Thursday, July 24, 2008

Taarifa kwa Vyombo Vya Habari.
*Shaggy Kuwasha Moto Bongo

Pichani ni mkurugenzi wa PrimeTime Promotions Godfrey Kusaga akizungumza na waandishi wa habari leo asubuhi ndani ya Idara ya habari MAELEZO jijini Dar es Salaam.

------------

Ndugu zetu, kwa mara nyingine tena tumekuja kuendeleza ile jadi yetu ya burudani ambapo mara kwa mara,tunakuwa tunajitahidi kuhakikisha kwamba medani ya burudani hailali, kila kukicha inakuwa na kitu cha kuchangamsha mashabiki wake, kuwaelimisha, na kutoa nafasi kwa wanamuziki wa nyumbani kujifunza zaidi kuhusu muziki ulio katika kiwango cha kimataifa

Leo tumekuja kuwatangazia ujio wa mwanamuziki maarufu wa muziki wa Ragga kutoka chini Marekani,Orville Richard Burrell,maarufu kwa jina la Shaggy,kutokana na matakwa ya mashabiki,Primetime Promotions tumeamua kumleta hapa ambapo atafanya onesho moja katika viwanja vya Leaders Club siku ya tarehe 8,mwezi Agosti mwaka huu, ambayo itakuwa ni sikukuu ya wakulima.

Shaggy ambaye kwa sasa anatamba na vibao kama Bonafide Girl,Sexy Lady,Why me,na vingine vingi anatarajiwa kuingia nchini akiwa ameambatana na kundi la wanamuziki 15 ambapo kama kawaida yake anapiga muziki wake kwa kutumia ala za muziki(Live Band),na atasindikizwa na wasanii mbali mbali wa nyumbani ambao muda si mrefu tutakuja tena hapa kuwatajia watakuwa ni akina nani,hii itakuwa ni baada ya tarehe 1.

Wanamuziki watakaoambatana na mwanamuziki huyu ni pamoja na Bancroft Bancombe,Fabian Smith,Bruce Brewste,Robert Livingstone,Oscar Ohare, Robert Browne, ShaunDarson,Natasha Watkins,Michael Fletcher, Paul Lee na NIgel Lynn.Wengine ni Patrick Morrison,Brian Thompson,Mario Gordon,na Jeffrey Esposito.

Hii ni mara ya pili kwa mwanamuziki huyu kuja nchini, mara ya kwanza alikuja mwezi Machi mwaka 2006, ambapo alifanya onesho lenye ubora wa hali ya juu katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha ambapo aliweza kukonga nyoyo za mashabiki kwa kiasi kikubwa sana.Sasa baada ya miaka hii miwili,ameweza kutoa vibao viwili ambavyo ni gumzo ikiwa ni utangulizi wa albam yake mpya ambayo bado hajaitaja jina.

Moja ya vibao hivyo ni Church Heathen, na cha kwanza ni kile cha Bonafide Girl ambavyo vinafanya vema katika chati mbali mbali za muziki huku video zake zikiongoza kwa kuoneshwa katika vituo mbali mbali vya Televisheni duniani na kusababisha mashabiki wa muziki wa Ragga kumpachika jina la Balozi wa muziki huo baada ya kufanikiwa kukaa kwenye chati tangu kuanza kujulikana katika medani ya muziki wa kizazi kipya. Ikumbukwe Shaggy alikuwepo tangu enzi za akina Shabba Ranks,na Chaka Demus and Pliers ambao kwa sasa hawasikiki sana kwenye anga za muziki wa kimataifa.

Kiingilio katika onesho hili la kimataifa kitakuwa ni shilingi 7,000 tu za kitanzania. Hii imewekwa kwa makusudi ili kila shabiki, bila kujali tabaka, aweze kushuhudia onesho hili la kimataifa ambalo linatarajiwa kuwa na sura mpya katika utamaduni wa matamasha nchini.

Haya ndio kwa leo tuliyowaletea ndugu zetu, tunaomba ushirikiano wenu, tutakuja tena kuwaambia kitakachokuwa kinaendelea kuhusiana na ziara ya mwamuziki huyu, ahsanteni

Godfrey Kusaga
Mkurugenzi
PrimeTime Promotions