashitaka sababu za kuchelewesha upelelezi wa kesi yake.
Baada ya Ramadhani kupandishwa tena kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mwendesha Mashitaka Hudson Nduysepo alieleza kuwa upelelezi wa shitaka hilo bado haujakamilika.
Mara baada ya Mwendesha ashtaka huyo kutoa maelezo hayo na kabla hajaruhusiwa na hakimu Ramadhani alisimama na kuhoji sababu za upelelezi wa kesi inayomkabili yeye na mama yake Hadija Ally (38), kuchukua muda mrefu kukamilika. Pia alitaka alezwe ni lini upelelezi huo utakamilika.
''Kila siku tukija mahakamani tunaambiwa upelelezi bado, je utakamilika lini,'' alihoji Ramadhan.
Hakimu Euphamia Mingi anayesikiliza kesi hiyo alimtaka Ndusyepo kujibu hoja hiyo, naye akaeleza kwamba upelelezi unachukua muda mrefu kwa sababu kesi hiyo ni tofauti na kesi nyingine za kawaida ambazo upelelezi wake unatakiwa ukamilike ndani ya siku 60.
''Endelea kuwa mvumilivu kwa sababu kesi hii ni ya mauaji na lazima tufanye upelelezi kwa kina, ili kuhakikisha tunazitendea haki pande zote mbili,'' alisema Ndusyepo.
Wakati Ramadhani akihoji hayo, mama yake alikuwa amekaa kimya. Hata hivyo, mtuhumiwa huyo alionyesha kutoridhika na maelezo hayo.
''Kwa hiyo inawezekana mkatumia hata miaka 60 mnafanya upelelezi. Kwanza mimi sijaua, lakini kila siku mnanileta mahakamani na kunirudisha, ni afadhali msinilete mpaka mkimaliza upelelezi wenu ndiyo mnilete hapa,'' alisema Ramadhan.
Hakimu Mingi baada ya kusikiliza hoja zote aliuagiza upande wa mashitaka kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 11, mwaka huu itakapotajwa tena.
Ramadhan alikamatwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akidaiwa kwamba alikuwa amebeba kichwa cha marehemu Salome Yohana (3).
Awali ilidaiwa katika mahakama hiyo Aprili 24, mwaka huu kwamba majira ya usiku mtuhumiwa alimuua mtoto huyo katika eneo la Segerea kwa Bibi, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment