Friday, July 18, 2008

balozi wa redds 2008 kujulikana kesho mwanza
warembo wakila darasa huko mwanza katika kujiandaa na mchuano wa kumpata balozi wa redds
tizi la jinsi balozi wa redds atavyotafutwa
msosi wa haja
tabasamu kila mahali
ufukweni
bufee la nguvu

Mwanza, Julai 19, 2008:
Mchakato wa kumtafuta Balozi wa Mitindo wa REDD’S wa mwaka 2008 ambao umefanyika Mwanza unafikia kilele chake kesho Jumamosi usiku katika tukio la aina yake kwenye ukumbi wa NSSF jijini Mwanza.

Hii inafuatia wiki nzima ambayo ilijaa shughuli mbalimbali ndani na nje ya jiji hilo zote zikilenga katika kuhakikisha mshindi wa mwaka huu ni wa kipekee. Safari hiyo ya washiriki wa mchakato huo kwenye Kanda ya Ziwa pia ilijumuisha nafasi ya kihistoria ya kutembelea kaburi la Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Nyerere.

Akizungumzia kilele cha mashindano hayo, Meneja wa bia ya REDD’S, Bw. George Kavishe alisema,”Nina uhakika mchakato huu umefanikiwa kupata Balozi wa kweli wa Mitindo wa REDD’S, mtu ambaye anashabihiana na sifa za kinywaji chetu. Kinywaji cha REDD’S kina sifa za umahiri, utulivu, na mwonekano mzuri ambazo ni baadhi tu ya sifa zake na ninaamini tukio la leo litatuonyesha sifa hizi kama zilivyo.”

Akisubiri fainali za leo kwa hamu kubwa, Mkurugenzi Mkuu wa Beautiful Tanzanie Agency, Bi. Irene Kiwia aliongeza, “Washindani wana hamu mno na wako tayari kwa shindano la leo, siku ya leo imekuwa na shughuli nyingi lakini wasaa ukifika naamini kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.”

Angela Lubala, Mrembo wa Temeke wa mwaka 2008 alisema, “Kwa kweli hili litakuwa tukio la kukumbukwa kwa muda mrefu hasa miongoni mwetu washindani. Wakati mwingine ilionekana kama kazi ngumu sana lakini ilikuwa nzuri tu, tumejifunza mambo mbalimbali na nina hakika yote tuliyoyapata yataonekana leo usiku.”


Mchakato kumtafuta Balozi wa Mitindo wa REDD’S mwaka huu ulikuwa hivi:

Ijumaa Julai 11, 2008 – Washiriki walihudhuria semina Bagamoyo ambapo walipatiwa utaratibu mzima wa shindano la kumtafuta balozi wa REDD’S.

Jumamosi Julai 12, 2008 – Warembo waliondoka kuelekea Mwanza kwa ndege ya Air Tanzania na walipowasili walilakiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, baadaye walitalii mitaa ya jiji la Mwanza kwa gari na baadaye walikwenda Yacht Club kwa ajili ya chakula cha mchana. Jioni walifanya mazoezi yaliyofuatiwa na chakula cha usiku kwenye mgahawa wa Kiss Pub.

Jumapili Julai 13, 2008 – Baada ya kifungua kinywa warembo walicheza mpira wa wavu, chakula cha mchana kilifuata baadaye Tunza Lodge. Siku yao ilimalizika kwa chakula cha jioni Yacht Club baada ya bonanza iliyofanyika BoT.

Jumatatu Julai 14, 2008 – Washiriki waliianza siku kwa mazoezi na maandalizi kisha mkutano na waandishi wa habari La Kairo Hotel. Walibaki hapohapo hotelini ambapo baada ya chakula cha mchana walipima na kujaribu nguo kisha kurejea tena kwenye mazoezi. Chakula cha jioni kilikuwa hapohapo La Kairo Hotel.

Jumanne Julai 15, 2008 – Siku ilianzia studio za Kiss FM, baadaye warembo walielekea makao makuu ya Vodacom kabla ya kutembelea Hospitali ya Sekou Toure kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii. Walikula chakula cha mchana makao makuu ya Vodacom kabla ya kuingia tena kambini kwa ajili ya mazoezi. Siku yao ilimalizika kwa hafla ya jioni iliyofanyika Tilapia Hotel.

Jumatano Julai 16, 2008 – Washiriki walifanya safari ya kihistoria kwa kutembelea kaburi la Mwl. Julius Nyerere. Hii ilifuatiwa na chakula cha mchana na Mkuu wa Mkoa wa Mara na siku yao ilifungwa kwa chakula cha jioni na dansi iliyofanyika Multi Villa, Musoma.

Alhamisi Julai 17, 2008 – Warembo waliondoka Musoma kurudi Mwanza mapema asubuhi na baadaye kutembelea kiwanda cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambapo pia walikula chakula cha mchana. Baadaye walitembelea kituo cha kulelea watoto cha Starehe ambapo waliungana na wafanyakazi wa TBL katika shughuli za kijamii. Usiku walikula na kucheza dansi Kirumba Pub.

Leo Ijumaa Julai 18, 2008 – Siku itaanza kwa warembo kupima nguo wakiwa na wanamitindo na kisha kufanya mazoezi kabla ya kwenda Yacht Club kwa chakula cha mchana. Baadaye watakwenda La Kairo Hotel ambapo watafanya majaribio kwa ajili ya fainali na chakula cha jioni watakula TGIF Villa Park.

KESHO USIKU: Jumamosi Julai 19, 2008 – Siku iliyosubiriwa na kila mtu. Warembo wanatarajia kufanya mazoezi yao ya mwisho masaa ya asubuhi, kisha majaribio yatafuata na baadaye watakula chakula cha mchana kwenye ukumbi wa NSSF. Hiki kitafuatiwa na maandalizi ya urembo kwa ajili ya tukio la usiku huo.


Itakapofika takribani saa 2 usiku wageni watakaofurika kwenye ukumbi wa NSSF watapata fursa ya kujionea tukio kubwa na la kipekee katika jiji la Mwanza.

Kama ilivyokusudiwa, mchakato wa kumtafuta Balozi wa Mitindo wa REDD’S wa mwaka 2008 ulikuwa na mfululizo wa shughuli nyingi kuliko miaka ya nyuma.

Mshindi atatangazwa kwenye shindano la kumtafuta Mrembo wa Tanzania litakalofanyika jijini Dar es Salaam mwezi ujao.

No comments: