Tuesday, July 29, 2008

Makachero walaaniwa bungeni kwa uvamizi ofisi za Gazeti Mwanahalisi *Mkurugenzi Mawasiliano Ikulu alipuliwa

*Ambiwa hana tija, upinzani wataka nafasi ifutwe

Na Ramadhan Semtawa, Dodoma

SAKATA la makachero wa Polisi kuvamia na kupekua ofisi za Kampuni ya Halihalisi Publishers, limeingia katika sura mpya baada ya baadhi ya wabunge kulaani na kuitaka serikali itoe tamko kuhusu kitendo hicho.

Kauli za wabunge zitolewa wakati tayari wadau mbalimbali wamelaani kitendo hicho ambacho kinatishia uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Wabunge kwa nyakati tofauti, walitoa kauli hizo mjini hapa jana wakati wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni

na Michezo, kwa mwaka 2008/09.

Dk. Raphael Chegeni (Busega-CCM), alikuwa wa kwanza kulaani uvamizi katika ofisi hizo na kumpekua Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Saed Kubenea, akikiita kuwa ni chenye kutishia uhuru wa vyombo vya habari nchini. Kampuni hiyo mdiyo inachapisha magazeti la MwanaHalisi na Mseto.

Chegeni alifafanua kwamba vyombo vya habari katika siku za karibuni vimekuwa na mchango mkubwa katika kufichua uovu ikiwamo ufisadi uliofanyika katika mkataba wa Richmond na katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Alisema ni lazima serikali ibadilishe mfumo wake wa utendajikazi na vyombo vya habari, ili kuweza kuondoa migongano isiyo na msingi.

''Nimesikitishwa na taarifa za kuvamiwa ofisi za gazeti la MwanaHalisi, vyombo vya habari vinafanyakazi nzuri, mambo ya EPA na Richmond yalianza kama rojorojo, na serikali iliwahi kukanusha ikisema ni uzushi tu, sasa haya mambo ya kupekuana ni kutisha waandishi,'' alisisitiza Dk Chegeni.

Hata hivyo, Dk Chegeni alionya na kukumbusha waandishi kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao kwani kama watapotosha wataiweka jamii katika wakati mgumu na

kuivuruga nchi.

Alisema habari ni uchumi na kuhoji sababu za kupuuzwa kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete,

ambalo liliweka utaratibu wa kutaka mawaziri kukunatana na waandishi kuzungumzia

mambo mbalimbali.

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, aliunga mkono hoja hiyo huku akiitaka serikali kutoa tamko kuhusu makachero kuvamia na kupekua ofisi ya Halihalisi.

Zitto alisema ni vema Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, (George Mkuchuika), akatoa maelezo na kisha leo Waziri wa Mambo ya Ndani atoe kauli wakati akiwasilisha hotuba ya mapato na matumizi ya wizara hiyo.

Alisema kama uharaka uliofanywa na makachero kuvamia ofisi hiyo ungeelekezwa katika

vita dhidi ya ufisadi, basi kwa sasa ungekuwa unakaribiakwisha.

�Napenda nichukue fursa hii, kuungana na wenzangu wote kulaani nguvu za polisi kukamata na kupekua ofisi za Halihalisi na Mkurugenzi wake ndugu Kubenea, haraka na

nguvu hizi zingeelekezwa katika vita ya ufisadi, saa hizi ingekuwa

imemamalizika,� alisisitiza Zitto.

Zitto akichangia ukuaji wa uhuru wa vyombo vya habari, pia alitaka serikali ichague kufanya jambo moja kati ya mawili ambayo ni kutoa ruzuku ya asilimia 100 kwa Shirika la Utangazi nchini (TBC) au kulicha liwe huru kufanya biashara.

Mbunge wa Mchinga (CCM), Mudhihir Mudhihir, ambaye amekua kimya kwa muda mrefu katika mkutano wa 12 unaoendelea mjini hapa, aliibuka na kuchangia hoja huku akitumia misamiati na misemo mbalimbali ikiwemo ya Kiarabu.

Mudhihir alisema kilichopo sasa ni kwamba kuna vyombo vingi vinavyobika, ambavyo baadhi yao hutaka kupanda juu hata kuandika habari ambazo si sahihi.

Hata hivyo, alisema ni vema serikali ikawa na subira kwani chombo kimoja kikikosea si vyote na kuongeza: ''Padre mmoja akizini, si Ukristo wala Sheikh, Imam au Ustaadh, akizini si Uislam.''

Mudhihir aliendeleza hulka yake ya kutoa misemo kwa kusema, ''Kuna msemo kwamba, vijogoo vingihuharibu usiku, kuna vingine vitawika saa nne, lakini majogoo wa kweli watatulia, sasa hata magazeti yale ya kweli yatabaki tu.''

Awali katika hotuba mbadala ya kambi ya upinzani, iliyosomwa na Waziri Kivuli wa wizara hiyo Mwanawetu Said (Viti Maalumu �CUF), ililaani kitendo hicho na kuhoji vipi polisi ipoteze muda wa kukamata aliyetoa taarifa badala ya kufanya uchunguzi wa taarifa hizo.

Kambi hiyo pia ilimlaumu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, kwa kusema kazi ya kurugenzi yake hainonekani kutokana na tovuti ya Ikulu ambako ni ofisi ya Rais kutofanyakazi. Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais ni Salva Rweyemamu.

Msemaji huyo alisema tatizo hilo la tovuti ya Ikulu ni sawa na ile ya wananchi, ambayo huendeshwa na serikali kupitia Idara ya Habari (Maelezo), ambayo kwa muda wa mwaka mmoja sasa haifanyikazi na hata wananchi wakitaka kujibiwa maswali hayo hakuna

majibu wanayopata.

''Hatuoni umuhimu wa kuwepo Mkurugenzi wa Habari kama utendajikazi wake ndiyo huu,

tunashauri badala ya kuanzisha vyeo ambavyo havina ufanisi katika utendaji basi sasa

ni wakati wa kurudisha utamaduni wa kuwa na Mwandishi wa Habari wa Rais na majukumu

mengine chini ya wizara,'' alisema.

No comments: