Monday, July 21, 2008

MAKALA YA LEO..

Turejeshe fungate la Uhuru wetu
Na Deus Ngowi.
------------
WAMO; wamo kwenye ulimwengu, wabaya na wazuri, wote wanaangaziwa Jua na kunyeshewa mvua ya Manani pasipo ubaguzi. Wanauona mwanga wa mchana na giza la usiku, pasipo kusahau mwanga wa usiku uletwao na mwezi.

Wengine wamo kwenye mstari sahihi, japokuwa daima hawakosekani waliokwenda mchomo, kwani tabia hazifanani na wakorofi si wachache kwetu hapa;na kwao huko pia.Wamo;katika makundi tofauti kisiasa,kiuchumi,kitamaduni na mengine mapya ya siku hizi.Wamegawanyika.
Ni tofauti na siku zile za mwanzo,mfano wa FRELIMO(Frente de Libertação de Moçambique) kilichoikomboa Msumbiji,chini ya shujaa Samora Machel,ambaye kwa sasa ametangulia mbele ya haki,wote wakienda pamoja kwenye mstari sahihi,wenyewe wakijipiga vifua, wakijipongeza na kuimba kwamba wapo kwenye aligna correcta (mstari sahihi).

Alichosema Samora kilikuwa chao,na walichosema wao kilifanana na chake, kwa sababu walishakubaliana kwamba sasa basi wanachotaka ni uhuru wao,uhuru wa kweli,na kwamba kukaa katika nira ya mauti halikuwa chaguo lao.Alibeba jukumu hilo baada ya kufariki dunia Eduardo Mondale 1969.FRELIMO ilianzishwa hapa Tanzania, na nchi yetu imekuwa kitovu cha uhuru wa nchi nyingi kusini mwa Afrika.

Waliokuwa Msumbiji, na waliokuwa karibu na Wamachinga hao hapa kwetu wakati huo, wanakumbuka ilivyokuwa ikiimbwa (na Watanzania pia)“Viva,Viva a FRELIMO”(FRELIMO idumu),ukawa wimbo wao wa Taifa tangu Juni 25,1975 hadi Aprili 30,2002 walipoubadilisha.Ni sawa na kaka na dada zao wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)walivyoimba,wakaimba na sasa bado wanasema “Kidumu Chama Cha Mapinduzi.”Wengine sasa wameweka utani,wakisema kigumu.
Na vyote bado vipo, na vinatawala au vinaendesha serikali halali za nchi zao. Sawa, vidumu.
Uhuru wa nchi moja huimarisha wa jirani yake, ndiyo maana Mwalimu Nyerere akasema afadhali uhuru wa Tanganyika uchelewe ili Afrika kwingineko nao wawe huru. Wakafanya harakati nyingi, ikiwa ni pamoja na kuleta uhuru uliochelewa wa Zimbabwe, ambao kamaradi wetu, ndugu yetu na mwenzetu wa zamani aliyekuwa kwenye mstari sahihi, Robert Mugabe anauharibu.

Siku kama ya leo ilikuwa ya furaha kwa mateka 105 kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebbe mwaka ule wa 1976, kwa sababu makomandoo wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) walifanikiwa kuwaokoa, kupitia operesheni iliyoitwa Yonatan. Walifanikiwa kuwaondoa mateka kwenye kifungo, pingu, upweke, wasiwasi na hofu kuu. Wengine hupenda kuiita Operation Thunderbolt, lakini ilikuja kupewa jina hili la Yonatan kwa heshima ya Luteni Kanali Yonatan ‘Yoni’ Netanyahu aliyeuawa katika operesheni hiyo. IDF hadi sasa inaendelea kulinda uhuru wao, na daima wamo kwenye fungate.

Uhuru ni jambo zuri, lakini uhuru lazima uwe na mipaka yake, kwa sababu unapoishia uhuru wako, ni hapo hapo unapoanza wa mwingine au unapokaribia kuingilia uhuru wa mwingine, ni mwisho wa uhuru wako. Hata hivyo, uhuru wa nchi nyingi umepatikana baada ya mauaji ya watu. Na hata baada ya uhuru, maadui wameua walioleta uhuru, mfano mmojawapo ukiwa ni Samora Machel.

Ikiwa Tanzania ndiyo kiini cha uhuru wa nchi nyingi kusini mwake, kuna kila sababu ya yenyewe kuhakikisha inaulinda kwa nguvu zote uhuru wake, na wananchi wanafaidi matunda ya uhuru. Kwamba uhuru wa Hassan usitofautiane na wa Yohana, lakini pia wa Mwajabu usizidi ule wa Maria. Yaani kila mmoja atendewe sawa, haki na haki tupu pasipo nyongeza wala punguzo, japokuwa tunajua sawa haiwezi kumaanisha sawa sawa kabisa.

Ni kutokana na hayo, kuna kila sababu za kurejea tena maagano yetu, viapo vyetu na fungate letu la uhuru. Tuamke na iwe kana kwamba uhuru umekuja jana. Tujikumbushe sababu zake, jinsi ya kuulinda na jinsi ya kuufaidi wote.

Siku zinakwenda na miaka inapita, ya jana si ya leo, wala ya kesho hayatafanana na ya keshokutwa. Tutafika mahali kujilaumu kwa kutoshiriki matunda ya uhuru wetu. Alice Chase, katika shairi lake aliloelekeza kwa mwanaye 2005, ambaye sasa amekua na hawakai pamoja tena, anasikitika kwamba zama zake hakufanya mema, ambayo anatamani kuyafanya sasa, lakini wakati ukuta.

Anasema maisha ni mafupi na miaka inakwenda kasi sana, mvulana anakua haraka, hakai tena pamoja na mama yake na mambo yake mengi yanakuwa ya siri. Hawatazami tena picha pamoja kitabuni, hawachezi tena, hawapigani busu la alamsiki usiku baada ya kusali kama zamani. Anataja mengine mengi kwa masikitiko, akisema siku hizo zimepita, ni miaka mingi nyuma, na hawezi kurejea huko.
Kwamba mikono yake sasa haina kazi kwake, imekaa tu, siku inakuwa ndefu akikosa cha kufanya na anatamani angerejea siku hizo na kufanya mengi kwa mwanawe.
Nembo za uhuru wetu zipo nyingi, kwa uchache ni bendera, wimbo wa Taifa na sarafu. Lakini pia sie ni tofauti na nchi nyingine, tunao Mwenge wa Uhuru, ambao uliwashwa na kuwekwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, lengo likiwa ni kumulika kote ndani ya mipaka yetu.

Kadhalika ni kwa ajili ya kurejesha amani palipo na chuki, matumaini penye mkato wa tamaa na kuangaza wabaya wote (siku hizi wanaitwa mafisadi) popote walipo. Hata hivyo, kama ilivyoelezwa awali, Mwenge wetu bado haufanyi ile kazi yake, haumuliki tena ipasavyo wala kuleta matumaini inavyotakiwa.

Badala yake umekuwa wenye usumbufu mkubwa kwa baadhi ya watu, hasa wanyonge, kote unapokimbizwa, ukimaliza fedha za watu kununulia mafuta na hata kuwaathiri kiafya wanaoukimbiza. Kumi ni uchafu unaofanywa na baadhi ya wanaokuwa kwenye mikesha yake, mijini na vijijini.

Ndio maana inashangaza waziri mwenye dhamana ya Mwenge, Athumani Kapuya anaposema Mwenge hauchochei hata kidogo maambukizi ya Ukimwi, badala yake watu wanaokesha humo hupata mafunzo mazuri tu. Lakini wanaokuwa huko wanafahamu vizuri, na hata asubuhi baada ya mkesha watu huokota kondomu zilizotumika katika uchafu huo. Na Kapuya anafahamu hayo, lakini badala ya kuangalia Uhuru unalindwaje na kuenziwa vipi, anaishia kutoa majibu ya kisiasa wakati suala ni la kijamii na hatari kubwa kwa Tanzania na watu wake.

Mikesha hiyo ni moja ya nyenzo za kupukutisha watu wetu, hasa vijana, ndio maana inashauriwa ama Mwenge uzimwe kabisa au turejee maagano, viapo na kuuenzi Uhuru wetu ambao kwao Mwenge ulianzishwa.

Lakini uhuru unatakiwa uwanasue wadogo au wanyonge kwenye madhila, kama alivyopata kusema Machel. Uondoe dhiki na kwa kasi kubwa usaidie kuondoa maadui aliowataja Mwalimu Nyerere – ujinga, maradhi na umasikini kwa sababu tunayo ardhi na watu. Uhuru utadumishwa vema na kuenziwa iwapo tutakuwa na siasa safi na uongozi bora katika kila ngazi. Na tuanze sasa kurejea kwenye fungate la uhuru wetu, tusiusahau na kujifanya kama akina Mugabe sasa, wakijimaliza wenyewe kwa uchu wa madaraka na kujiona bora kuliko wengine.

Maadui hao hawawezi kuondoka katika mazingira ambamo Serikali (kwa maana ya wizara yenye dhamana ya kazi na ajira) inakaa na wakubwa wenye viwanda na kampuni kujadili kuwapunguzia wafanyakazi mishahara. Tena wanakaa baada ya kuwa kima cha chini kimeshatajwa, halafu wanawaruhusu kupunguza mishahara, huku wanyonge wakiwa hawana kimbilio.

Uhuru hauna maana yoyote ikiwa hata viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanawekwa kwapani kwa mwajiri, wanashiriki katika dhifa na hafla kila mara na kuzungumza lugha moja, huku wakiwacheza shere wafanyakazi wenzao.

Lini wanyonge hao nao watasikilizwa shida zao na wizara, kisha iwaruhusu kuongeza kima cha mishahara kiwe juu zaidi? Mwenye nguvu anaachwa apite na kuongezewa nguvu, huku mnyonge akinyang’anywa hata kile kidogo alicho nacho. Viongozi wanajikusanyia fedha tele na marupurupu mengi, wakikaa bure kwenye majumba na kupewa huduma kedekede, wakati mnyonge anafungwa na kukabwa kwa kodi katika hata kidogo anachopata. Hilo si fungate la uhuru, bali ni mfano mbaya kabisa wa unyonyaji.

Wenzetu majirani wanalinda uhuru wao kwa nguvu zote, na sasa wanaingia hata kwetu kutaka kuchukua ule kidogo ulio kwa watu wetu.Wanalinda uhuru wao kwa maana ya kuhakikisha wanafaidi rasilimali zao; madini, wanyamapori na kadhalika. Tazama Botswana, ambaye hoja zake za kiuchumi, hasa kuhusu utalii zilipata kuchapishwa na gazeti hili, wamekuwa ‘matawi ya juu’, sie tukibaki kula nyasi kavu na chafu za chini, kwa uvivu wetu wa kuchagua kuulinda uhuru na kudumu katika fungate letu la uhuru.

Wala uhuru hautalindwa kwa kuwanyanyasa wachezaji wetu wanaoonyesha uungwana kwa kubadilishana jezi na wenzao. Imesikika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likimdai fedha au fulana Nadir Haroub Cannavaro, eti kwa kubadilishana jezi na Samuel Eto’o Fils wa Cameroon walipocheza majuzi jijini Yaounde. Ni kituko na aibu kwa TFF kufanya kitendo hicho.

Uhuru wetu utalindwa kwa vyama kujijengea uimara, kuweka malengo ya siasa safi na uongozi bora, ili kutoka huko, wapatikane viongozi bora wa kitaifa kwenye serikali. Kuendelea kupoteza muda, kutatufanya tuje kujilaumu na wakati huo mwana atakuwa si wetu tena. Shime tuzingatie na turudi kwenye mstari sahihi, kisha tutasema kama enzi zile; “aligna correcta.”

No comments: